Nenda kwa yaliyomo

Mtaguso wa Firenze

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mtaguso wa Florence)

Mtaguso wa Basel, Ferrara na Firenze ulikuwa mtaguso wa 17 wa Kanisa Katoliki. Mikutano yake ilifanyika katika miji ya Basel, Ferrara na Firenze. Uliitishwa na Papa Martin V (1417-1431) mwaka wa mwisho wa uongozi wake ili kutekeleza shingo upande agizo la Mtaguso wa Konstanz la kwamba mtaguso ufanyike mara kwa mara.

Huko Basel

[hariri | hariri chanzo]

Mtaguso ulianza Basel (Uswisi) chini ya Papa Eugenio IV (1431-1447), ukiwa na maaskofu wachache kulingana na mapadri na walei wenye haki ya kupiga kura.

Ingawa mtaguso ulifaulu kupatanisha wafuasi wa Jan Hus na Kanisa, na kutoa sheria kadhaa za urekebisho kwa kibali cha Papa, baadaye ulianza kumshambulia yeye pamoja na makardinali, ukionyesha wazi wengi waliuona una mamlaka ya juu kuliko Papa, kinyume cha mapokeo.

Hapo Papa Eugenio IV aliuvunja halafu akauhamishia Ferrara (Italia) mwaka 1438, ulipokutanika tarehe 8 Januari 1438, bila ya kujali upinzani wa wale ambao walibaki Basel na kumchagua antipapa wa mwisho, Felix V.

Huko Ferrara

[hariri | hariri chanzo]

Huko Italia ulifika ujumbe mkubwa kutoka Konstantinopoli kwa ajili ya kurudisha umoja kati ya Kanisa Katoliki na Waorthodoksi.

Kati ya wajumbe 700 kulikuwa na kaisari na patriarki wa Konstantinopoli, walioogopa Waturuki watateka mji wao (kama ilivyotokea kweli tarehe 29 Mei 1453); hivyo walihitaji msaada wa Wakristo wenzao wa magharibi.

Ferrara iliachwa kutokana na uhaba wa majengo na hofu ya tauni.

Huko Firenze

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1439 mtaguso ulihamia Firenze ukafikia makubaliano ya kurudisha umoja (6 Julai 1439), ingawa uamuzi ukashindwa kutekelezwa kwa kiasi kikubwa kutokana na upinzani wa waumini wa Konstantinopoli.

Vilevile tarehe 22 Novemba 1439 yalifikiwa makubaliano na Waorthodoksi wa Mashariki wa Armenia na tarehe 4 Februari 1440 yale na Wamisri.

Hatimaye tarehe 24 Septemba 1443 mtaguso ulihamia Roma kwenye Laterano. Huko yalifikiwa makubaliano ya kurudisha umoja na Wasiria kadhaa (30 Aprili 1444) na Wakaldayo na Wamaroni wa Kupro (7 Agosti 1445).

Hakuna hati kuhusu mwisho wa mtaguso. Lakini waliobaki Basel na kujitenga na Papa, kufikia tarehe 19 Aprili 1449 walimkubali Papa Nikolaus V na siku sita baadaye walifunga mkutano wao.

Mtaguso huo ulichochea Wakristo wa magharibi kutamani mawasiliano na wenzao wa Ethiopia na India, jambo lililowafanya waanze zile safari za mbali kupitia baharini zilizowafikisha Afrika Kusini na Mashariki, China na Amerika.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mtaguso wa Firenze kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.