Mohamed Said
Mohamed Said | |
Nyuma wapili Bakari Saleh, mwisho kulia Ilunga Hassan Kapungu, Mstari wa mbele watatu kutoka kushoto Mwanahistoria - Mwandishi Mohamed Said. Hawa walikuwa baadhi ya vijana wa Kiislamu waliohudhuria Semina Dodoma Chuo Cha Biashara 1988. | |
Amezaliwa | 25 Februari 1952 Gerezani, Dar es Salaam |
---|---|
Nchi | Tanzania |
Kazi yake | Mwandishi, mwanahistoria |
Mohamed Said Salum (alizaliwa Gerezani, Dar es Salaam, 25 Februari, 1952) ni mwandishi na mwanahistoria kutoka nchini Tanzania. Ametunga vitabu mbalimbali, lakini anafahamika zaidi kwa kitabu chake cha "Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes" kilichotolewa kwa lugha ya Kiingereza kwa mara ya kwanza 1998. Baadaye kikatafsiriwa kwa Kiswahili na kutolewa tena mnamo mwaka 2002.
Maisha na kazi
[hariri | hariri chanzo]Sheikh Mohamed Said Abdallah alizaliwa mnamo tarehe 25 Februari katika mwaka wa 1952 huko Gerezani jijini Dar es Salaam - ambapo ndiko kulikokuwa na asili ya upinzani dhidi ya ukoloni wa Waingereza katika Tanganyika. Babu yake, Mzee Salum Abdallah Popo alikuwa muasisi wa harakati za vyama vya wafanyakazi na alikuwa mmoja kati ya watu wa awali kabisa kuanzisha upinzani na kuunga mkono hoja ya kupinga utawala wa kikoloni. Mwaka wa 1947, Mzee Popo aliongoza mgomo wa kwanza nchini Tanganyika katika majimbo ya kati nchi uliopangwa na wafanyakazi wa Tanganyika Railways.
Tanganyika ilipopata uhuru wake mwaka 1961, Mzee Popo aliachana na mkono wa Nyerere kama jinsi wengi walivyofanya na alitiwa kizuizini na serikali kwa ajili ya msimamo wake wa kuwa vyama vya wafanyakazi sharti viwe huru. Akiwa mwenyekiti wa Tanganyika Railways African Union (TRAU) alipinga vyama vya wafanyakazi kuwekwa chini ya Tanganyika African National Union (TANU) chini ya Rais Julius Nyerere.
Sheikh Mohamed Said ana shahada katika masuala ya Sayansi ya Siasa kutoka katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Vilevile ana Stashahada katika masuala ya Maritime Studies kutoka katika Chuo Kikuu cha Wales huko mjini Cardiff, Wales na nyingine ya BIMA kutoka katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha cha Dar es Salaam (IFM).
Utafiti juu ya historia ya uhuru wa Tanganyika
[hariri | hariri chanzo]Mohamed Said amefanya utafiti mwingi sana juu ya historia ya uhuru wa Tanganyika, historia ambayo kabla ya utafiti wake ilichukuliwa kama iliyohitimishwa na ameweza kufukua mambo muhimu ambayo yalifichwa katika historia iliyokuwa ikitambulikana rasmi.
Alianza kufahamika zaidi katika miaka ya themanini kupitia makala zake za kusisimua zilizokuwa zinahangaisha fikra za wasomaji kwa kufichua yale yaliyofichwam zilizoelezea mchango muhimu wa Waislamu na Uislamu katika harakati za kupinga ukoloni katika Tanganyika na khiyana waliofanyiwa Waislamu na serikali zote mbili, yaani, kabla ya uhuru na baada ya uhuru - jambo ambalo kwa wakati ule lilikuwa mwiko kufanyiwa utafiti au kuandikwa.
Makala hizo zilipata kuchapishwa katika magazeti na majarida maarufu barani Afrika na katika magazeti ndani na nje ya Tanzania. Baadhi tu ya makala zake za utafiti ni pamoja na "In Praise of Ancestors" (1988), "Africa Events (London), "Abdulwahid Sykes: Founder of a Political Movement" Africa Events - London (1988), "Islam and Politics in Tanzania" (1989), Al Haq Internation (Karachi), "The Plight of Tanzania Muslim" (1993) Change (Dar es Salaam) na "The Secular Unsecular State" (1995) Change (Dar es Salaam).
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]- Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes
- Sheikh Ilunga Hassan
- Sheikh Suleiman Takadir
- Abdulwahid Sykes
- Ally Sykes
- Azimio la Tabora
- TANU
- Titi Mohamed
- Ali Msham
Viungo vya Nje
[hariri | hariri chanzo]- http://www.mohammedsaid.com/ Ilihifadhiwa 5 Februari 2016 kwenye Wayback Machine.