Vita ya uhuru wa Marekani

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta

Vita ya Uhuru wa Marekani ilipiganiwa kati ya Uingereza na walowezi wa koloni zake 13 kwenye pwani la Amerika ya Kaskazini katika miaka 1775 hadi 1783. Jeshi la walowezi lililoongozwa na George Washington na wengine lilishinda jeshi la Dola la Uingereza kwa msaada wa Ufaransa. Koloni zikapata uhuru kama “Muungano wa Madola ya Amerika" au Marekani.

Sababu za vita[hariri | hariri chanzo]

Samuel Adams, kiongozi wa walowezi wakati wa uhuru

Vita lilitokea kutokana na kutoelewana kati ya Dola la Uingereza na walowezi wake katika Amerika ya Kaskazini. Uingereza ilikuwa hapa na koloni 13 zilizokaliwa na wahamiaji kutoka Uingereza penyewe.

Serikali ya London ilitawala maeneo haya kwa njia ya magavana na wanajeshi wake. Sheria zilitungwa London zilizokataza kuanzishwa kwa viwanda kwenye koloni na hivyo walowezi walilazimishwa kununua bidhaa nyingi kutoka Uingereza kwa bei za juu. Baada ya Vita ya miaka saba Uingereza ilihitaji pesa ikaongeza kodi kwa bidhaa zilizosafirishwa kati ya koloni na nchi mama. Walowezi hawakupendezwa na kodi za nyongeza walidai kupewa wawakilishi katika bunge la London na nafasi ya kushiriki katika maazimio juu ya sheria zilizowaathiri. Walitangaza wito la “no taxation without representation” (hapa kodi bila kuwakilihswa). Mwaka 1767 bunge la Uingereza lilikataa maombi ya wakoloni na badala yake idadi ya wanajeshi iliongezeka katika koloni.

Kwa sababu hizo wakoloni wengi walijisikia vibaya eti walidharauliwa wakaongeza ukali wa upinzani. Mwaka 1773 umati ya watu walishiriki katika tukio la “Boston Tea Party“ wakatupa mizigo ya majani ya chai kwenye bandari ya Boston kwa kuonyesha upinzani wao dhidi ya kodiy a Waingereza.

Waingereza walijibu 1774 kwa sheria kali mpya na wanajeshi wao walianza kukusanya akiba za baruti katika koloni. Hatua hii iliongeza uchungu na wanamigambo kati ya wakoloni walianza kufanya mazoezi ya kijeshi. Viongozi wao wakaitisha mkutano wa kwanza wa wawakilishi kutoka koloni zote (Connecticut, Delaware, Georgia, Maryland, Massachusetts, New Hampshire, New Jersey, New York, North Carolina, Pennsylvania, Rhode Island, South Carolina, Virginia) wakaamua kwa pamoja kukataa biashara yoyote na Uingereza kwa muda wa mwaka mmoja hadi madai yao ya kupunguza kodi yatakubaliwa pia wakaanza kufanya mazoezi ya wanamigambo bila usimamizi wa Waingereza. Lakini hadi sasa hawakulenga bado kutafuta uhuru.

1775 Waingereza walitangaza koloni ya Massachusetts kuwa eneo la waasi na sheria ya kukataza wavuwi kutoka Marekani kuvua samaki katika Atlantiki.

Mwanzo wa vita[hariri | hariri chanzo]

Jaribio la wanajeshi wa kifalme kukamata tena akiba za baruti kati ya walowezi lilisababisha mapigano ya kwanza ya kijeshi yaliyotokea tar. 19 Aprili 1775 karibu na mji wa Boston. Wanajeshi waingereza walikutana na wanamigambo kwenye kijiji cha Lexington na baada ya kipindi cha kutazamana risasi yalifyatuliwa; wanamigambo 8 waliuawa. Mapigano yalisamabaa pia kwenye vijiji vya karibu. Wanamigambo wengi walifika nje ya Boston wakawazuia Waingereza ndani ya mji.

Baada ya wiki mbili mkuu Mwingereza alijaribu kuwafukuza na mapigano ya Bunker Hill nje ya Boston yalitokea. Hii ilikuwa mapigano makubwa ya kwanza; waingereza walishinda lakini walipotea wanajeshi 226 waliouawa lakini wanamigambo walipotea wafu 140 pekee.

Vita na uhuru[hariri | hariri chanzo]

Sasa vita kamili ilisambaa. Mwanzoni Waingereza walikuwa na silaha na wanajeshi zaidi wakasogea mbele lakini wanamigambo ya walowezi wakioongozwa na George Washington waliendelea kuwashambulia.

Tarehe 4 Juli 1776 wawakilishi kutoka koloni zote zilitangaza uhuru wa Muungano wa Madola ya Amerika. Bado Waingereza walisogea mbele wakatwaa pia mji wa New York. Lakini tangu 1777 Ufaransa ilianza kwa siri kutuma silaha kwa Wamarekani; mwaka 1778 Ufaransa, Hispania na Uholanzi ziliungana na kutangaza vita dhidi ya Uingereza. Manowari za Ufaransa zilishambulia meli za Waingereza zilizopeleka silaha na askari kwenda Marekani.

Mwaka 1781 sehemu kubwa ya jeshi la Uingereza ilishindwa kwenye mji wa Yorktown ikalazimika kujisalimisha. Tangu siku hii mapigano yalipungua na mwaka 1783 Uingereza ukakubali uhuru wa koloni zake za awali.

Wakazi wengi wa koloni walioendelea kusimama upande wa Uingereza walihamia Kanada iliyoendelea kuwa koloni.