Nenda kwa yaliyomo

Ruhollah Khomeini

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Ruhollah Khomeini

Ayatollah Ruhollah Musawi Khomeini (Kifarsi: آیت الله روح الله موسوی خمینی‎) (* 24 Septemba 1902 mjini Khomein; 3 Juni 1989 Tehran) alikuwa kiongozi wa mapinduzi ya Uajemi ya 1979 na baadaye kiongozi wa kiroho wa Jamhuri ya Kiislamu ya Uajemi hadi kifo chake.

Masomo

Alizaliwa mnamo 1902 mjini Khomein katika Uajemi wa Kati katika familia ya Masayyid. Baada ya shule ya msingi aliendelea kusoma mafunzo ya kidini huko Qom kuanzia mwaka 1922 akawa mujtahid 1936 pamoja na cheo cha kidini cha Hodjatolislam. 1943 aliandika kitabu cha "Kašf al-asrār" (ufunuo wa siri) alikoeleza mafundisho yake juu ya serikali ya kiislamu na kudai kufutwa kwa ufalme wa Uajemi. Aliendelea kufundisha sharia ya Kiislamu kwenye chuo cha Qom.

Tangu miaka ya 1950 alikubaliwa kama ayatollah yaani mwalimu wa dini kwenye ngazi ya juu. Tangu mwanzo wa miaka ya 1960 alichaguliwa na Washia wengi kama mmoja wa marja, yaani vielelezo wa kidini wanaofaa kuigwa na Waislamu wengine.[1]

Uasi dhidi ya Shah

Khomeini aligongana na serikali ya shah (mfalme) mara ya kwanza 1963. Katika mahubiri kwenye nafasi ya sikukuu ya Ashura aliwaita wasikilizaji wake waanzishe mapinduzi na jihad dhidi ya "utawala wa wakosaji" akimaanisha familia ya kifalme bila kuwataja waziwazi. Alikamatwa na kufungwa jela kwa muda fupi, baadaye kufungwa kwake nyumbani. 1964 alifukuzwa nchini akahamia Irak alikokaa Najaf na kufundisha kwenye chuo cha Kishia. Sifa zake huko Uajemi zilikua na mahubiri yake yalisambazwa kwa njia ya kaseti.

Mwanzo wa mapinduzi 1978

Mwanzo wa mapinduzi ya Uajemi ulitokea 1978. Jeshi na polisi walivunja maandamano ya wanafunzi mjini Qom waliopinga makala dhidi ya Khomeini katika gazeti ya serikali. Vifo vya wanafunzi 80 vikaanzisha ufuatano wa maandaano mapya kwa sababu katika kawaida ya Shia kuna ibada za kukumbuka marehemu baada ya siku 40. Hivyo mazishi ya watu waliouawa yalifuatwa na maandamano siku 40 baadaye yaliyosambaa kote nchini. Kwenye maandamano haya vifo vipya vikatokea tena vilivyosababisha maandamano mapya yaliyoendelea kukua na kuvuta watu wengi walioonyesha upinzani wao kwa jumla dhidi ya serikali ya Shah. Haya yote yalisaidia kueneza jina la Khomeini kati ya Wajemi.

Khomeini alivyorudi Uajemi 1979 wakati wa kuwasili Tehran

Katika Oktoba 1978 Khomeini alifukuzwa katika Irak kwa sababu wakati ule Saddam Hussein alitafuta uhusiano mwema na jirani yake Uajemi. Kwa miezi minne Khomeini alipata kimbilio katika Ufaransa alikotembelewa mara kwa mara na wanahabari wa magazeti na TV ya magharibi walioeneza habari zake kote duniani.

Kurudi Uajemi na Jamhuri ya Kiislamu

16 Januari 1979 Shah mgonjwa aliondoka Uajemi iliyokuwa katika hali ya uasi na Khomeini alirudi nchini 1 Februari. Alipokelewa na mamilioni ya watu. Serikali ya mwisho wa Shah ikajiuzulu na katika muda wa mwaka moja Khomeini alibadilisha Uajemi kuwa Jamhuri ya Kiislamu alikokuwa na mamlaka ya juu kupitia halmashauri ya mapinduzi iliyoendesha shughuli za kusimamia serikali mpya na kufanya mabadiliko katika jeshi, polisi na mahakamani.

Khomeini alikaa mbali na taasisi kama serikali au bunge lakini aliongoza kupitia watu wengine na mara kwa mara kwa kuwahotubia wananchi. Aliishi katika nyumba ya binti yake mjini Qom na hakuondoka humo kila mtu alipaswa kumtembelea huko.

Wakati wa kutwaliwa kwa ubalozi wa Marekani katika Tehran na wanafunzi Waislamu pia baadaye wakati wa vita kati ya Irak na Uajemi Khomeini alifanya maazimio mengi yaliyofuatwa na serikali hata kama yeye mwenyewe hakuwa na madaraka rasmi.

Tarehe 14 Februari 1989 Khomeini alitoa fatwa yenye hukumu ya mauti dhidi ya Mwingereza Salman Rushdie mwandishi wa riwaya "Ayat ya kishetani" kwa sababu aliona kitabu hiki kukashifu imani ya Kiislamu.

Kifo na urithi wake

Khomeini aliaga dunia 3 Juni 1989 baada ya upasuaji katika hospitali ya Teheran.

Aliacha nchi iliyobadilika sana. Maskini wa Uajemi walimpenda na kumheshimu karibu sawa na maimamu wa imani ya Kishia. Tabaka za juu na katikati walikimbia nchini kwa jumla ni mamilioni ya watu waliondoka Uajemi kwa sababu ya mapinduzi ya Khomeini. Wataalamu na wenye elimu waliondoka pia kwa sababu uhuru wa vyuo ulibanwa sana. Haki za wakinamama zilibanwa walipaswa kuvaa nguo za hijabu wakazuiliwa katika nafasi mbalimbali walipoweza kufanya kazi wakati wa shah. Wapinzani wengi waliuawa au kufungwa jela.

Makala hii kuhusu mwanasiasa fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Ruhollah Khomeini kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
  1. https://www.britannica.com/biography/Ruhollah-Khomeini