Abdallah Rashid Sembe

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Abdallah Rashid Sembe
Picha ya Abdallah Sembe katika gazeti la Rai mnamo Juni 17-23 1999​.
AmezaliwaAbdallah Rashid Sembe
1912
Amekufa22 Mei, 1999
Kazi yakeMwanaharakati, mwanasiasa
Historia ya Tanzania
Coat of Arms of Tanzania
This article is part of a series
Uendo
Historia ya Zanzibar
Afrika Mashariki 1800-1845
Ukoloni
Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Mkataba wa Zanzibar-Helgoland
Mkwawa
Vita vya Maji Maji
Vita vikuu vya kwanza Afrika Mashariki
Tanganyika
Mapambano ya uhuru Tanganyika
Uhuru
Uhuru wa Tanganyika
Mapinduzi ya Zanzibar
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Julius Nyerere
Ujamaa
Tamko la Arusha
Vita vya Kagera
Ali Hassan Mwinyi
Benjamin Mkapa
Jakaya Kikwete
John Magufuli
Samia Suluhu Hassan

Tanzania Portal

Sheikh Abdallah Rashid Sembe (1912 - 22 Mei, 1999) alikuwa mwanaharakati na mzalendo aliyeshiriki katika kupigania uhuru wa Tanganyika katika miaka ya 1950. Vilevile alikuwa mwenyekiti wa TANU jimbo la Tanga. Huhesabiwa kama shujaa wa Azimio la Tabora lilofanyika kuanzia tarehe 21-26 Januari, 1958.

Maisha, mchango wake katika uhuru wa Tanganyika, TANU Tanga[hariri | hariri chanzo]

Maisha ya Tanga na uhodhi wa ukoloni, TAA hadi TANU[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1955 Sheikh Abdallah Rashid Sembe alikuwa akijishughulisha na biashara ya kuuza nazi katika soko la Ngamiani mjini Tanga. Hali ya siasa katika jimbo la Tanga ilikuwa ni ya kipekee kabisa ukilinganishwa na jinsi hali ilivyokuwa sehemu nyingine za Tanganyika. Ilikuwa ni Tanga tu katika historia ya Tanganyika kuwa dhana mpya ya siasa zaidi ya ile hali kukubali kila jambo la Waingereza, hali hii iliongezeka katika uhusiano baina ya Waafrika na watu wa rangi nyingine.

Katika jimbo la Tanga kwa bahati mbaya sana Uarabu ulichukua nafasi ya tabaka la utawala juu ya Waafrika. Dhana hii ilitiwa nguvu na wakoloni ili kuwagawa wananchi na kuwakandamiza Waafrika. Hiki kilikuwa kitu ambacho Waafrika walikuwa hawajapamba nacho. Kwa zaidi ya karne moja walikuwa wamezoea ubwana wa Waingereza. Uongozi wa siasa kupitia African Association ulikuwa chini ya watu waliojinasibu kuwa asili yao ni Uarabu zaidi kuliko Uafrika ingawa wengi wao walikuwa na damu ya Kiafrika. Katika hali kama hii African Association Tanga haikuwa na nguvu ya kuwaunganisha wananchi kupambana na ukoloni kama ilivyokuwa sehemu nyingine. Mara chache sana watu waliihusisha ofisi ya TAA Tanga na siasa. Ofisi ya TAA inakumbukwa na kuhusishwa na mahakama ya kadhi ambako kadhi Sheikh Ali bin Hemed alihukumu jamii ya Waislamu kwa kutumia sharia.

Mwaka wa 1875 The Universities' Mission to Central Africa (UMCA) ilikuwa imehama kutoka Mkunazini Zanzibar kwenda Magila katika Jimbo la Tanga. Ukristo ulianzishwa na kustawi katika nchi ya Wabondei, na vivyo hivyo nafasi za elimu kwa watoto wa Wabondei ambao wengi walibatizwa katika lile wimbi la kuwania nafasi za elimu. Jimbo la Tanga likabarikiwa na kuwa na Waafrika walioelimika sana. Vijana wengi kutoka Ubondei waliingia Chuo Kikuu cha Makerere na siasa za kizalendo zilizoanza baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Wabondei walikuwa wamejaa katika utumishi wa serikali ya kikoloni. Katika hali kama hii ingelitegemewa kuwa hawa wasomi wa Makerere ambao wengi walikuwepo pale Tanga mjini wakifanya kazi wangetoa uongozi katika African Association na kuanzisha harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.

Vuguvugu kutoka kwa wanaharakati wasoelimu, kutokea kwa Sembe[hariri | hariri chanzo]

Hawa Waafrika wasomi kutoka shule za misheni na Makerere badala ya kuwa wapigania haki wakawa watiifu kwa taasisi mbili zenye nguvu, serikali ya kikoloni na Kanisa. Wasomi hawa waliunda vikundi vyao kwa kushawishiwa na Waingereza vilivyokuwa vikijulikana kama Discussion Groups yaani vikundi vya majadiliano. Vikundi hivi vilijitenga na siasa. Kwa ajili hii basi, ilibakia kwa Waafrika "wasiokuwa na elimu" kuunda TANU na kuongoza harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Hapa ndipo unakutana na Shekh Abdallah Rashid Sembe.

Mikutano ya awali ya kisiasa na kutafuta wanachama wa TANU, Tanga[hariri | hariri chanzo]

Kikundi cha wafanyabiashara wadogo wadogo katika soko la Ngamiani, Abdallah Rashid Sembe akiwamo kiliitisha mkutano katika ukumbi wa Tangamano Septemba 5, 1955. Waliohudhuria mkutano huo walikuwa Abdallah Rashid Sembe, Hamis Heri, Peter Mhando, Mohamed Kajembe, Tuwa Abdallah, Dhili Mgunya, Victor Mkello, Mohamed Sadik, Hassan, Peter Ramadhani Jembe na Ali Mohamed. Peter Ramadhani tayari alikuwa mwanachama wa TANU huko Arusha na alikaribishwa mkutanoni ili waasisi wa TANU wanufaike kutokana na uzoefu wake.

Wasomi wa Makerere, uongozi wa TAA na Mwalimu Kihere mmoja wa wanasiasa wa wakati ule hawakuwepo kwenye mkutano huu muhimu. Mkutano ulifunguliwa na Hamis Heri na ulifungwa kwa uamuzi kuwa mkutano mwingine wa kuchagua viongozi wa chama ufanyike tarehe 23 Oktoba. Mkutano uliamua vile vile kuwa juhudi zifanyike kupata wanachama wengi iwezekanavyo. Kiasi kidogo cha fedha kilikusaywa na Harir Omari Siagi alipewa aende makao makuu ya TANU, Dar es Salaam kununua kadi sabini za TANU. Abdallah Rashid Sembe alikuwa mmoja wa wanachama wa mwanzo wa TANU.

Tarehe 23 Oktoba, wanachama wa mwanzo wa TANU huko Tanga walikutana kuchagua viongozi wao wa kwanza. Hamisi Heri alichaguliwa kuwa mwenyekiti na Peter Mhando Katibu. Jumla ya watu arobaini na tano walihudhuria mkutano huo na wakapewa kadi za TANU. Mwalimu Kihere alihudhuria mkutano lakini hakuchaguliwa katika nafasi yoyote ya uongozi. Kamati ya wanachama iliundwa kutokana na wale wanachama kumi na moja waasisi waliokutana katika ule mkutano wa kwanza mwezi uliopita.

Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe wafuatao: Abdallah Rashid Sembe, Mohamed Kajembe, Victor Mkello, Dhili Mgunya, Ali Mohamed, Abdallah Mohamed na Mohamed Sadik. Peter Mhando alijitolea nyumba yake kuwa ofisi ya kwanza ya tawi la TANU mjini Tanga. Mara tu baada ya mkutano huu wazee wa Tanga wakiongozwa na Makoko Rashid, mwanachama wa zamani wa TAA walianza kufanya kampeni kwa ajili ya TANU. Chama kilipata msukumo mwingine na kuongezeka nguvu wakati Sadik Ali Patwa Muasia tajiri alipoingia TANU.

Kuanzishwa kwa Tawi la TANU Tanga[hariri | hariri chanzo]

Baada ya kufungua tawi la TANU mjini Tanga, uongozi wa chama ulimwalika Julius Mwalimu Nyerere, Bibi Titi Mohamed, John Rupia na Mbutta Milando. Mwalimu Nyerere alifikia nyumbani kwa Hamis Heri. Huu ndiyo ukawa mwanzo wa urafiki kati ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Abdallah Rashid Sembe. Wazee wa Tanga wanakumbuka kuwa wakati wa harakati Mwalimu Nyerere alipata kufanya mikutano mingi ya siri nyumba ya pili kutoka nyumba ya Sheikh Sembe barabara ya kumi na nne Sheikh Sembe akiwa mwenyeji wake. Nyumba hii sasa hivi inamilikiwa na ukoo wa Salim Mbaruku, moja ya koo maarufu mjini Tanga. Baada ya kushindwa kupata nafasi yoyote katika chama, Mwalimu Kihere alipoteza shauku ya siasa. Mwalimu Nyerere alipokuja Tanga kuifanyia kampeni TANU ndipo Mwalimu Kihere alikaribishwa na Mwalimu Nyerere kujiunga na chama. Matokeo ya ziara ya Mwalimu Nyerere Tanga ilikuwa ni kumrudisha tena Mwalimu Kihere katika siasa.

Mkutano wa kwanza wa hadhara Tanga[hariri | hariri chanzo]

Mabingwa wa kuhamasisha wa TANU enzi zile, Julius Mwalimu Nyerere, Bibi Titi Mohamed walihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja maarufu wa Tangamano. Hii ilikuwa hatua kubwa sana kwa TANU, na kwa harakati dhidi ya ukoloni katika jimbo la Tanga. Haya yalikuwa mapinduzi makubwa kutoka enzi za zile siasa za wasomi katika Discussion Group ambazo kama akina Sembe na wenzake wangeziendekeza uhuru ungelichelewa sana. Baada ya hapo, Mwalimu Kihere alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Tanga badala ya Hamis Heri, na Amos Kissenge alichaguliwa Katibu. Abdallah Rashid Sembe mmoja wa wanachama wasisi wa mwanzo kabisa wa TANU alichaguliwa kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya TANU akiwakilisha Jimbo la Tanga. Sheikh Abdallah Rashid Sembe alidumu katika nafasi hiyo hadi mwaka 1969 akiwa mmoja wa viongozi waliopitisha Azimio la Arusha mwaka wa 1967.

Kifo cha Sheikh Sembe[hariri | hariri chanzo]

Kifo cha Abdallah Rashid Sembe kilitokea Hospitali ya Bombo, Tanga tarehe 22 Mei, 1999. Siku ya pili yake, Jumapili asubuhi kwa wale waliokuwa wanasikiliza Radio One walisikia katika matangazo ya vifo Mwalimu Julius Kambarage akiarifiwa msiba ule. Kisha jina lililofuata likawa la Rais wa Zanzibar Dk. Salmin Amour na baadaye mtangazaji akasema habari za msiba ziwafikie ndugu na jamaa wote. Hili halikuwa tangazo la kifo la kawaida. Si kila siku wananchi wanapata bahati kama hiyo ya kusikia Mwalimu Nyerere akitangaziwa taarifa ya kifo kwenye redio. Ni wazi kuwa wananchi wengi walikuwa wamepigwa na mshangao. Pana uhusiano gani kati ya Sheikh Abdallah Rashid Sembe na Mwalimu Nyerere kiasi ya kifo cha Sheikh aarifiwe.

Urithi wake, kutotambulika kitaifa na kichama[hariri | hariri chanzo]

Wengi hawamfahamu Sheikh Abdallah Rashid Sembe na wengi wataendelea kutomjua hadi hapo Mwalimu Nyerere, wana-historia na CCM yenyewe itakapoamua kuandika upya historia yake na kuwaenzi wale wote waliopigania uhuru wa nchi hii. Hata pale makaburini Msambweni katika makaburi ya Sharif Haidar, CCM walipokuwa wakieleza habari za mchango wa Sheikh Rashid Sembe katika kuasisi TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika habari zilizotolewa zilijaa makosa matupu.

Msomi maarufu na makini, Juma Mwapachu katika taa'zia aliyomwandikia marehemu Dossa Aziz katika gazeti la The African kwa uchungu alisema kuwa, wakati mwingine inakuwa aibu na fedheha unapowasikia viongozi wa CCM wakijaribu kwa shida sana kueleza mchango wasiojua wa mzalendo aliyefariki dunia.

Juma Mwapachu akamaliza kwa kumwuliza Mwalimu Nyerere kuwa hadi lini atanyamaza kimya bila ya kuwataja wenzake aliokuwa nao katika kupigania uhuru wa Tanganyika. Hali kadhalika akawauliza wasomi wazalendo kwanini hadi leo hakuna juhudi ya kutafiti na kuandika historia ya kweli ya uhuru wa Tanganyika.

Hadi hapo Mwalimu Nyerere atakapofungua kinywa chake kuwaeleza wananchi habari za mashujaa wenzake aliokuwa nao katika harakati za kudai uhuru, wananchi na hasa kizazi cha hivi karibuni kitakuwa kinamtukuza yeye pekee kama shujaa wa uhuru wa Tanganyika. Na wenzake wengi waliomsaidia watabaki hawafahamiki na mwishowe historia nzima ya uhuru wa Tanganyika itatoweka.

Juma Mwapachu

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]