Uhuru wa nafsi
Uhuru wa nafsi ni hali kamili ya ndani ambayo mtu ameondolewa vifungo vyote vilivyomzuia asiwe mwenyewe kweli wala asitende anavyoona ni vema kutenda. Kadiri mtu alivyopatwa na vizuio vya namna hiyo hapo awali, anahitaji kupiga hatua nyingi ya ukombozi au uponyaji wa ndani, pengine kwa msaada wa watu wengine wanaoweza kumpatia ushauri nasaha.
Safari ya uhuru
[hariri | hariri chanzo]Ndani mwetu mambo mbalimbali yameunganika na kufanya kazi pamoja tuwe tulivyo. Hasa mwili na roho vimeunda kiumbe kimoja kizima, yaani binadamu. Sehemu ya kwanza, inayoonekana, ni mwili. Mwili wetu ni wa ajabu, lakini nafsi ni ya ajabu zaidi: kwa kumbukumbu tunashika yaliyopita na kwa ubunifu tunaweza kujichorea picha za mambo tusiyowahi kuyaona, pia kubuni vitu vipya. Kwa akili tunaweza kujua na kuelewa mambo mengi; akili inakusanya habari mbalimbali, inazipanga na kuzipeleka kwa utashi ili uchague na kuamua. Binadamu ni tofauti na wanyama wote hasa kwa sababu anaweza kuchagua au kukataa kitu chochote chema au kibaya, hata tunu za maadili na dini na hatimaye Mungu. Lakini je, hiari yetu ni kamili? Tuache kwamba pengine watu wanatumia nguvu tusitende tunavyotaka. Tunachohitaji kuona ni kama ndani mwetu mna mambo yanayopunguza uhuru. Neno hilo linaelezwa na kamusi kuwa “hali ya kutotawaliwa na mtu au nchi nyingine; hali ya kufanya mambo bila ya kuingiliwa”. Je, maneno hayo yanaridhisha? Kadiri ya elimunafsia, mtu huru hasa ni yule aliyekomaa, kwa kuwa ametimia katika umbile lake asizuiwe na chochote. Mtazamo huo wa kibinadamu unakamilishwa na ule wa imani unaoonyesha kuwa mtu huru hasa ndiye mtakatifu, yaani yule anayeongozwa na ukweli na upendo katika yote. Uhuru ni kazi. Maisha yetu yote ni safari ambayo tujifunze kuwa huru kweli kuanzia ndani. Hali hiyo haipatikani ghafla, wala kimuujiza, wala kwa kukua kiumri. Kutokana na dhambi ya asili tunakuwa huru polepole, na kwa sharti la kufuata hatua zinazotakiwa. Kulingana na bidii tunazozifanya, mara tunaweza kufaulu, mara tunakuja kushindwa, kama vile mambo tunayokutana nayo mara ni ya kufurahisha na kutia moyo, mara ni ya kukatisha tamaa. Safari hiyo ina matatu ya maana sana: 1. Uhuru kutoka vizuio. 2. Uhuru kwa ajili ya malengo. 3. Uhuru pamoja na wenzetu.
Vizuio vya uhuru
[hariri | hariri chanzo]Tuanze kuona vizuio vinavyotufanya tusiwe huru kabisa; lengo letu ni kutoka katika hali hiyo. Vizuio vya kwanza ni maelekeo ya silika tuliyorithi. Sisi ni watoto wa watu: hatukuumbwa moja kwa moja, bali kupitia wazazi. Tumerithi maumbile yao, na kwa njia yao tumerithi yale ya akina babu na bibi na ya wazee wa kale kabisa. Tutake tusitake, tangu tutungwe tunaelekea kuwa sawa nao katika mema na mabaya, hasa sawa na mmojawao kitabia. Vizuio vingine ni mazingira tunayoishi, yale tunayoyaona na tunayoyasikia kandokando yetu kuanzia utotoni. Huo pia ni mkondo unaotusukuma tutende namna fulani bila ya kupima na kuamua wenyewe kwa uhuru. Siku hizi mazingira yanategemea sana vyombo vya upashanaji habari ambavyo vinafanya ulimwengu mzima uwe kama kijiji kimoja tu, na utamaduni wake kuelekea kuwa mmoja. Uhuru wetu unapunguzwa pia na mazoea yetu ya kufanya mambo kadhaa, tena kuyafanya namna ileile. Hivyo tunaweza tukashindwa kujiuliza kama ni mema au mabaya ili tuyaache yakiwa mabaya. Tena uhuru wetu unapunguzwa na maono (kuogopa, kukasirika, kufurahi n.k.). Hayo ni hali za nafsi zinazoonekana kwa nje kupitia mwili. Ni maitikio yetu kwa mambo au watu fulanifulani ambayo hatuyaamui yatokee. Kinyume chake yenyewe yanatusukuma kutenda au kutotenda namna fulani. Maono hayo yanaonyesha tunathamini nini. Mbali ya mambo yaliyo katika upeo wa ufahamu wetu, ndani mwetu mna mambo tusiyoweza kuyafahamu kwa kuwa yamefichika kabisa kama katika kisima kirefu. Baadhi yake ndiyo asili ya matatizo ya nafsi yetu. Tusipoyakabili kwa ukweli na kuyatoa nje hatutapona. Kweli kuna mengi kuliko macho yawezayo kuyaona. Mifano ya vizuio vya ndani: 1. mambo ya ndani ambayo tunayatambua au la na ambayo yametokana na matatizo yasiyotatuliwa tuliyoyapata utotoni; 2. mazoea mabaya (majivuno, uroho, uasherati, uongo, ukaidi n.k.); 3. hali ya dhambi inayotutenga na Mungu; 4. kujisikia watu wasio na maana; 5. kujisikia wabaya sana, wenye makosa yote; 6. kuona haya kupita kiasi; 7. woga wa kujitokeza; 8. kuishi kijuujuu. Mifano ya vizuio vya nje: 1. haja za mwili (chakula, kinywaji n.k.); 2. hali ya afya (vilema n.k.); 3. masharti ya mazingira na jamii (sheria, mila, desturi, miiko n.k.); 4. kutegemea wakubwa kama watoto wadogo.
Kuwa huru kutoka vizuio
[hariri | hariri chanzo]Ili tuweze kuvishinda vizuio hivyo inatubidi:
- kuvitambua;
- kujikubali tulivyo;
- kutoridhika na uhuru tulionao tangu utotoni;
- kutojidanganya kuwa tutaweza kupata uhuru kamili kwa urahisi.
Tusiendelee kujitetea kwamba, “si kosa langu, ni tabia yangu, siwezi kujishinda, sitabadilika, nashindwa kujirekebisha, huyu simpendi, bahati mbaya n.k.” La sivyo tutabaki daima “watumwa wetu wenyewe”, na matokeo yake yatakuwa kama ifuatavyo:
- kujitafutia faida kwa ubinafsi. Matokeo yake ni kutojitolea kwa upendo, kutojenga urafiki halisi, kutokuwa na lengo maalumu nje yangu, kusababisha matatizo mengi katika mafungamano na wengine, kutamani mno kufaulu, kutambulikana na kutawala n.k.
- kuwategemea mno wengine. Matokeo yake ni kujifanya mnyonge ili kuhurumiwa na kubembelezwa, mara kujitafutia sifa, mara kuzikataa, kushindwa kuamua lolote n.k.
- kutafuta ukamilifu katika yote. Matokeo yake ni kutokubali makosa, hitilafu na kasoro (hata za afya), kuogopa mno kukosa, kujitetea daima, kukandamiza wengine, kutaka kuonekana mtakatifu, kuogopa mno hukumu za watu, kutoridhika na mambo ya kawaida n.k.
- kushikamana mno na sheria. Matokeo yake ni kujali sheria kuliko watu, kushikilia maoni hata kukataa ya wengine, kuwa mnafiki, mgumu, mkali, kutokuwa na huruma, kujisikia daima mdhambi asiyestahili huruma, kuhitaji kujitakasa kila wakati n.k.
- kuona mno haya. Matokeo yake ni kutojiamini, kuogopa kuhukumiwa, kukosa raha katika kundi, kuwa mpweke, kujifungia ndani zaidi na zaidi, kukauka, kukata tamaa, kushindwa kujieleza, kukosa moyo wa kusema ukweli n.k
Kama hatujatambua vizuio vya namna hiyo vinayotufanya watumwa, tukumbuke matukio yaliyopita, hisia zetu, mazoea yetu n.k. Tujiulize:
- mambo gani hasa yananizuia nisiwe mwenyewe?
- Kulingana na mazingira yangu mambo gani yanaweza kunizuia nisiwe huru kweli (nyumbani, kazini, mkutanoni n.k.)?
- Wanaonifahamu vizuri wananiona kuwa huru au la? Kwa nini?
- Nimefanya jitihada gani niweze kuwa huru zaidi?
- Uhuru wa ndani nitaupata wapi? Lini nimewahi kujisikia ninao?
- Nafahamu watu wenye uhuru wa ndani kweli? Kwa nini nawaona hivyo?
Kuwa huru kwa ajili ya lengo
[hariri | hariri chanzo]Miguu yako inakufaa nini usipojua njia ya kwenda mahali? Vifaa vyako vina kazi gani usipofahamu nyumba ipi unataka kujenga? Utajiri wa upendo wako una faida gani ikiwa hujaamua utauelekeza kwa nani? Ina maana gani kujitawala kwa kuyashinda yasiyokufaa (maelekeo au mazoea mabaya, vizuio n.k.) usipoelekeza uhuru wako kwenye wema fulani? Basi, baada ya kujikomboa kutoka utumwa wa nje au wa ndani, ni kazi yako kuulinda uhuru uliojipatia, usije ukatawaliwa tena kwa njia tofauti. Uhuru wako usikose lengo lenye maana na ukweli, ukingojea mambo yatokee yanavyotaka bila ya wewe kujishughulisha. Kinyume chake, utambue ubora wa kutekeleza uhuru kama changamoto inayostahili uipokee, ubunifu wa mambo mapya utakaojitokeza katika utendaji wa bidii, uwezo wa kujiamulia kadiri ya lengo jema. Uhuru ni fursa kubwa ya kujijenga sawasawa, kufuatana na tunu za maana, kutekeleza mpango kamambe kwa maisha yako, kuitikia wito toka kwa Mungu, kutambua uhuru unavyoundwa na [[wajibu wa kutumikia watu, kujitawala kwa bidii na bila ya kurudi nyuma ili uwe mwaminifu, kujali utu wako na dhamiri yako na kuweza kujitolea kadiri ya tunu unazozithamini bila ya kudai kitu. Fanya uamuzi wako wa msingi ambao uwe daima na kipaumbele katika maisha yako na kuongoza maamuzi mengine mengi madogomadogo. Uhuru wako usiwe tena kuchagua kati ya mema na mabaya, bali kuchagua mema yale yanayofaa zaidi kwa utu wako na wa wenzako. Kisha kutambua tunu za maisha yako, polepole utatambua pia kuwa chemchemi na msingi wake ni Mungu mwenyewe. Bila yake uko bado katika hatari ya kutofikia uhuru wa kweli, au kutoudumisha au kutochuma matunda yake. Uhuru wako utakamilika hasa kwa kuwajibika kwa wengine, kutokana na kuwathamini kama watu wanaostahili heshima na huduma yako. Hapo utakuwa macho kutambua wanayoyahitaji na utakuwa tayari kujitolea na ujuzi, mang’amuzi na vipawa ulivyo navyo bila ya kujali gharama (hata kama ni kutoa uhai wako) wala kurudi nyuma kwa lolote. Kielelezo cha uhuru huo ni Yesu, halafu mtume Paulo, aliyejichagulia tunu za maisha, halafu akajitoa mhanga kuzitekeleza. “Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi... Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu” (1Kor 9:19,22).
Kuwa huru pamoja na wengine
[hariri | hariri chanzo]Tukiongozwa bado na ubinafsi jitihada zetu hazitatosha kuondoa vizuio vyote vinavyotufanya tusifikie uhuru wa mtu aliyekomaa. Tutapata uhuru huo ikiwa tu tunafungamana vizuri na jumuia. Tutaupata pamoja na wale tunaoishi nao, tukithaminiana na kuongozana katika safari ya kuelekea uhuru wa kweli. Tusipopiga hatua hiyo ya lazima tutazidi kustawisha ubinafsi wetu na kuwa mzigo kwa jumuia. Ili kupata maendeleo ya kweli ni lazima tushirikiane na kufanya bidii jumuia nzima katika kufuata lengo maalumu la maisha, kadiri ya alama za nyakati na mahitaji ya jamii. Kwa ajili hiyo tuwe tayari kuungana na wengine kwa kuachana na mazoea ya ubinafsi, uvivu na starehe, na kwa kupokea mawazo yao katika kutekeleza mipango ya jumuia. Hivyo polepole tutajisikia “sisi”, tutaonja uzuri wa kuwa kitu kimoja na kushirikiana kikamilifu pamoja na kuheshimu uhuru wa kila mmoja.