Mbawakawa mkimbiaji

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mbawakawa mkimbiaji
Calosoma planicolle
Calosoma planicolle
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Coleoptera (Wadudu wenye mabawa magumu)
Nusuoda: Adephaga
Familia ya juu: Caraboidea
Familia: Carabidae
Latreille, 1802
Ngazi za chini

Nusufamilia 33, 11 katika Afrika ya Mashariki:

Mbawakawa wakimbiaji ni mbawakawa wa familia Carabidae katika nusuoda Adephaga ya oda Coleoptera wanaoonekana mara nyingi wakikimbia. Wengi sana wa hao ni mbuai wa wadudu wengine. Kuna zaidi ya spishi 40,000 na karibu na spishi 2000 katika Afrika wa Mashariki. Mbawakawa-bastola wamo katika familia hiyo pia.

Maelezo[hariri | hariri chanzo]

Ukubwa wa wengi wa mbawakawa hao ni wa kati, kama mm 4-25, lakini spishi kadhaa ni kubwa hadi mm 70 (Carabus gigas) na nyingine ni chini ya mm 4. Kwa kawaida rangi yao ni nyeusi mwili mzima na mara nyingi yenye ng'ao ya kimetali kama kijani, buluu au zambarau. Wanaweza kuwa na madoa meupe au njano. Hata hivyo kuna spishi zilizo na rangi tofauti, kama kahawia, nyekundu, zambarau na shaba, mara nyingi kwa mwungano. Wana mandibulo kubwa zinazoelekea mbele kwa kuwa mbuai. Vipapasio vyao vina umbo la uzi na zina pingili 11. Miguu ni mirefu yenye trokanta kubwa za umbo la maharagwe. Mabawa ya mbele (elitra) ni magumu yenye mifuo ya kingoringori. Katika spishi kubwa zaidi, mara nyingi huunganishwa na kuzuia mbawakawa kuruka. Walakini, hata ikiwa hazijaunganishwa, mabawa ya nyuma au ya kurukia yanaweza kupunguzwa na kufanya kuruka kusiwezekane.

Lava ni warefu na wembamba. Wana sehemu za kinywa zinazojitokeza na jozi ya viambatisho vya mkia kama brashi ndogo.

Biolojia na ekolojia[hariri | hariri chanzo]

Mbawakawa wakimbiaji kwa ujumla hukiakia usiku. Wakati wa mchana wanajificha chini ya takataka za majani, magogo au mawe. Wakionekana walikuwa na uwezekano mkubwa wa kuhangaishwa. Hula wadudu wengine, nyungunyungu au konokono.

Wanajilinda dhidi ya mbuai kwa kutoa kioevu chenye harufu na ladha mbaya sana. Mbawakawa-bastola wamekamilisha hii. Kioevu chao kina kwinoni zenye sumu. Kabla ya kutolewa hizi huchanganywa kwa peroxide ya hidrojeni. Utendaji utokeao hufanya kiowevu kuchemka na shinikizo kukipiga kuelekea kwa mshambulizi.

Chakula cha lava ni kama wapevu kwa kawaida, lakini wale wa spishi chache hula mbegu.

Spishi zilizochaguliwa za Afrika ya Mashariki[hariri | hariri chanzo]

  • Anthia hexasticta
  • Bradybaenus opulentus
  • Calleida centralis
  • Calosoma planicolle
  • Cerapterus spp.
  • Cypholoba trilunata
  • Eccoptoptera cupricollis
  • Galerita procera
  • Pheropsophus spp., Mbawakawa-bastola
  • Psecadius eustalactus
  • Scarites spp.
  • Stereostoma stuhlmanni

Picha[hariri | hariri chanzo]