Nenda kwa yaliyomo

Kwemashai

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kwemashai ni kata ya Wilaya ya Lushoto katika Mkoa wa Tanga, Tanzania.

Katika sensa ya mwaka 2022 wakazi walihesabiwa 5,488 [1]. Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 5,649 waishio humo.

Kata ya Kwemashai inapatikana kilomita nne mashariki kwa Lushoto mjini baada ya safu ya mlima Kwemsani wenye minara ya simu. Upande wa kaskazini inapakana na msitu mnene wa magamba, upande wa mashariki imepakana na kata ya Gare na upande wa kusini imepakana na kata ya Ubiri.

Historia ya jina "Kwemashai" imetokana na kata hiyo kuwa na miti mingi aina ya Mishai, hivyo enzi za uundwaji wa vijiji watumiaji wa jina hilo waliita Kwemishai, lakini miti ya mishai ikiwa mikubwa sana huitwa mashai hivyo jina Kwemishai lilibadilika na kuwa Kwemashai.

Kata ya Kwemashai imetokana na uendelezaji wa kijiji cha Kwemashai ambacho kilikuwa sehemu ya kata ya Ubiri kujitegemea yenyewe.

Hali ya hewa ya Kwemashai ni baridi kali kipindi kirefu cha mwaka kutokana na kuwa nyanda za juu.

Wakazi wa kata ya Kwemashai ni Wasambaa ambao ndani yake kuna makabila madogomadogo kama: Wambugu, Wahea, Washee, Wazigua, Wapare. Lugha kubwa ya mawasiliano ni Kisambaa ikifuatiwa na Kiswahili.

Wasambaa ni wakarimu na wenye upendo kati yao na kwa wageni, pia ni wachapakazi.

Shughuli kubwa za kiuchumi ni kilimo (kahawa, miwati, mbogamboga, viazi, miwa na matunda), ufugaji wa bandani, biashara, uchanaji mbao, utalii, uchomaji mkaa na ufundi.

Huduma za kijamii zinapatikana kama shule ya msingi, shule ya sekondari, maduka ya bidhaa za nyumbani, mashine za kusagia nafaka n.k.

Miundombinu ni barabara za vumbi zisizopitika kipindi cha mvua, hakuna huduma za afya: wananchi hulazimika kuzifuata hospitali ya wilaya wanapoumwa ambapo ni umbali usiopungua kilomita sita.

Njia kuu za usafiri ni: miguu, pikipiki, taksi, daladala.

Kata yote imeunganishwa na nguvu ya umeme wa TANESCO mwaka 2013.

Kata ya Kwemashai ina taasisi za kitaaluma kama: Shule ya msingi Kwemashai, shule ya msingi Kirangwi, shule ya secondari Kwemashai.

Kata bado haina miundombinu ya maji safi na maji taka, wananchi hulazimika kutumia maji ya chemchem ambapo kipindi cha kiangazi baadhi ya maeneo hukumbwa na shida ya maji.

Kata pia ipo mbele kimichezo, ina timu mbili za mpira wa miguu ambazo ni Kahe FC na Mlimani FC ambazo ni maarufu wilaya nzima ya Lushoto na zinatumia kiwanja kimoja cha Kwelugogo. Kuna wachezaji mahiri waliowahi kuichezea Kahe FC kama Sanguue, Rudovick Michael, M'baharia, Mhando, Khalid Kacim, Husein Said, Michael Makamba, Maghuju(Agogo), Juma na wengine wengi.

Kata ya Kwemashai ina vitongoji kama Kwelugogo, Misalai, Magira, Kunguli, M`bambala, Kwegundi, Bara, Tamota, Kirangwi, Makungwi, Mgwagwarai, Kwemlua, Kwendaga, Kizungu, Mheza, Kwetongo, Kizaa.

Kwemashai kuna vivutio vya kitalii kama: Kivuga ambao ni mlima mrefu wa jimbo zima la Lushoto, mlima Kwemsani wenye kilele chenye mvuto mzuri, msitu mnene wenye wanyama kama: kima, mbega, fungo, paa, nguruwe mwitu, mwewe n.k.

Kuna miti mbalimbali yenye mvuto kwa wageni kama vile: Muomboa, N'kwati, Mvumo, Mkuyu, Muua, Mshihwi, Mnyasa, Bangwe, Ghai, Kulo n.k.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Kata za Wilaya ya Lushoto - Mkoa wa Tanga - Tanzania

Dule "M" | Gare | Hemtoye | Kilole | Kwai | Kwekanga | Kwemashai | Kwemshasha | Lukozi | Lunguza | Lushoto | Magamba | Makanya | Malibwi | Malindi | Manolo | Mbaramo | Mbaru | Mbwei | Migambo | Mlalo | Mlola | Mnazi | Mng'aro | Mtae | Mwangoi | Ngulwi | Ngwelo | Rangwi | Shagayu | Shume | Sunga | Ubiri


Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Tanga bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Kwemashai kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno.