Nenda kwa yaliyomo

Visiwa vya Heard na McDonald

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Visiwa vya Heard na Mcdonald baina Australia, Antaktiki na Afrika
Sili wa Tembo-bahari Kusini na wavindaji waliowachinjwa kisiwani Heard wakati wa karne ya 19
Ndege kwenye ufuko wa Heard Island

Kisiwa cha Heard na Visiwa vya McDonald (kwa kifupi: HIMI [1]) ni eneo la ng'ambo la Australia. Ni visiwa katika Bahari ya Hindi vinavyopatikana takribani katikati ya Australia, Madagaska na Antaktiki.[2] Hakuna watu wanaoishi huko.

Visiwa hivyo vimepokewa katika Orodha ya Urithi wa Dunia ya UNESCO.

Historia [3][hariri | hariri chanzo]

Visiwa hivyo havikufikiwa na binadamu hadi karne ya 19. Inawezekana kwamba mabaharia wa meli zilizowinda nyangumi katika sehemu hiyo ya bahari walipita mapema zaidi, lakini mtu wa kwanza wa kutoa habari huhusu visiwa hivyo alikuwa nahodha John Heard kutoka Marekani aliyeona kisiwa tarehe 25 Novemba 1853 akipita kutoka Boston kuelekea Melbourne. Kutokana na taarifa yake kisiwa kikubwa kilipokea jina lake "Heard Island". Muda mfupi baadaye Mmarekani mwingine McDonald alipita kwenye visiwa vidogo vilivyopokea jina lake.

Watu wa kwanza waliotua kisiwani Heard kuanzia mwaka 1855 walikuwa mabaharia kutoka Marekani waliowinda sili, hasa spishi ya Tembo-bahari Kusi (Mirounga leonina) na kuchemsha shahamu yake ili kupata mafuta. Hadi mwaka 1880 waliangamiza karibu sili wote wa kisiwani wakivuna jumla ya mapipa 100,000 ya mafuta ya sili. Baadaye waliondoka.

Mnamo mwaka 1908 Uingereza ilitangaza visiwa kuwa eneo lake na kuvikabidhi kwa Australia kwenye mwaka 1947. Mwaka 1948 Australia ilituma kundi dogo la wataalamu walijenga vibanda kwenye hori ya Atlas Cove na kutekeleza utafiti wa kitaalamu wa jiografia wa visiwa, wanyama na mimea yake. Waliondoka tena mwaka 1954 na tangu mwaka ule ni mara chache kwamba vikundi vya wataalamu vilirudi kwa miezi kadhaa kwa utafiti mwingine.

Visiwa vidogo vya McDonald vilitembelewa mara ya kwanza mwaka 1971 na wanasayansi kutoka Autralia waliotua kwa msaada wa helikopta.

Jiografia[hariri | hariri chanzo]

Kisiwa cha Heard ni kisiwa kikubwa katika eneo hili chenye eneo la kilomita za mraba 368. Asilimia 80 ya eneo lake hufunikwa na barafu ya kudumu inayolishwa na barafuto 41 zinazotelemka kwenye milima hadi ufukwe[4].

Sehemu kubwa ya eneo ni milima ya Big Ben na mlima mkubwa ni volkeno hai ya Mawson Peak yenye kimo cha mita 2,745 juu ya UB.

Mawson Peak ni pia mlima mrefu kabisa katika maeneo ya Australia.

Visiwa vya McDonald ni vidogo, viko umbali wa km 44 upande wa magharibi wa Heard Island. Maeneo yake kwa jumla si zaidi ya km² 2.5, na nusu yake ni kisiwa kikubwa zaidi cha McDonald.

Kilomita 10 upande wa kaskazini wa Heard kuna kundi la visiwa vidogo vingine, eneo la kwa jumla ni km² 1 tu.

Kutokana na tabianchi baridi hakuna mimea mikubwa ila vichaka vidogo, nyasi, mimea ya buabua na kuvumwani[5].

Wanyama ni sili ambao wameongezeka tena tangu mwisho wa uwindaji pamoja na pengwini na ndege wa bahari[6].

Australia imetangaza visiwa pamoja na eneo la bahari kuwa hifadhi ya mazingira ya bahari. Hairuhusu vikundi vikubwa vya wageni kufika huko.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Commonwealth of Australia. "About Heard Island - Human Activities". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2006-10-18. Iliwekwa mnamo 2006-10-21.
  2. 7718 km location
  3. Maelezo katika kifungu hiki hufuata Makala "Heard Island (Sub-Antarctic), katika William James Mills, Exploring Polar Frontiers: A Historical Encyclopedia, vol 2, ABC-CLIO, 2003
  4. Ken Green and Eric Woehler (2006). Heard Island: Southern Ocean Sentinel. Surrey Beatty & Sons. ku. 28–51.
  5. Plants. Australian Department of the Environment, Australian Antarctic Division. Updated 28 February 2005.
  6. Kigezo:WWF ecoregion

Tovuti zingine[hariri | hariri chanzo]