Sheikh Suleiman Takadir

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Sheikh Suleiman Takadir
Sheikh Suleiman Takadir, Mbutta Milando, John Rupia na Julius Nyerere. Waliowazunguka na silaha za jadi ni Bantu Group, kundi la vijana wa TANU lililokuwa linatoa ulinzi kwa viongozi wa TANU. Picha hii ilipigwa mwaka wa 1955.
Sheikh Suleiman Takadir, Mbutta Milando, John Rupia na Julius Nyerere. Waliowazunguka na silaha za jadi ni Bantu Group, kundi la vijana wa TANU lililokuwa linatoa ulinzi kwa viongozi wa TANU. Picha hii ilipigwa mwaka wa 1955.
Nchi Tanzania
Kazi yake Mwanaharakati
Baraza la Wazee wa TANU Sheikh Suleiman Takadir wa pili chini kulia, wa pili waliosimama Dossa Aziz, wa sita Julius Nyerere, wa saba John Rupia, wa tisa Said Chamwenyewe, anayefuatia Jumbe Tambaza, Mshume Kiyate.
Historia ya Tanzania
Coat of Arms of Tanzania
This article is part of a series
Uendo
Historia ya Zanzibar
Afrika Mashariki 1800-1845
Ukoloni
Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Mkataba wa Zanzibar-Helgoland
Mkwawa
Vita vya Maji Maji
Vita vikuu vya kwanza Afrika Mashariki
Tanganyika
Mapambano ya uhuru Tanganyika
Uhuru
Uhuru wa Tanganyika
Mapinduzi ya Zanzibar
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Julius Nyerere
Ujamaa
Tamko la Arusha
Vita vya Kagera
Ali Hassan Mwinyi
Benjamin Mkapa
Jakaya Kikwete
John Magufuli
Samia Suluhu Hassan

Tanzania Portal

Sheikh Suleiman Takadir alikuwa mwanaharakati mzalendo na mwanazuoni wa Kiislamu kutoka nchini Tanzania. Vilevile alikuwa mmoja kati ya watu wa awali walioshirikiana na Julius Nyerere katika harakati za kudai Uhuru wa Tanganyika. Pamoja na yote hayo, jina la Sheikh Suleiman Takadir halijapata kutajwa popote katika historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika wala katika historia ya TANU.

Hatajwi na hakupata kutajwa baada ya uhuru kupatikana mwaka 1961, wala haidhaniwi hata kama atakuja kutajwa au kukumbukwa na viongozi walio katika madaraka hivi sasa. Sheikh Suleiman Takadir hutajwa kila linapotokea jambo ambalo Waislamu huonekana wanadhulumiwa na serikali kwani ndiye aliyeweka agenda ya hali ya baadae ya Waislamu na Uislamu katika Tanganyika huru mwaka 1958.

Jambo hili alipolileta lilitishia kuigawa TANU kwa misingi ya dini katika wakati ambapo umoja wa Waafrika ulikuwa unahitajika sana. Mwaka wa 1958 TANU ilikuwa imeenea nchi nzima na tayari iko katika barabara ya kuelekea kuchukua madaraka ya ndani na kisha Tanganyika kupata uhuru wake kamili.

Historia yake katika siasa na TANU[hariri | hariri chanzo]

Sheikh Suleiman Takadir kwanza alikuwa "mwanazuoni kisha alikuwa Mwenyekiti muasisi wa Baraza la Wazee wa TANU kuanzia TANU ilipoundwa mwaka 1954 hadi "alipotoswa" mwaka 1958 kwa kosa la "kuchanganya dini na siasa. Sheikh Takadiri alishiriki vilivyo ndani ya Baraza la Wazee wa TANU katika kutayarisha safari ya Nyerere kwenda UNO mwaka 1955. Wapenzi wake katika harakati za kupigania uhuru walimpachika jina la utani wakimwita "Makarios," wakimlinganisha na Askofu Makarios wa Cyprus na Ugiriki aliyekuwa anapambana na ukoloni wa Waingereza wakati yeye alipokuwa anapambana na Waingereza katika ardhi ya Tanganyika. Sasa kwa kuwa Suleiman Takadir alikuwa sheikh na mpambanaji ndipo walimpa jina hilo la "Makarios" na kwa hakika jina hili lilimkaa, likamwenea vyema na yeye akalipenda.

Mikutano ya mwanzo ya TANU ilikuwa ikifanyika Mnazi Mmoja mbele ya baadaye ilipojengwa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima. Wakati ule pale palikuwa hakuna jengo lolote, palikuwa na kiwanja kitupu na ardhi ile ilikuwa mali ya Mzee John Rupia Makamu wa Rais wa TANU. Kiwanja hiki baaadaye Mzee Rupia aliwapa TANU na TANU wakaanzisha Chuo Kikuu pale mara baada ya uhuru. Mikutano ya kwanza ya TANU ikifanyika pale Mnazi Mmoja na kabla Nyerere hajapanda juu kwenye jukwaa kuzungumza na wananchi alikuwa kwanza anatangulia Sheikh Suleiman Takadir kusawazisha uwanja na kuwaweka wananchi tayari kumsikiliza kiongozi wao.

Kama alivyokuwa Nyerere, Sheikh Suleiman Takadiri alikuwa na kipaji cha kuongea. Leo hii huenda baadhi ya wasomaji wangu wasiamini lakini ukweli ni kuwa Sheikh Suleiman Takadir alikuwa kabla hajazungumza lolote alikuwa akipiga "fatha," wananchi wakaitika na kwa umoja wao wakasoma, "Surat Fatha," sura ya ufunguzi katika Qurani Tukufu, kisha Sheikh Takadir akaomba dua na wananchi wakawa wanaitika kwa pamoja, "Amin," Amin," "Amin." Baada ya hapo ndipo atapanda Nyerere na kuanza kuhutubia. (Picha za mwanzo za mikutano hii zipo na zilipigwa na Mzee Shebe ambae katika miaka ile ya 1950 alikuwa na studio yake Mtaa wa Livingstone na Kipata. Vilevile inaaminika ya kwamba Mzee Shebe ndiye mpiga picha wa kwanza wa TANU na Nyerere).

Sheikh Suleiman Takadir na huyu ndiye Nyerere kama alivyokuja kutambulishwa kwa watu wa Dar es Salaam na Sheikh Suleiman Takadir kwa mara ya kwanza mwaka wa 1954. Kabla ya hapo Nyerere alikuwa akijulikana na watu wachache katika TAA. Sheikh Takadir alimpenda sana Nyerere kiasi kuwa mwaka 1957 katika hotuba aliyotoa katika tafrija moja ya taarab Mtaa wa Mvita, alimwita Nyerere, "Mtume wa Afrika," aliyetumwa na Mungu kuwaokoa Waafrika. Maneno yale ya Sheikh Suleiman Takadir alikuwa kama anamtabiria Nyerere makubwa katika mustakabali wa Afrika, kwani miaka mingi baadaye Nyerere alikuja kusimama mstari wa mbele katika kuikomboa Afrika kutoka makucha ya wakoloni.

Nyerere akawa hapungui nyumbani kwa Sheikh Takadir Mtaa wa Swahili. Nyumba hii iko jirani na kilabu ya mpira ya Pan Africa. Kutembelewa na Nyerere pale nyumbani kwake ikapelekea baba mwenye nyumba, Jumbe bin Jumaa wa Digosi amuhamishe nyumba Sheikh Takadir asije kumponza kwani Nyerere alijulikana kama adui mkubwa wa Waingereza.

Kufukuzwa katika chama cha TANU[hariri | hariri chanzo]

Uswahiba wao ulikuja kuvunjika na watu wawili hawa wakawa mahasimu wakubwa, Sheikh Suleiman kafa hasemi na Nyerere na Nyerere kwa upande wake hakupata hata siku moja kumtaja Sheikh Takadir popote hadi anaingia kaburini. Inaaminika Sheikh Takadir alikufa kihoro baada ya kupigwa pande na TANU na wakazi wote wa Dar es Salaam na wanachama wa TANU kwa kosa la "kuchanganya dini na siasa." Wakati huo TANU ikiongozwa na Mufti Sheikh Hassan Bin Amir ilipitisha azimio la kupiga vita hisia zozote na chembechembe za Uislam ndani ya TANU. Hakika Uislam ulikuwa na nguvu ndani ya TANU lakini haukuachiwa uvuke mipaka kuwabagua wengine waliokuwa si Waislam.

Chanzo cha mtafaruku huu ni Uchaguzi wa Kura Tatu wa mwaka 1958. Waingereza waliweka masharti ambayo kwa hakika yalikuwa ya kibaguzi na yalifanya wananchi wengi wasiweze kukidhi sifa zilizowekwa za kuweza mtu kupiga au kupigiwa kura. Kulikuwa na sifa ya elimu, kipato na kazi ya kukubalika na kupiga kura kwa tabaka za rangi. Mpiga kura Mwafrika alitakiwa ampigie kura Mzungu, Muasia na Mwafrika. Masharti haya yalikuwa kisiki kigumu kwa uongozi wa TANU na wanachama wake kutimiza. TANU na viongozi wake wengi hawakuwa na hiyo elimu iliyokuwa ikitakikana wala kipato cha maana. Ili mtu asimame kama mgombea kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria au awe angalau mpiga kura ilibidi azikusanye sifa zote hizo mahali pamoja. Wapiga Kura na wagombea walitakiwa wawe na kisomo cha darasa la 10 au kipato cha pauni 400 kwa mwaka na kuwa na kazi ya maana. Waafrika waliokuwa na sifa hizi hawakuwa wengi katika TANU. Wengi katika TANU kama walivyokuwa wakipenda kujiita wenyewe walikuwa, "Baba Kabwela." Ikawa sasa ili TANU iweze kuweka wagombea ilibidi iwatafute watu nje ya uongozi wa TANU. Hapa ndipo lilipokuwa tatizo.

Ilibidi TANU sasa iwalete watu wenye sifa nje yake na wengi wa watu hawa walikuwa Wakristo waliosomeshwa na wamishionari. Jambo hili lilimkera sana Sheikh Takadir na wanachama wengi wa TANU kwa ujumla wao na kwa hakika TANU nzima hawakutaka kabisa kuingia uchaguzi ule kwa masharti yale waliyoyaona ya kibaguzi. Wanachama wa TANU walikuja na kauli mbiu isemayo, "Kuingia Kura Tatu ni sawa na kujipaka kinyesi." Ilikuwapo minong'ono kuwa Wakristo wataichukua nchi lakini kwa muda mrefu hofu hii ilizuiwa kwenye vifua hakuna aliyekuwa na ujasiri wa kulisema hilo waziwazi kwani jambo la dini lilikuwa mwiko mkubwa katika TANU. Ikawa tatizo lile la kushiriki kwa TANU katika Uchaguzi wa Kura Tatu lijadiliwe kwenye Mkutano Mkuu wa TANU wa mwaka 1958 uliopangwa kufanyika Tabora.

Mpinzani mkubwa wa Kura Tatu alikuwa Zuberi Mtemvu, Katibu Mwenezi wa TANU kwa wakati ule. Ukweli ni kuwa Kura Tatu ilitishia uhai wa TANU na zilikuwapo dalili za chama kumeguka pande mbili. Kulikuwa na uwezekano mkubwa sana kuwa Zuberi Mtemvu na Sheikh Takadir wangelikuwa upande mmoja na wangeweza kuja na chama kingine ingawa agenda zao zilikuwa tofauti. Mtemvu yeye alisimama kwenye Afrika kwa Waafrika na Sheikh Takadir kwenye Uislam. Sheikh Suleiman Takadir na baadhi ya wazee katika Baraza la Wazee wa TANU walikuwa wajumbe katika mkutano wa Tabora. TANU ilipiga kura kukubali kuingia kwenye Uchaguzi wa Kura Tatu na manusruna kura zifungane kati ya wale wanaounga mkono na wale waliokuwa wakipinga. TANU iliingia katika Uchaguzi wa Kura Tatu na ikapata ushindi mkubwa.

Hofu aliyokuwanayo Sheikh Takadir ilikuwa kuwa watu walioingia katika TANU kuchukua uongozi ni Wakristo. Sheikh Takadir alikuwa anajua nguvu ya madaraka waliyokuwa wanakabidhiwa akawa na hofu kama uongozi huu mpya utakuja kutoa haki kwa Waislam uhuru utakapopatikana. Sheikh Takadir alitaka uhakika wa hali ya baadae ya Waislam katika Tanganyika huru. Katika mkutano wa Halmashauri Kuu Makao Makuu ya TANU, New Street Sheikh Takadir alimkabili Nyerere akamshutumu kuwa hakuwa na nia nzuri na Waislam, atakuja wapendelea ndugu zake Wakristo katika Tanganyika huru. Sheikh Takadir akawageukia wenzake katika Baraza la Wazee wa TANU akasema, "Tuzibe ufa tusije tukajenga ukuta." Jambo lile lilikuwa zito. Nyerere alijiinamia na aliponyanyua uso wake machozi yalikua yanambubujika. Mkutano haukuweza kujadili jambo lile na kikako kile kikavunjika pale pale na wajumbe wakawatawanyika.

Sheikh Takadir akatoswa, kwani alikuwa amevunja mwiko mkubwa katika TANU. Mzee Iddi Tulio akachaguliwa kushika nafasi yake. Huku 'kutoswa na kutengwa na jamii ndiko kulikosababisha kifo cha Sheikh Takadir. Alikuwa hata akitoa salamu hakuna aliyeitika. Akienda sokoni Kariakoo kununua chochote kile hakuna aliyekuwa tayari kupokea hela yake. Haikuchukua muda mrefu Sheikh Takadir akaaga dunia. Kabla Sheikh Takadir hajafa TANU ilifanya mkutano mkubwa sana na Nyerere akamshambulia Sheikh Takadir kwa kutaka kuwagawa Watanganyika katika misingi ya dini.

[1]

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]