Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Maandamano dhidi za Shah mjini Tehran, mwaka 1979

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalitokea katika mwaka 1979 nchini Uajemi (Iran) (mwaka 1357 katika kalenda ya Kiajemi). Yalimaliza utawala wa kifalme wa Shah Mohamed Reza Pahlavi na kuleta dola jipya la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kiongozi mpya wa nchi alikuwa Ayatollah Ruhollah Khomeini, aliyerudi Iran katika Februari 1979 na kuwa kiongozi aliyekubaliwa na wananchi wengi. Katika kipindi cha miezi michache tangu kurudi kwake utawala wa Shah uliporomoka, viongozi wa awali waliuawa, kukamatwa au kukimbia nchi. Mwisho wa mwezi wa Machi 1979 wananchi wengi walipiga kura na kuchagua "Jamhuri ya Kiislamu" kama dola jipya. Katika mwezi wa Desemba katiba mpya ya Jamhuri ya Kiislamu ilikubaliwa katika kura ya wananchi.

Utangulizi[hariri | hariri chanzo]

Maandamao ya mwaka 1963 mjini Tehran

Tangu mwaka 1923 Iran ilitawaliwa na wafalme wa familia ya Pahlavi, walioona sababu ya matatizo mengi ya nchi, hasa udhaifu wake, katika utamaduni wa kidini na athira kubwa ya viongozi wa kidini. Hapo Shah Reza Pahlavi aliamua kufuata mfano wa Uturuki na kiongozi wake Kemal Atatürk. Mwana wake, Mohamed Reza Pahlavi, aliamua kuongeza kasi ya mabadiliko, hasa katika siasa ya "Mapinduzi Meupe" aliyotangaza maka 1963. Hatua zake kama unyangaji wa ardhi wa wenye mashamba mengi (iliyogawiwa kwa wakulima wasio na ardhi), haki ya kura kwa wanawake na upanuzi wa sheria ya kidola kulingana na sheria ya Kiislamu, zilisababisha upinzani wa sehemu za ulema na hasa kutoka Ruhollah Khomeini aliyekuwa mwalimu wa dini kwenye seminari za Qom. Upinzani ulikandamizwa, Khomeini alikamatwa na kufukuzwa nchini; alihamia kwanza Uturuki halafu tangu 1965 Iraki alipoendelea kufundisha huko Najaf.

Katia miaka iliyofuata, Shah aliendelea kuimarisha utawala wake lakini upinzani dhidi ya siasa zake za kiimla ulibaki.

Upinzani dhidi ya Shah[hariri | hariri chanzo]

Kulikuwa na mikondo tofauti katika upinzani dhidi ya Shah:

  • Chama cha Tudeh (Wakomunisti) kilikuwa na msingi kati ya wafanyakazi wa viwanda na tasnia ya mafuta, na pia kieneo hasa kati ya Waazeri wa Iran. Kulikuwa pia na Wakomunisti wengine waliofuata mwelekeo wa ukomunisti wa China (Maoist) wakijaribu kuendesha vita dhidi ya serikali.
  • Wafuasi wa vyama mbalimbali visivyo vya Kikomunisti, wala vya kidini walishirikiana katika National Front; kati ya viongozi wao alikuwepo Mehdi Bāzargān.
  • Mkondo wa tatu ulikuwa mkondo wa kidini, uliofanywa na ulama vijana kwenye seminari za Qom waliolenga kumpindua Shah; kati ya waanzilishi wao walikuwepo Ali Khamenei na Ali-Akbar Rafsanjani.

Changamoto ya miaka ya 1970[hariri | hariri chanzo]

Mnamo 1971 Shah aliamua kusheherekea miaka 2500 ya ufalme katika Iran kwa kualika wageni wa kimataifa kwa sherehe iliyogharimu pesa nyingi, akimrejelea mfalme Koreshi Mkuu pamoja na urithi usiokuwa wa Kiislamu, ilhali sehemu ya wananchi waliona njaa.

Tangu mwaka 1973 bei ya mafuta ililipuka duniani, na nchi zilizozalisha mafuta ziliongeza mapato yao. Asilimia kubwa ya mapato hayo ya nyongeza yalifika mikononi mwa familia ya Shah, hali iliyoongeza ukosoaji dhidi ya utawala wake. Tofauti kati ya maskini na matajiri wa Iran ziliongezeka. Mfumko wa bei na hatua za siasa ya serikali dhidi yake ulisababisha matatizo ya nyongeza kwa maskini kwenye miji waliongezeka kutokana na wafanyakazi kutoka vijijini waliowahi kuhamia mjini kwa shughuli za ujenzi. Pamoja na hayo, serikali ilianzisha chama kipya cha Rastakhiz kama chama cha kisiasa cha pekee, ambako kila raia alitakiwa kuwa mwanachama na kutoa michango yake. Hatua hiyo iliongeza upinzani, hasa baada ya umoja wa Vijana wa Rastakhiz kuanzisha kampeni dhidi ya "wahujumu uchumi", iliyolenga hasa wafanyabiashara wa bazari (masoko ya kidesturi).

Mwaka 1975 Shah alibadilisha Kalenda ya Kiajemi ya nchi yake, akianza kuhesabu miaka tangu Koreshi, hivyo nchi yote, mara moja iliruka kutoka mwaka 1355 ya Kiislamu kwenda mwaka 2535 ya kifalme. 1978 alipaswa kufuta kalenda mpya.

Tangu 1977 serikali ya Shah iliona shinikizo kutoka kwa Marekani ambako raisi Jimmy Carter alisisitiza umuhimu wa kuheshimu haki za kibinadamu na za kidmokrasia. Shah alijibu kwa kuongeza uvumilivu yake mbele ya ukosoaji na kuachisha kazi makamanda makali wa polisi ya kisiri.

Maandamano na upinzani wa 1978[hariri | hariri chanzo]

Kwenye Januari 1978 makala ilichapishwa katika gazeti la kiserikali iliyomkosoa vikali Khomeini. Nakala ilisababisha maandamano mjini Qom, ambako wanafunzi kadhaa waliuawa na polisi. Kufuatana na desturi ya Kishia, ibada za maombolezi yalirudia siku 40 baada ya kifo chao; sherehe hizo zilileta maandamano mapya ambayo yalisababisha tena vifo vipya. Hivyo, mwaka 1978 uliona mawimbi ya maandamano katika miji mbalimbali ya Iran.

Tabriz katika magharibi ya Irani ilikuwa mji wa kwanza ambako waandamanaji walishambulia sinema, vilabu, benki na vituo vya polisi hadi jeshi likapaswa kuingilia kati, ambako watu waliuawa.[1][2][3][4][5] Shah alifaulu kukusanya wafuasi wake pia; lakini kwenye 19 Agosti 1978 wapinzani wake walichoma sinema kote Iran walizoona kama mifano ya utamaduni wa kigeni na hasa moto wa mjini Abadan ilisababisha vifo 400 hivi; wapinzani walifaulu kusambaza uvumi kuwa moto ulianzishwa na polisi ya siri kwa kusudi la kuchafua upinzani, uvumi ulioaminiwa na wengi na watu maelfu waliaandamana tena. Kwenye mwezi wa Septemba Shah alipiga marufuku maandamano yote ,hata hivyo wengi walikuwako barabarani kwenye tarehe 8 Septemba; wanajeshi waliua angalau watu 88. Wafanyakazi katika viwanda vingi walianza kugoma na uchumi ulisimamishwa.

Kwenye mwezi wa Novemba Shah aliomba serikali ya Iraki kumfukuza Khomeini alipokaa Najaf alipopokea mara kwa mara wafuasi wake kutoka Iran. Khomeini alihamishwa Ufaransa alipokaa katika kijiji cha Neauphle-le-Château karibu na Paris. Shah alikuwa na tumaini kwamba pale angetengwa na wafuasi wake wa Najaf, lakini kinyume chake Khomeini aliweza kutumia uhuru wa kisiasa na miundombinu bora nchini Ufaransa kuongeza mawasiliano yake na wafuasi wake Iran na pia na vyombo vya habari vya kimataifa.

Katika mwezi wa Desemba maandamano yalipanuka zaidi, ilhali wapinzani walitumia mwezi wa Muharram katika Kalenda ya Kiislamu ambao ni mwezi mtakatifu kwa Washia wanaokumbuka hapo mateso ya imamu wao Hussein huko Karbala. Tarehe 2 Desemba zaidi ya watu milioni 2 waliandamana dhidi ya Shah na kudai kurudi kwake Khomeini kutoka uhamishoni.

1979: Ushindi wa mapinduzi[hariri | hariri chanzo]

Kurudi kwake Khomeini tar. 1. Februari 1979

Shah alishindwa kuamua mwelekeo wake dhidi ya upinzani. Alisita kutumia nguvu yote ya jeshi dhidi ya wananchi wake, akijaribu mara kwa mara kukubali wanasiasa wa upinzani alioona afadhali kuliko wengine; alifukuza mara kadhaa viongozi wa kijeshi na wa polisi alizoamini walijibu vikali mno; polisi haikuandaliwa kushughulika umati mkubwa, na wanajeshi walikiuwa tu na silaha kali ambazo mara nyingi hawakutakiwa kuzitumia. Kwa jumla Shah alipambana na ugonjwa wa kansa; tsrehe 16 Januari 1979 aliamua kuondoka nchini na kukabifhi shughuli za utawala kwa kundi la wanasiasa na wanajeshi.

Tarehe 1 Februari Khomeini aliwasili Tehran kwa ndege ya Kifaransa alipopokelewa na watu milioni. Katika hotuba yake ya kwanza alitangaza serikali kuwa bila haki na bila mamlaka akatanza kwamba angeteua serikali mpya karibuni.

Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  1. Hitilafu ya kutaja: Invalid <ref> tag; no text was provided for refs named Axworthy
  2. Hitilafu ya kutaja: Invalid <ref> tag; no text was provided for refs named Afkhami
  3. Hitilafu ya kutaja: Invalid <ref> tag; no text was provided for refs named Ritter
  4. Hitilafu ya kutaja: Invalid <ref> tag; no text was provided for refs named Pahlavi 2004
  5. Abrahamian (1982), pp. 510, 512, 513.