Nenda kwa yaliyomo

Zubeir Mtemvu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Zuberi Mtemvu)
Zubeir Mtemvu
Kuanzia kushoto: John Rupia, Julius Nyerere, Zuberi Mtemvu. Waliosimama nyuma yao ni BANTU Group Vijana Walinzi wa Viongozi wa TANU.
Kuanzia kushoto: John Rupia, Julius Nyerere, Zuberi Mtemvu. Waliosimama nyuma yao ni BANTU Group Vijana Walinzi wa Viongozi wa TANU.
Nchi Tanzania
Kazi yake Mwanaharakati
Historia ya Tanzania
Coat of Arms of Tanzania
This article is part of a series
Uendo
Historia ya Zanzibar
Afrika Mashariki 1800-1845
Ukoloni
Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Mkataba wa Zanzibar-Helgoland
Mkwawa
Vita vya Maji Maji
Vita vikuu vya kwanza Afrika Mashariki
Tanganyika
Mapambano ya uhuru Tanganyika
Uhuru
Uhuru wa Tanganyika
Mapinduzi ya Zanzibar
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Julius Nyerere
Ujamaa
Tamko la Arusha
Vita vya Kagera
Ali Hassan Mwinyi
Benjamin Mkapa
Jakaya Kikwete
John Magufuli
Samia Suluhu Hassan

Tanzania Portal

Alhaji Zuberi Mwinshehe Manga Mtemvu[1] alikuwa mwanaharakati na mzalendo aliyeshiriki katika kupigania uhuru wa Tanganyika katika miaka 1950. Zuberi Mtemvu alikuwa kati ya wanachama wa mwanzo shupavu na msomi kabisa kujiunga na TANU na alikuwa mwanachama wa tatu kuacha kazi ya kuajiriwa ili akitumikie chama.[2] (Mwanachama wa kwanza kuajiriwa na chama alikuwa Alexander Tobias aliyeacha kazi na kuajiriwa na TAA wa pili alikuwa Mwalimu Julius Nyerere aliyeacha ualimu na kufanya kazi ya TANU na mzalendo wa tatu alikuwa Zuberi Mtemvu).

Mtemvu alikuwa akiishi Somali Street jirani na nyumba ya akina Sykes. Baba yake Mtemvu, Mzee Mwinshehe Manga Mtemvu, alikuwa amejenga nyumba yake nyuma ya nyumba ya Kleist Sykes. Kwa hiyo Mtemvu hakushikwa na mtu mkono kuingizwa TANU kwa kuwa hiyo mitaa ndiyo chimbuko la TANU. Mwalimu Nyerere alipokuja kufahamiana na Abdulwahid na Ali Sykes, Dossa Aziz, John Rupia na viongozi wengine wa TAA mwaka wa 1952, Mtemvu akawa mmoja wa watu wa mwanzo kuwa karibu na Nyerere.

Mtemvu alikuwa na kipaji cha kuzungumza kama alichokuwanacho Nyerere, halikadhalika alikuwa na kipaji cha kuweza kushawishi na kuwashirikisha watu katika harakati. Takriban mwezi mmoja baada ya kuundwa kwa TANU mwaka 1954, Nyerere na Mtemvu walikwenda kuifanyia kampeni TANU huko Morogoro ambako ndiko ilipokuwa asili ya ukoo wa Mtemvu. Baba yake Mtemvu, Mzee Mwinshehe, alikuwa ameongea na baadhi ya wazee wenzake kuhusu TANU mjini Morogoro.

Ijapokuwa Nyerere alijaribu kwa uwezo wake wote kuwafikishia watu ujumbe wa TANU matokeo hayakuwa mazuri. Mzee Mtemvu ana picha na nyaraka muhimu sana kwa mtafiti yeyote atakaye kufahamu kuhusu historia ya TANU na siku za mwanzo za Mwalimu Nyerere katika siasa. Katika barua ambayo Mtemvu alimwandikia Ally Sykes mnamo tarehe 15 Agosti, 1954 aliwaelezea watu wa kabila lake kama 'wagumu'. Inaaminika hii ndiyo ilikuwa safari ya kwanza kwa TANU kuanza kujitangaza hadharani. Ndani ya barua hiyo Mtemvu alimjulisha Ally Sykes kuhusu mwanachama mpya wa TANU, Ally Mwinyi Tambwe. Wakati ule Tambwe alikuwa Katibu wa Al Jamiatul fi Tanganyika. Mchango wake mkubwa ukiacha kuipa TANU uongozi wa wasomi ilikuwa kutumia ushawishi wake kwa mweka hazina wa Al Jamiatul Islamiyya Ali Jumbe Kiro kuruhusu fedha nyingi sana za jumuia hii ya Waislamu kutumika katika harakati za uhuru na hasa katika kufanikisha safari ya kwanza ya Mwalimu Nyerere kwenda Umoja wa Mataifa kudai uhuru wa Tanganyika mbele ya Baraza la Udhamini mwaka 1955.

Zuberi Mtemvu alikuwa kati ya watu wa mwanzo kabisa kufikisha chama kwa wananchi. Katika barua hiyo iliyomwandikia Ally Sykes, Mtemvu aliomba kadi mia mbili ili atafute wanachama. Kitu cha kufurahisha ni kuwa kadi ya Mtemvu ya TANU aliandikiwa na Ally Sykes hii ni pamoja na kadi ya Mwalimu Nyerere ambayo ni kadi namba moja. Jambo la kushangaza kuwa nyaraka hizi muhimu katika kumbukumbu ya nchi hadi leo hii bado zimeachwa katika mikono ya watu binafsi badala ya kuwa katika Makumbusho ya Taifa kama kielelezo cha historia ya Tanganyika.

Historia inaonesha kuwa Mtemvu alikuwa mmoja wa wazalendo waliotayarisha mkutano wa TANU wa kwanza uliofanyika Ukumbi wa Arnautoglo ambao haukuhudhuriwa na watu zaidi ya ishirini. Mkutano wa uzinduzi wa TANU ulihudhuriwa na kikundi kidogo cha takriban watu 20 miongoni mwao Julius Nyerere, Abdulwahid na Ally Sykes, Dossa Aziz, John Rupia, Mshume Kiyate, Makisi Mbwana, Jumbe Tambaza, Juma Waziri, Clement Mtamila, Rajabu Diwani, Schneider Abdillah Plantan, Marsha Bilali, Rashid Ally Meli, Frederick Njiliwa, Idd Faiz Mafongo, Idd Tulio, Denis Phombeah na wengineo.

Tangazo la mkutano huu lilichapishwa katika gazeti la Ramadhani Mashado Plantan Zuhra. Lau kama mwaka wa 1954 Mashado na Mtemvu walikuwa pamoja ndani ya TANU wote wakiwa wahamasishaji wakubwa wa umma miaka minne baadae walitupana mkono na Mwalimu Nyerere na kuanzisha vyama vya upinzani.

Kuanzisha chama cha upinzani[hariri | hariri chanzo]

Wanaonekana Zuberi Mtemvu (aliyeshika tama) aliyekuwa Katibu Mwenezi wa TANU akiwa na Sheikh Suleiman Takadir, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU na kushoto yake Mzee John Rupia Makamu wa Rais wa TANU wakiwa katika moja ya hafla za TANU katika tawi hilo. Rais wa TANU Mwalimu Nyerere haonekani amezibwa na John Rupia lakini mlinzi wake katika vijana wa BANTU Group anaoenakana amesimama karibu yake amevaa lubega.
Ofisi ya TANU Mtaa wa Jaribu Magomeni Mapipa kama ilivyokuwa ikionekana katika miaka ya 1950 ikiwa imezungikwa na wanachama wake.

Mtemvu akiongoza Congress na Mashado All Muslim National Union (AMNUT). Katika wanachama wa mwanzo katika TANU alikuwa Mzee Said Chamwenyewe. Huyu alikuwa mwanachama shupavu wa TANU na alikuwa karibu sana na Mtemvu na Mwalimu Nyerere.[3]

Mtemvu alipohama TANU kuunda chama chake cha upinzani, Said Chamwenyewe alitoka TANU na kujiunga na Mtemvu katika Congress. Umuhimu wa Chamwenyewe ni kuwa Msajili wa Vyama alipokataa kuisajili TANU kwa kisingizio kuwa haina wanachama, marehem Abdulwahid Sykes alimpa Chamwenyewe kitabu cha rejesta na kadi za TANU akamuomba aende Rufiji akatafute wanachama.

Katika TANU kulikuwa na kundi la wasomi wengi wakiwa wamezama sana katika nadharia za staili ya Fabian Society. Hawa fikra na kuchanganua mikakati ilikuwa zaidi kuliko kufanya vitendo vyenyewe. Kundi hili lilikuwa likiongozwa na Abdulwahid Sykes, Hamza Mwapachu na Mwalimu Nyerere. Halafu kulikuwa na kundi la wale waliokuwa hawaoni tabu kuandika mada na kufanya michanganuo ya fikra na mikakati lakini waliona ili TANU ifanikiwe wananchi wafundishwe na kuhamasishwa kupinga dhulma kwa dhahiri hata kama itakuwa kwa kufanya hivyo watakuwa wanavunja sheria za wakandamizaji. Huu ulikuwa uwanja wa Zuberi Mtemvu, Ally Sykes na Steven Mhando. Kwa ajili ya msimamo wao huu Waingereza wakawaita "wakomunisti". Taarifa za kijasusi za Waingereza zinamueleza Mtemvu kama "Mkomunisti, mtu asiyejali sheria".

Ilikuwa katika kipindi hiki cha Kuijengea TANU misingi imara ya uongozi ndipo Mwaimu Nyerere alimshauri Mtemvu aache kazi serikalini aajiriwe na TANU. Mtemvu alikubali ushauri ule na akaacha kazi. Mtemvu akawa Katibu wa kwanza wa TANU. Mtemvu akiwa Katibu Mwenezi alikuwa na kazi ngumu ya kuwashawishi na kuwashirikisha watu kujiunga na kusajili matawi ya TANU. Ili kampeni ya kuwaingiza watu ifanikiwe na ujumbe wake uwafikie wananchi ilibidi TANU ifanye mikutano ya hadhara. Kwa bahati mbaya serikali ikawa haitaki kutoa kibali cha TANU ili ifanye mikutano. TANU ilijikuta katika hali ambayo haiwezi kuwasiliana na watu kuwatayarisha katika harakati za kuhamasisha umma. Katika hatua kadhaa za ujasiri Mtemvu alifanya mikutano ya hadhara bila ya kupata kibali cha serikali.

Nyerere mtu wa hadhari hakutaka kuonekana anavunja sheria. Alifahamu kwamba vitendo kama hivyo vingesababisha matatizo kutoka serikalini. Jambo kama hilo lilikuwa sawa na kuikaribisha misukosuko bila sababu ambayo ingeathiri chama na uongozi wake wote. Nyerere, kama Rais wa TANU, alikuwa amepokea barua kadhaa kutoka kwa Chief Secretary, T. Griffith-Jones, kuhusu mikutano isiyokuwa na kibali aliyokuwa akiifanya Mtemvu. Lakini kwa hakika kwa TANU kunyimwa haki ya kuitisha mikutano ilikuwa sawasawa na kuifunga mikono. Hakukuwa na namna nyingine TANU ingeweza kufanya ili iwasiliane na watu. Kuacha kufanya mikutano TANU ingebakia dhaifu na harakati zingekufa. Mtemvu alikuwa akifahaamu kuwa serikali ilikuwa imedhamiria kabisa kuiua TANU ingali bado changa. Akiwa bado amenaswa katika kitendawili hicho cha 'kibali cha kufanya mkutano', Mtemvu alipata nakala ya mkutano wa 674 wa Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa ambayo Mwanasheria Mkuu, Gratten Below, alifafanua juu ya msimamo wa serikali kuhusu suala hilo. Mwanasheria Mkuu aliarifu kwamba watu wanaweza kuanza shughuli za chama mara tu maombi ya usajili ya chama cha siasa yatakapowakilishwa; na wanaweza kuendelea na shughuli za siasa mpaka majibu kutoka kwa Msajili Mkuu yamepokelewa kwamba tasjili imekataliwa. Uongozi wa TANU katika makao makuu ulisisimka kwa taarifa hiyo iliyofukuliwa na Mtemvu.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. TERRETTA, MEREDITH (2013). "From Below and to the Left? Human Rights and Liberation Politics in Africa's Postcolonial Age". Journal of World History. 24 (2): 389–416. ISSN 1045-6007.
  2. "Political Parties and Democracy in Tanzania (Dar Es Salaam University Press, 1994, 228 p.): Chapter 2: Political Parties in Tanzania: The Antecedent Political Parties". www.nzdl.org. Iliwekwa mnamo 2021-06-27.
  3. "Zuberi Mtemvu: Mzalendo aliyekuwa na msimamo mkali – Raia Mwema". web.archive.org. 2017-05-31. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2017-05-31. Iliwekwa mnamo 2021-06-27.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]