Uzima wa neema

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Uzima wa neema au hali ya neema katika teolojia ya Kanisa Katoliki ni uzima wa juu kabisa unaoweza kupatikana ndani ya binadamu hapa duniani kwa neema ya Mungu, kwa stahili za Yesu Kristo na kwa miminiko la Roho Mtakatifu[1].

Ufafanuzi wa teolojia[hariri | hariri chanzo]

Kwa ufafanuzi zaidi, maisha ya Kiroho yanadai hali ya neema inayotia utakatifu, ambayo ni kinyume cha hali ya dhambi ya mauti. Kila mtu ana mojawapo kati ya hali hizo mbili, yaani ama anamuelekea Mungu kama lengo kuu, ama amepotoka mbali naye. Hakuna anayeweza kuwa na hali ya kimaumbile tu, kwa kuwa wote wanaitiwa lengo linalopita maumbile, yaani kumuona Mungu uso kwa uso na hivyo kumpenda kabisa. Lakini ili tuwe na maisha ya Kiroho haitoshi tuwe na neema inayotia utakatifu, kama vile mtoto aliyebatizwa, bali ni lazima tupigane na yale yote yanayoweza kutuangusha dhambini, na tuwe na juhudi halisi za kumlenga Mungu.

Tungeng'amua hali ya neema, tungeona kwamba si tu chanzo cha maisha matakatifu bali mbegu ya uzima wa milele pia. “Neema inayotia utakatifu ya mtu mmoja ni bora kuliko mema ya kimaumbile ya ulimwengu wote” (Thoma wa Akwino); kwa sababu neema hiyo ni mbegu ya uzima wa milele, ambao una ubora mkuu mno kuliko uzima wa kimaumbile wa kwetu na wa malaika. Ndilo linalotuonyesha vizuri kuliko yote thamani ya neema inayotia utakatifu, ambayo tunaipata katika ubatizo na kurudishiwa na kitubio ikiwa tumeipoteza. Kwa Wakatoliki ni muhimu tuthamini kweli neema hiyo ambayo Uprotestanti umeisahau, ukifuata wanafalsafa wengi wa karne XIV. Hatuwezi kujua thamani ya mbegu tusipojua kinachoweza kutokana nayo: ili tuthamini roho iliyosinzia bado katika mtoto, ni lazima tujue nguvu ya roho ya mtu aliyekomaa. Vilevile hatuwezi kuthamini neema inayotia utakatifu tusipozingatia ustawi wake kamili katika uzima wa milele.

“Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye, kwa maana tutamwona kama alivyo” (1Yoh 3:2), yaani si kwa kuzingatia mng'ao wa sifa zake katika viumbe (vile vinavyoonekana, pamoja na roho za watakatifu zinazojitokeza katika maneno na matendo yao), bali moja kwa moja jinsi alivyo. “Wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana” (1Kor 13:12). Mtume Paulo hakusema nitamjua ninavyojijua mpaka ndani; kwa sababu najifahamu kuliko wengine, lakini mimi pia sielewi yote niliyonayo ndani, k.mf. siwezi kupima uzito wote wa dhambi zangu. Mungu tu ananijua fika: yeye tu anaelewa kikamilifu siri za moyo wangu. Mbinguni nitamjua anavyonijua, moja kwa moja, pasipo kupitia kiumbe chochote wala wazo lolote la kimaumbile, kwa sababu hakuna wazo la namna hiyo linaloweza kumchora Mungu na ukweli wake usio na mipaka. Kila wazo la namna hiyo linazingatia sifa mojawapo ya Mungu (k.mf. wema). Mawazo hayo mbalimbali hayatoshi kutujulisha dhati yake, umoja usiogawanyika kamwe. Mawazo hayo yanahusiana na uzima wake wa ndani kama vile rangi saba za upinde wa mvua zinavyohusiana na mwanga mweupe ambao zinatokana nao. Hapa duniani sisi ni kama tumeona hizo rangi saba na sasa tunatamani kuona huo mwanga mweupe unaozisababisha. Kabla hatujaona umungu wenyewe hatuwezi kuona ulinganifu wa dhati wa sifa zake, hasa huruma isiyo na mipaka na haki isiyo na mipaka. Mawazo yetu kuhusu sifa za Mungu ni vipande tu vya sura nzima, ambavyo vinaleta picha ya Mungu isiyopendeza vya kutosha. Tukifikiria haki yake, inaonekana ni kali mno, na tukifikiria upendeleo wa huruma yake unaonekana kwenda kinyume cha haki. Tukitafakari zaidi tunakiri kuwa ndani ya Mungu haki na huruma ni kitu kimoja, hazitofautiani kweli. Tunaungama hivyo kwa hakika, lakini hatujaona ulinganifu wa dhati wa sifa hizo, kwa kuwa unadai tutazame umungu ulivyo, moja kwa moja, pasipo mawazo ya kimaumbile.

Mtazamo huo ndio uzima wa milele. Nani anaweza kueleza ukuu usiopimika wa furaha na upendo utakaokuwemo ndani mwetu kutokana na mtazamo huo? Upendo wa Mungu wenye nguvu na wa moja kwa moja, hivi kwamba hakuna lolote litakaloweza kuupunguza; kwa upendo huo tutamfurahia hasa Mungu kuwa Mungu, mtakatifu, mwenye haki na huruma pasipo mipaka, na tutaabudu mipango yote ya maongozi yake iliyolenga kufunua wema wake. Tutazama katika heri yake, alivyosema Mwokozi, “Vema, mtumwa mwema na uaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako” (Math 25:21,23). Tutamuona Mungu vile anavyojiona, ingawa hatutaweza kumaliza vilindi vya hali yake, vya upendo wake na vya uweza wake. Pia tutampenda anavyojipenda. Vilevile tutamuona Bwana wetu Yesu Kristo. Ndiyo heri ya milele yenyewe, mbali ya furaha ya ziada tutakayokuwanayo kwa kuwaona na kuwapenda Bikira Maria na watakatifu wote, hasa tuliowafahamu duniani.

Huo mtazamo wa moja kwa moja unapita uwezo wa kimaumbile wa akili yoyote, ya malaika na ya binadamu, kwa kuwa ungehitaji ulingane na ule wa Mungu. Basi, akili ya kiumbe inaweza kupata mtazamo huo kwa neema ya Mungu tu, ambayo ni kama kupandikiza chipukizi la mti bora katika shina la mti mwitu ili uzae matunda mema. Malaika na binadamu hawawezi kumjua na kumpenda Mungu kwa namna inayopita maumbile yao kabla hawajapandikiziwa neema inayotia utakatifu, ambayo ni kushiriki umungu, yaani uzima wa ndani wa Mungu. Neema hiyo tu, ikipokewa rohoni mwetu kama zawadi isiyolipika, itatuwezesha kutenda Kimungu, yaani kumuona moja kwa moja vile anavyojiona, na kumpenda vile anavyojipenda. Kwa maneno mengine, kushirikishwa umungu kwa vipawa vya akili na utashi kunategemea kushirikishwa umungu kwa roho yenyewe iliyonavyo.

Neema hiyo ikikamilika isiweze kupotezwa inaitwa utukufu, ambao unazitia akili za watakatifu wa mbinguni mwanga usio wa kimaumbile unaowawezesha kumuona Mungu, na unautia utashi wao upendo wa kumiminiwa unaowawezesha kumpenda wasiachane naye kamwe. Kwa ubatizo tumeshapokea mbegu ya uzima wa milele, kwa kupokea neema inayotia utakatifu ambayo inaleta uzima huo na upendo wa kumiminiwa unaokusudiwa kudumu milele. “Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, ‘Nipe maji ninywe’, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai… Yeyote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele, bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele” (Yoh 4:10,14). “Atakayekunywa maji hai ya neema yanayotolewa na Mwokozi hatatamani mengine, ila atatamani kuyapokea hayohayo kwa wingi zaidi... Lakini, tofauti na maji ya kawaida yanayoelekea chini, yale ya Kiroho yanapanda juu. Ni maji hai ambayo hayaachani kamwe na chemchemi yake na yanabubujikia uzima wa milele ambao yanatustahilisha” (Thoma wa Akwino). Hayo maji hai yanatoka kwa Mungu, ndiyo sababu yanaweza kurudi juu kwake. “Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe. Aniaminiye mimi, kama vile Maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake” (Yoh 7:37-38). Anayemuamini Mwokozi, anaweza kuchota katika chemchemi ya maji hai, si kwa ajili yake tu, bali pia kwa wokovu wa wengine. “Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele” (Yoh 3:36). Hatakuwa nao baadaye tu, bali kwa namna fulani anao tayari, kwa kuwa uzima wa neema ni mwanzo wa uzima wa milele. Kwa dhati ni uzima uleule wa Kimungu, ambao hapa chini umo ndani ya Mkristo kama mbegu na huko juu utachanua kikamilifu katika watakatifu. Ndiyo maana Bwana aliongeza, “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho” (Yoh 6:54). Ufalme wa Mungu umo ndani mwetu kama mbegu ya haradali, kama chachu itakayoumua donge lote, kama hazina iliyositirika shambani.

Tunawezaje kujua kama tumeshaupokea uzima huo unaokusudiwa kudumu milele? “Sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti… Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu” (1Yoh 3:14; 5:13). Yesu aliahidi, “Amin, amin, nawaambia: Mtu akilishika neno langu, hataona mauti milele” (Yoh 8:51). Kwa kuwa, liturujia inavyosema, “Ee Bwana, uzima wa waamini wako hauondolewi ila unageuzwa tu”, tena unastawi kikamilifu mbinguni tu. Hakika uzima wa neema hapa duniani ni mbegu ya utukufu, hivi kwamba kiwango kidogo cha neema inayotia utakatifu ni bora kuliko mema ya kimaumbile ya ulimwengu wote na ya malaika pia, kwa sababu kinahusu hali ya juu, yaani uzima wa ndani wa Mungu; kwa hiyo ni bora kuliko miujiza pia na ishara nyingine za nje za ufunuo. Uzima uleule unaopita maumbile, ndio unaopatikana duniani katika waadilifu na mbinguni katika watakatifu. Ni pia upendo uleule wa kumiminiwa, isipokuwa tofauti mbili kuhusu imani na tumaini: kwamba hapa chini tunamjua Mungu si kwa kumtazama mwangani, bali katika giza la imani ya kumiminiwa; halafu hapa chini, ingawa tunatumaini kuwa naye milele, tunaweza kupotewa naye kwa kosa letu.

Kwa mwanga huo tuelewe maisha yetu ya Kiroho yanavyotakiwa kuwa na kustawi yawe utangulizi wa kufaa kwa uzima wa milele. Ikiwa mfumo wa neema inayotia utakatifu, maadili ya kumiminiwa na vipaji vya Roho Mtakatifu unaulenga uzima wa milele, je haukusudiwi kulenga kwanza muungano wa hali ya juu na Mungu?

Neema inayotia utakatifu na upendo, vinavyotuunganisha na Mungu katika maisha yake ya ndani, ni bora, tena sana, kuliko neema za pekee (k.mf. kusema kwa lugha ngeni) ambazo ni ishara tu za kazi za Mungu lakini hazituunganishi naye (taz. 1Kor 12:28-13:13). Hali ya kuzama katika mafumbo haitokani na neema hizo za pekee, bali ni tunda la imani tuliyomiminiwa, ikiangazwa na vipaji vya akili na vya hekima. Hivyo inatokana na neema inayotia utakatifu, ambayo inaitwa pia “neema ya maadili na vipaji” na tunaipata wote katika ubatizo. Kwa kuwa neema hiyo kwa mfumo wake inalenga uzima wa milele, inalenga pia hali ile inayohitajika ili kupata mwanga wa utukufu. Hali hiyo ni upendo kamili pamoja na hamu kubwa ya kumuona Mungu ambayo kwa kawaida inatokana na neema ya kuzama katika mafumbo. Basi, kuzama humo si karama, bali ni hali ya juu iliyopo katika njia ya kawaida ya utakatifu, ingawa ni adimu kama ukamilifu. Kwa vile neema inayotia utakatifu inalenga uzima wa milele, inalenga pia kutuweka tayari kupata mwanga wa utukufu mara baada ya kufa bila kupitia toharani, ambako ni adhabu inayotokana na kosa lisilotakiwa pamoja na malipizi yasiyotosha. Ingekuwa kawaida kutakaswa katika maisha haya kwa kujilimbikizia stahili na kukua katika upendo, badala ya kutakaswa kisha kufa pasipo stahili yoyote. Utayari wa kupokea mwanga wa utukufu mara baada ya kifo unahitaji kwanza utakaso kamili unaolingana na ule wa roho zinazotoka toharani zenye hamu kubwa ya kumuona Mungu. Hamu hiyo imedhihirishwa na Mt. Paulo vizuri ajabu, “Katika nyumba hii twaugua, tukitamani sana kuvikwa kao letu litokalo mbinguni… twaugua, tukilemewa, si kwamba twataka kuvuliwa, bali kuvikwa… Basi yeye aliyetufanya kwa ajili ya neno lilo hilo ni Mungu, aliyetupa arabuni ya Roho” (2Kor 5:2-5).

Tukitaka kujadili vilivyo maisha ya Kiroho, hatupaswi kusahau vilele hivyo ambavyo tunajulishwa na Maandiko na kuelezwa na walimu wakuu. Hasa katika masuala hayo tunatakiwa kuzingatia watu si jinsi walivyo tu, bali wanavyokusudiwa kuwa. Tupumue hewa bora ya vilele vya juu, badala ya kuishia katika hali ya wastani ya binadamu. Heri watu wanaojaribiwa hata wanakuta hewa ya kuwafaa upande wa Mungu tu na kumuonea hamu kuu.

Uzima wa kimaumbile na unaopita maumbile[hariri | hariri chanzo]

Ili tuelewe mbegu ya uzima wa milele iliyomo ndani mwetu, tunatakiwa kuzingatia jinsi neema ya utakaso inavyoleta katika akili na utashi maadili ya kumiminiwa na vipaji saba vya Roho Mtakatifu. Maadili hayo na vipaji hivyo ndio utendaji wa muundo uleule wa Kiroho unaokusudiwa kustawi hadi tuingie mbinguni.

Kwanza tutofautishe ndani ya roho yetu yale yaliyo ya kwake kwa jinsi ilivyoumbwa, na yale ambayo ni zawadi tu ya Mungu. Hata umbile la malaika, ingawa ni roho tu, ni la chini kuliko neema inayotia utakatifu. Basi, umbile la binadamu lina pande mbili tofauti: wa kwanza unalingana na wanyama, ukiwa na hisi za nje (milango ya fahamu) na za ndani (ubunifu na kumbukumbu) pamoja na uwezo wa kupatwa na maono mbalimbali (hasa pendo na chuki, hamu na hofu, furaha na huzuni, hasira).

Juu yake, umbile letu lina upande mwingine unaolingana na malaika, ingawa ndani mwao una nguvu na uzuri zaidi. Upande huo wa roho unapita mwili, maana hauutegemei moja kwa moja, bali unaweza kudumu baada ya mwili kufa. Kutokana na umbile la roho upande huo wa juu tuna vipawa vya akili na utashi. Akili inajua si tu sifa za viumbe zinazohisikana (rangi, sauti n.k.), bali dhati zao na kweli zisizobadilika kama vile: “Hakuna kinachotokea pasipo sababu, na hasa pasipo sababu kuu, yaani Mungu”; “tunapaswa kutenda mema na kuepa maovu”; “timiza wajibu wako, liwalo na liwe”. Mnyama hatajua kamwe kweli hizo. Kwa kuwa akili inaweza kujua si tu yanayotupendeza au yanayotufaa bali pia maadili (k.mf. kwamba “ni afadhali kufa kuliko kusaliti”), basi utashi unaweza kupenda uadilifu, kuutaka na kuutekeleza kwa kutawala hisi na maono. Kwa akili na utashi mtu anafanana na malaika, ingawa katika maisha haya akili yetu, tofauti na ya malaika, inazitegemea hisi ianze kujua mambo. Akili na utashi vinaweza vikastawi visifikie kujua na kupenda maisha ya ndani ya Mungu, ambayo inapita maumbile ya malaika na ya binadamu. Hao wanaweza kumjua kimaumbile Mungu kwa nje, kutokana na mng'ao wa sifa zake katika viumbe, lakini haiwezi kuumbwa akili yenye nguvu ya kuyajua yaliyo ya Mungu tu: “Ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu” (1Kor 2:11).

Kumbe neema inayotia utakatifu inatuingiza katika hiyo hali ya juu ya ukweli na uzima inayopita maumbile yoyote, kwa kuwa inashiriki maisha ya ndani ya Mungu; ni hali ya Kimungu inayotuandaa tumuone milele anavyojiona na hivyo tumpende anavyojipenda. “Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu, mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao. Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho” (1Kor 2:9-10). Neema ya utakaso inayotuwezesha tuanze kuishi ndani ya Mungu, juu kuliko umbile la malaika, ni kama chipukizi la Kimungu lililopandikizwa ndani ya roho ili kuiinua isizae tu matunda ya kimaumbile, bali matendo yanayostahili uzima wa milele. Kupandikizwa huko kunapita miujiza inayojulikana na hisi. Kwa mfano, ufufuo unaurudishia mwili uhai wa kimaumbile, ndiyo sababu unaweza kujulikana na umbile letu; kumbe neema ya utakaso inaipatia roho uzima usio wa kimaumbile, ndiyo sababu hauwezi kuhakikishwa. Tangu sasa uzima huo wa neema unatutia maadili ya kumiminiwa na vipaji vya Roho Mtakatifu. Kama vile umbile la roho lina kipawa cha akili na vinginevyo, katika ngazi ipitayo maumbile neema ya utakaso inaleta rohoni maadili na vipaji hivyo ambavyo, pamoja na mzizi unaovisababisha, ndio muundo ambao tulijaliwa katika ubatizo na kurudishiwa na ondoleo la dhambi ikiwa tuliupoteza.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Kadiri ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki, No. 2000: "Sanctifying grace is an habitual gift, a stable and supernatural disposition that perfects the soul itself to enable it to live with God, to act by his love. Habitual grace, the permanent disposition to live and act in keeping with God's call, is distinguished from actual graces which refer to God's interventions, whether at the beginning of conversion or in the course of the work of sanctification". taz. [[1]]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Catholic Answers, Grace: What it is and What it Does
  • Catholic Teaching on Sin & Grace (Center for Learning, 1997), ISBN|1-56077-521-1
  • George Hayward Joyce, The Catholic Doctrine of Grace (Newman, 1950), ASIN|B0007E488Y
  • "Grace." The Catholic Encyclopedia. Vol. 6. New York: Robert Appleton Company, 1909.
  • Stephen J. Duffy, The Graced Horizon: Nature and Grace in Modern Catholic Thought (HPAC, 1992), ISBN|0-8146-5705-2
  • Vincent Nguyen, The Pauline Theology of Grace from the Catholic Perspective, ASIN|B0006S8TUY}
Christianity Symbol.png Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Uzima wa neema kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.