Prometheus
Prometheus alikuwa mmoja wa miungu wa nasaba ya Watitani katika mitholojia ya Kigiriki. Alitazamwa kuwa mwana wa Iapetos na Clymene, hivyo alikuwa mjukuu wa Uranos. Kati ya miungu mbalimbali ndiye Prometheus aliyeumba binadamu.
Katika masimulizi ya Wagiriki wa Kale siku moja alimdanganya mungu mkuu Zeu; wakati wa sadaka alificha nyama nzuri iliyotakiwa kuchomwa na badala yake alitoa sehemu zisizokuwa na thamani, maana alitaka kuhifadhi nyama nzuri kwa ajili ya binadamu aliowahi kuumba. Hapo Zeu alikasirika, hivyo alikataa binadamu wasipate siri ya kutumia moto. Lakini Prometheo aliamua kuiba moto mbinguni na kuwaletea binadamu.
Zeu alikasirika akaamuru Prometheus afungwe kwa mnyororo kwenye milima ya Kaukazi. Kila siku alikuja tai aliyekula ini lake, ila wakati wa usiku ini lilikua upya, ili liliwe na tai siku iliyofuata. Prometheus alipaswa kuvumilia mateso haya miaka mingi hadi siku moja akaja shujaa Herakles aliyemwua tai na kumrudishia uhuru wake. Hatimaye Zeu alimsamehe akarudi katika baraza la miungu kwenye mlima Olimpos.
Masimulizi ya Prometheus yalipokewa na Waroma wa Kale ambako Prometheus alitazamwa mara nyingi kama mwalimu wa ubinadamu aliyekuwa chanzo cha elimu na sanaa. Baadaye hadithi zake zilijadiliwa katika sanaa, fasihi na falsafa ya Ulaya, hasa tangu zama za Mwangaza. Wengine walimchukua kama mfano wa maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayomwezesha binadamu kutawala mazingira asilia. Wengine tena walimchukua kama mfano wa kiburi cha binadamu katika kutafuta maendeleo kwa kila njia, bila kutaka kukubali hali yake kama kiumbe, hivi kwamba anaharibu mazingira na maisha kwa jumla.
Tovuti nyingine
[hariri | hariri chanzo]- Matini ya Hesiod kuhusu miungu, Theogony
- Hadithi ya miungu, Prometheus
- Hadithi ya Theoi, Pronoea
- GML, Prometheus Archived 2012-05-26 at Archive.today
- Encyclopedia Mythica, Prometheus Archived 20 Januari 2008 at the Wayback Machine.
- Messagenet, Prometheus Archived 10 Januari 2008 at the Wayback Machine.
- Prometheus, shairi la Noevel (Kifaransa) Archived 23 Julai 2012 at the Wayback Machine.
- Prometheus, shairi la Byron Archived 27 Februari 2015 at the Wayback Machine.