Nenda kwa yaliyomo

Kichomi (diwani)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kichomi ni diwani au mkusanyiko wa mashairi ya mwandishi Euphrase Kezilahabi kutoka nchini Tanzania. Kitabu kilitolewa mwaka 1974.

Diwani hii inaakisi mawazo ya kizazi kipya cha washairi wasomi waliofuzu kutoka kwenye vyuo vikuu miaka ya 1970. Mawazo ya mshairi yaliyomo katika mashairi haya ni mawazo ya kisasa, ni mawazo ya kijana aliyezungukwa na mazingira ya kisiasa, kielimu, kijamii na hata kidini.

Kwenye utangulizi wa diwani hii, mshairi anaeleza kuwa katika sehemu ya kwanza anayoiita mashairi ya mwanzo ameandika juu ya mambo mbalimbali ikiwemo dini, siasa, utamaduni, ndoa na uchumi; lakini katika sehemu ya pili aliyoiita Fungueni mlango, wazo moja hasa lilimsumbua: swali linalohusu maana ya maisha ambalo liliukera moyo wake, akaona bora aandike kuwauliza wenzake.

Shairi la kwanza "Jinamizi" linatalii dhamira ya dhuluma barani Afrika. Siasa za Afrika zimekoleza msingi wa dhuluma. Kuna aina mbili za ukoloni: ukoloni mkongwe unaowakilishwa na watu weupe kwenye mtumbwi na ukoloni mamboleo unaowakilishwa na watu weusi kwenye mtumbwi. Jazanda ya mtumbwi inawakilisha nchi za Afrika. Samaki baharini ni wananchi wazalendo, majitu yenye meno ya kutisha ni wakoloni wa kisasa na mabepari wanaoendelea kulifyonza bara la Afrika. Kupitia kwa tashtiti na kejeli mshairi anaudhihaki 'utawala wa chuma' yaani utawala wa kimabavu. Mamba wanasimamia wakombozi ambao baada ya mapinduzi wanawasaliti wananchi wenzao. Hapa sanaa ya ushairi inatumiwa kama jukwaa la kutetea haki ya mnyonge katika jamii. Hata hivyo, mwelekeo na tuni inayotawala kwenye shairi hili ni ile ya utamaushi na udhanaishi. Mshairi amekata tamaa kuhusu suala la uhuru barani Afrika. Baada ya uhuru ukoloni unaendelea Afrika kwa misingi na sura mpya.

Shairi linalofuatia ni "Upepo wa Wakati". Kwenye shairi hili mshairi anatuchorea taswira ya ziwa lililochafuka, kuna mawimbi yanayopanda na kushuka. Taswira hii ni ishara inayosimamia maisha ya binadamu duniani. Istiara kuu inayotumiwa hapa ni maisha ni bahari iliyochafuka. Maisha ya binadamu hudhihirisha hali ya ufanisi na shida kadri tunaposhuhudia msukumo wa wakati. Dhana ya wakati kuwa upepo mkali unaosukuma na kuyumbisha vyote duniani inajitokeza. Mshairi anazingatia suala la tamaa na ubinafsi ambalo tunalishuhudia kwenye uwanja wa siasa. Viongozi barani Afrika hunyakua madaraka na kupokezana madaraka kwa zamu kama mzamaji anayeshika mguu wa rafikiye. Isitoshe, mshairi anakashifu pupa na kuthamini hela kuliko utu kwa kutumia mfano wa watu wanaopakata pesa kama mtoto. Mwandishi anatoa onyo kwa viongozi wanaowanyamazisha wanyonge kwamba watapanda na kushuka kama bahari inayoyumbishwa na upepo mkali wa wakati. Kama ilivyo kwenye mashairi mengi ya diwani hii mshairi amekata tamaa kuhusu maisha kwa jumla na hasa jinsi siasa inavyoendeshwa barani Afrika. Mshairi anayaona maisha kama ziwa au bahari iliyochafuka na dunia kama uwanja wa fujo.

Wimbo wa Mlevi:

Kama Mungu angewauliza wanadamu
Wanataka kuwa nani kabla ya kuzaliwa,
Hilo ndilo lingekuwa swali gumu maishani.
Na watu wangeishi kujutia uchaguzi wao.
[…]
Wote wangetamani kuwa kinyume cha walivyo.
Sijui nani angekuwa nani.
Lakini mimi mlevi ningependa kuwa ye yote
[…] (uk. 64)

Nimechoka:

[…]
Ninaendelea kuning’inia kama picha iliyotundikwa
Katika shamba la mawele, na mwenye shamba
Huvuta waya kutoka nyumbani, itingishike kuwatisha ndege.
[…]
Sauti ya baba inasema kwa msisitizo
“Najua utafika wakati itakulazimu kudondoka,
Lakini endelea kushikilia hiyo waya
Kama unazo nguvu bado, na usikate tamaa,
Ila usitegemee kusifiwa au kusaidiwa,
Vichwa vyote hivi vilidondoka kutoka umbali huo,
Nawe kudondoka, utadondoka!
[…] (uk. 34-35)
Makala hii kuhusu kitabu fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kichomi (diwani) kama Mwandishi wake, hadithi au matoleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.