Nenda kwa yaliyomo

Kiwavijeshi wa Amerika

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Spodoptera frugiperda)
Kiwavijeshi wa Amerika
Mdumili wa kiwavijeshi wa Amerika (Spodoptera frugiperda)
Mdumili wa kiwavijeshi wa Amerika (Spodoptera frugiperda)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Lepidoptera (Wadudu walio na mabawa yenye vigamba)
Nusuoda: Glossata {Lepidoptera wenye ulimi unaoweza kuviringwa)
Familia ya juu: Noctuoidea (Nondo kama nondo wa nyanya)
Familia: Noctuidae (Nondo walio na mnasaba na nondo wa nyanya)
Nusufamilia: Hadeninae (Nondo wanaofanana na viwavijeshi)
Jenasi: Spodoptera (Viwavijeshi)
Guenée, 1852
Spishi: S. frugiperda
J.E. Smith, 1797

Viwavijeshi wa Amerika ni viwavi wa nondo Spodoptera frugiperda katika familia Noctuidae. Kwa kawaida viwavi hao hawatembei chanjari kama viwavijeshi wa Afrika lakini wadumili huhama mbali kubwa katika makundi makubwa.

Wakitoka mayai viwavi hao ni weupe wenye kichwa cheusi. Baadaye wanakuwa kijani wenye kichwa cha rangi ya machungwa. Hatua za mwisho ni hudhurungi au kijivu.

Mabawa ya mbele ya mdumili ni hudhurungi yenye madoa kahawia na meusi na yale ya madume yana doa moja jeupe kwenye ncha. Mabawa ya nyuma ni meupe yenye mlia mweusi pembezoni.

Viwavi hao hula zaidi ya spishi 80 za mimea lakini wanapenda sana nyasi na nafaka na pia mpamba. Mara nyingi hula ndugu zao mpaka kiwavi mmoja anabaki tu katika mmea mmoja. Wadumili hula mbochi.

Msambzo wa awali wa spishi hii ni Amerika kutoka majimbo ya kusini ya Marekani mpaka Amerika ya Kusini lakini inaweza kuhama kaskazini mpaka kusini kwa Kanada. Tangu 2016 nondo hawa wamewasilishwa katika Afrika ya Magharibi. Kisha walihama katika takriban nchi zote za Afrika kusini kwa Sahara. Siku hizi wanapatikana hata katika Uhindi na Sri Lanka.

Mzunguko wa maisha

[hariri | hariri chanzo]
Mayai

Mzunguko wa maisha wa kiwavijeshi wa Amerika unakamilika ndani ya siku 30 hadi 90 kulingana na nyuzijoto. Idadi ya vizazi ya nondo huyu inategemea hali ya hewa. Kwa sababu mabuu hawawezi kuingia kwenye diapause hawawezi kuishi wakati wa hali ya hewa baridi.

Kwa kawaida majike hutaga mayai takriban 1,500 katika maisha yao. Mayai hayo yana umbo la kuba na yana kipenyo cha mm 0.4 na urefu wa mm 0.3. Majike wanapendelea kutaga mayai kwenye upande wa chini wa majani, lakini ikiwa idadi ni kubwa watayataga takriban popote. Wakati wa hali ya hewa ya joto mabuu hutoka katika mayai ndani ya siku chache.

Kiwavi hatua ya sita

Viwavi hupitia hatua sita tofauti, zinazotofautiana kidogo katika mwonekano wa kiwiliwili na kilingo. Pamoja hatua zote hudumu siku 14 hadi 30 kulingana na nyuzijoto. Kiwavi aliyekomaa ana urefu wa takriban mm 38-51. Hii ni hatua ya maisha haribifu kabisa kwani viwavi wana sehemu za kinywa zinazokeketa. Kichwa kina muundo kama Y iliyopinduliwa juu ya paji. Kuna madoa manne meusi juu ya pingili ya nane ya fumbatio.

Mdumili wa kiume

Kiwavi wa hatua ya mwisho aliyekomaa huwa bundo chini ya ardhi kwa siku 7 hadi 37 katika kifukofuko anachounda kwa udongo na hariri. Muda wa kuishi kwa hatua ya bundo hutegemea nyuzijoto ya mazingira.

Baada ya kuibuka wadumili wanaishi siku 10 hadi 21. Jike hutaga mayai mapema kwa maisha yake. Wadumili hukiakia usiku na kufanya bora wakati usiku ni moto na mnyevu.

Uhamiaji

[hariri | hariri chanzo]

Wadumili wana uwezo wa kuruka mbali ndefu, kwa hivyo, ijapokuwa hawawezi kupita majira ya baridi kaskazini kwa eneo la kusini wa Marekani, nondo hawa wanaweza kuhama kaskazini hadi kusini mwa Kanada wakati wa miezi ya joto. Kiwango cha uhamiaji wao ni haraka inayoshangaza na kinakadiriwa kuwa km 500 kwa kila kizazi. Wanasayansi fulani wanadhani kwamba uhamiaji huu wenye kasi unasaidiwa na miendo ya hewa katika masi za hewa. Baada ya kuingia Afrika ya Magharibi mara ya kwanza mnamo 2016, spishi hiyo ilivuka kwenda Afrika ya Mashariki na ya Kusini ndani ya mwaka mmoja.

Lishe ya kiwavijeshi wa Amerika hujumuisha nyasi na mazao ya punje ndogo kama vile muhindi, lakini spishi hiyo imekumbwa kutumia mimea zaidi ya 80. Viwavijeshi walipata jina lao la kawaida kwa kula maada yote ya mimea wanayokutana nayo katika mitawanyiko yao, kama jeshi kubwa. Aina kadhaa za muhindi mtamu zina ukinzani kwa sehemu, lakini sio kamili, dhidi ya viwavijeshi. Ukinzani huo hutokana na proteasi ya kipekee ya kDa 33 ambayo muhindi huzalisha wakati unaliwa na viwavijeshi au lava wengine. Proteasi hii ilipatwa kupungua kwa kiasi kikubwa ukuaji wa lava wa kiwavijeshi.

Ulaji wa wenzake

[hariri | hariri chanzo]

Inapowezekana, lava atakula lava wa hatua ndogo zaidi. Uchunguzi wa 1999 ulionyesha kuwa ulaji wa wenzake unafaida kiwavi tu wakati chakula kingine ni chache. Licha ya hii viwavi watakula wenzake wakati wowote wanaweza, ingawa ilipatwa kupungua siha yao katika visa vingi. Sababu moja inayojulikana kwa nini ulaji wa wenzake ni hatari kwa kiwavijeshi wa Amerika ni kwa sababu ya uenezaji wa magonjwa kwa mlawenzake. Asilini athari hasi za ulaji wa wenzake zinaweza kusawazishwa na ukweli kwamba ulaji wa wenzake huondoa washindani na hivyo kufanya rasilimali zaidi kupatikana na kuongezeka siha ya viwavijeshi wa Amerika.

Wadumili

[hariri | hariri chanzo]

Nondo wapevu huchubuwa mbochi ya maua.

Udhibiti

[hariri | hariri chanzo]

Maadui ya asili

[hariri | hariri chanzo]

Kiwavijeshi wa Amerika ana maadui ya asili ambao wanaweza kupunguza idadi ya mdudu huyo. Wadudu mbuai hula viwavi. K.m. wadudu-kibibi na wadudu-koleo, lava na wapevu, hula mayai na viwavi wadogo wa hatua za kwanza hadi tatu. Sisimizi hula viwavi wa hatua zote. Mbawakawa wakimbiaji hula viwavi wanaojiangusha chini ili kuwa bundo. Ni muhimu kutokutumia dawa za kikemikali kwa wingi ili kuhifadhi maadui hawa na kuzuia mlipuko wa viwavi. Sisimizi hata wanaweza kuvutwa kwa kupulizia mimea maji na sukari au supu ya samaki. Sukari inavuta nyigu mbuai pia.

Wadudu wengine ni vidusia wa mayai au viwavi, nyigu vidusia hasa. K.m. nyigu wa jenasi Trichogramma na Telenomus hutaga mayai yao juu ya mayai ya nondo kisha lava huyala. Nyigu wa jenasi Chelonus, Campoletis na Cotesia hutaga mayai ao juu ya miili ya viwavi. Spishi za Trichogramma zinaweza kufugwa na kuachiliwa kwa wingi ili kupunguza idadi ya viwavi.

Viwavijeshi huambukizwa pia na pathojeni, kama vile virusi, bakteria na kuvu. Mifano ya virusi ni virusi ya granulosi ya Spodoptera frugiperda na virusi ya wingi ya polihedrosi ya kiina ya S. frugiperda. Kiwavi akiwa mgonjwa anapanda juu ya mmea wa lishe, kisha anakufa na mwili unapasuka ambayo inasababisha virusi kutoka na kunajisi majani. Viwavi wengine wakikula majani hayo wanaambukizwa na virusi.

Pathojeni aina za kuvu ni spishi za jenasi Beauveria na Metarhizium. Spishi moja ya bakteria, Bacillus thuringiensis, huzalishwa kama dawa ya kibiolojia inayoitwa Bt.

Dawa za kikemikali

[hariri | hariri chanzo]

Wakulima wengi hutumia dawa za kikemikali, kama vile Coragen, Dichlorvos, Match, Orthene, Profen, Prove na Voliam Targo. Dawa hizi huua haraka lakini kuua wadudu wengine pia pamoja na maadui wa kiwavijeshi.

Udhibiti wa kibiolojia

[hariri | hariri chanzo]

Kuna dawa kadhaa za kibiolojia ambazo zina Bt ndani yao, k.m. Dipel na Thuricide. Feromoni zinaweza kutumiwa ili kuvuta madume wa kiwavijeshi. Kwa kawaida hutumika katika mitego pamoja na karatasi yenye kunata na pengine katika vibao vilivyotiwa feromoni na dawa Dichlorvos.

Utafiti wa Kituo cha Kimataifa cha Fiziolojia na Ekolojia ya Wadudu (icipe) huko Nairobi umethibitisha kwamba spishi kadhaa za nyigu vidusia katika Kenya zinaweza kudhibiti viwavi hao kwa kiwango kikubwa kiasi wakiachiliwa kwa wengi baada ya kutuzwa katika kitovu maalum. Spishi hizo ni Trichogramma chilonis na Telenomus remus ambao wanaambukiza mayai na Cotesia icipe ambaye anaambukiza viwavi wachanga.