Ufahamu wa uwezo wa kushika mimba

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Ufahamu wa uwezo wa kushika mimba (kwa Kiingereza "Fertility Awareness", kifupi FA) ni elimu inayohusu mbinu zinazotumika kutambua wakati mwanamke anapoweza kushika mimba na asipoweza kushika mimba katika mzunguko wa hedhi. Mbinu hizo zinaweza kutumika ili kuzuia mimba isiyotamaniwa na vilevile kupata mimba iliyotamaniwa, lakini pia kama njia ya kusimamia afya ya uzazi wa mwanamke.

Mbinu kadhaa za kubaini siku ambazo mwanamke hawezi kupata mimba zinajulikana tangu zamani, lakini ujuzi wa kisayansi uliopatikana katika karne ya 20 umeongeza sana idadi na hasa usahihi wa mbinu hizo.

Kutoka mwaka 1930 hadi 1980, utafiti na ukuzaji wa uelewa huo wa masuala ya uzazi ulifanywa hasa na wataalamu wanaohusika na Kanisa Katoliki kwa lengo la kusaidia kupanga uzazi watu wa ndoa wanaokataa mbinu za teknolojia kwa msingi wa maadili au kwa kuzingatia madhara yake.

Kwa kiasi kikubwa mashirika yanayotafuta na kueneza ufahamu wa uwezo wa kushika mimba yanaendelea kuongozwa na Wakatoliki, lakini baadhi ya mashirika ya kawaida sasa yapo.

Mbinu za ufahamu wa uwezo wa kushika mimba hutegemea uchunguzi wa mabadiliko ya ishara za msingi yanayoashiria uwezekano wa kutunga mimba (kama vile joto la mwili, ute wa uke, na mkao wa seviksi) kwa kufuatilia mzunguko wote wa hedhi na hivyo kubaini wakati ambapo inawezekana kushika mimba.

Ishara nyingine pia zinaweza kuzingatiwa: hizo ni pamoja na ulaini wa matiti na uchungu wakati kijiyai kinapoachiliwa, uchunguzi wa mkojo kwa vifaa vya kubashiri udondoshwaji wa vijiyai, na uchunguzi wa kihadubini wa ute au ugiligili wa seviksi (yaani mlango wa kizazi). Isitoshe, ipo njia ya kufuatilia uwezo wa kushika mimba kwa tarakilishi.

Istilahi

Mbinu zinazotegemea dalili zinafuatilia moja au zaidi kati ya ishara tatu za msingi za kuweza kutunga mimba - joto la msingi la mwili, ute wa uke na mkao wa seviksi.[1]

Mbinu zinazotegemea ute wa uke tu ni pamoja na Mbinu ya Billings ya Kutambua Kijiyai Kuachiliwa, The Ovulation Method Archived 28 Mei 2018 at the Wayback Machine., Mbinu ya Creighton, na Mbinu ya Siku Mbili.

Mbinu za dalili ya joto la mwili hujumuisha pia uchunguzi wa joto la msingi la mwili (basal body temperature = BBT), ute wa uke, na wakati mwingine mkao wa seviksi.

Mbinu zinazotegemea kalenda hufuatilia mzunguko wa hedhi ya mwanamke na kwa kuzingatia urefu wa mzunguko wake kutambua anapoweza kupata mimba. Mbinu maarufu zaidi kati ya hizo ni Mbinu ya Siku Sanifu. Mbinu ya Urari-Kalenda pia huhesabiwa njia ya kutegemea kalenda, ingawa haijafafanuliwa vizuri na ina maana nyingi tofauti kwa watu tofauti.

Mbinu hizo za kupanga uzazi zinaweza kuitwa Mbinu za Uzazi Zinazotegemea Ufahamu (wa uwezo wa kuzaa), [2] Jina "Mbinu ya Uelewa wa Uzazi" (kwa Kiingereza Fertility Awareness Method = FAM) linatumika hasa kwa mfumo uliofundishwa na Toni Weschler. Jina "Mbinu Asili ya Uzazi wa Mpango" (kwa Kiingereza natural family planning = NFP) wakati mwingine hutumiwa kutaja mbinu yoyote inayotegemea Ufahamu wa Uzazi. Hata hivyo, msamiati huo ni mahsusi kuhusu mbinu zile zinazokubaliwa na Kanisa Katoliki: mbali ya uwezekano wa kutopata mimba wakati wa kunyonyesha (kwa Kiingereza Lactational amenorrhea method = LAM), ni kutofanya tendo la ndoa siku ambapo kuna uwezekano wa kupata mimba. Hapo mbinu za FA zinaweza kutumika ili kutambua nyakati hizo zinazoweza kuleta mimba.

Wanawake ambao wananyonyesha na wanapenda kukwepa mimba wanaweza kutegemea kukatizwa kwa hedhi wakati wa kunyonyesha. Hiyo ni tofauti na ufahamu wa uzazi, lakini kwa sababu haihusishi vifaa wala kemikali, mara nyingi hutajwa pamoja na FA kama njia asili ya uzazi wa mpango.

Historia

Ukuaji wa mbinu zinazotegemea kalenda

Haijulikani kwa hakika lini iligunduliwa kwa mara ya kwanza kuwa wanawake wana vipindi vya kutunga mimba na visivyo vya kutunga mimba vinavyoweza kutabirika. Mwaka 388 Agostino wa Hippo aliandika kuhusu kuepuka mara kwa mara tendo la ndoa ili kuzuia mimba akiwalaumu Wamani kwa kutumia njia hiyo ili kubaki bila watoto.[3]

Kitabu fulani kinasema kuacha ngono kwa muda kulipendekezwa na "watu wachache wasio wa dini tangu katikati ya karne ya 19",[4] lakini katika karne ya 20 ushawishi mkuu uliohamasisha mbinu za ufahamu wa uwezo wa kushika mimba ulitoka katika Kanisa Katoliki.

Mwaka 1905 Theodoor Hendrik van de Velde, mwanajinakolojia wa Uholanzi, alionyesha kuwa wanawake hutoa kijiyai mara moja tu kila mzunguko wa hedhi.[5] Miaka ya 1920 Kyusaku Ogino, mwanajinakolojia wa Ujapani, na Hermann Knaus, kutoka Austria, wakifanya kazi bila ushirikiano waligundua kwamba kijiyai hutokea siku kumi na nne hivi kabla ya kipindi cha hedhi kinachofuata.[6] Ogino alitumia uvumbuzi wake kutengeneza hesabu ya kuwasaidia wanawake wasiopata mimba kwa kufanya tendo la ndoa kwa wakati mwafaka kupata mimba. Mwaka 1930 John Smulders, daktari Mkatoliki kutoka Uholanzi, alitumia uvumbuzi huo kuunda mbinu ya kuepuka mimba. Smulders alichapisha kazi yake chini ya Chama cha Matabibu Wakatoliki wa Uholanzi, na hiyo ilikuwa mbinu sanifu ya kwanza ya kuepuka mimba kwa kuacha kujamiiana kwa kipindi fulani - mbinu ya kalenda.[6]

Uanzilishi wa mbinu za dalili za joto na ute wa mlango wa uzazi

Katika miaka ya 1930, Wilhelm Hillebrand, padri Mkatoliki nchini Ujerumani, alitunga mbinu ya kuzuia mimba kwa kutegemea joto la msingi la mwili.[7] Mbinu hiyo ya joto ilionekana kuwa na ufanisi mkubwa zaidi katika kuwasaidia wanawake kuzuia mimba kuliko mbinu ya kutegemea kalenda. Katika miongo michache iliyofuata, mbinu hizo mbili zikawa zinatumika sana miongoni mwa wanawake Wakatoliki. Hotuba mbili zilizotolewa na Papa Pius XII mwaka 1951 zilitoa kibali cha hali ya juu kutoka Kanisa Katoliki kwa mbinu hizo kutumiwa na mume na mke waliohitaji kuzuia mimba.[4][8]

Mwanzo mwa miaka ya 1950, John Billings aligundua uhusiano kati ya ute wa mlango wa uzazi na uwezekano wa kutunga mimba alipokuwa akifanya kazi katika Shirika Katoliki la Ustawi wa Jamii mjini Melbourne, Australia. Billings na madaktari wengine kadhaa, akiwemo mke wake Evelyn, walifanyia utafiti ishara hiyo kwa miaka kadhaa, na kufikia mwishoni mwa miaka ya 1960 walikuwa wamefanya majaribio ya kitabibu na kuanzisha vituo vya kufundishia mbinu yao duniani kote.[9]

Mashirika ya kwanza ya ufundishaji mbinu zilizozingatia dalili

Japo awali akina Billings walifundisha pamoja mbinu za dalili ya joto na ya ute wa uke, walipata shida katika kufundisha ishara ya joto kwa idadi kubwa ya watu wasiojua kusoma na kuandika katika nchi zinazoendelea. Hivyo katika miaka ya 1970 walibadilisha mbinu ili kutegemea ute tu.[7] Taasisi ya kimataifa iliyoanzishwa na Billings sasa inajulikana kama "Shirika la Kimataifa la Mbinu ya Kudondosha Kijiyai ya Billings" (kwa Kiingereza World Organization Ovulation Method Billings = WOOMB).

Shirika la kwanza kufundisha mbinu ya dalili za joto lilianzishwa mwaka 1971. John na Sheila Kippley, walei Wakatoliki, walijiunga na Konald Prem katika kufundisha mbinu iliyotegemea dalili zote tatu: joto, ute na mkao wa mlango wa uzazi. Taasisi yao sasa inaitwa "Shirika la Kimataifa la Wanandoa kwa Wanandoa" (kwa Kiingereza "Couple to Couple League International").[7]

Muongo uliofuata ulishuhudia kuanzishwa kwa mashirika mengine ya Kikatoliki ambayo sasa ni makubwa - "Familia ya Amerika" (kwa Kiingereza "Family of the Americas") iliyoundwa mwaka 1977 na kufundisha mbinu ya Billings,[10] halafu "Taasisi ya Papa Paulo VI" (1985), inayofundisha mbinu mpya ya ute pekee iitwayo Creighton Model.[11]

Hadi miaka ya 1980, habari kuhusu ufahamu wa uwezo wa kushika mimba ulipatikana tu kutoka vyanzo vya Kikatoliki.[12] Shirika la kwanza lisilo la kidini la kutolea mafundisho hayo ya uzazi lilikuwa Kituo cha Uelewa wa Uzazi cha New York, lililoanzishwa mwaka 1981.[13] Toni Weschler alianza kufundisha mwaka 1982 na kuchapisha kitabu kilichouzwa sana cha Taking Charge of Your Fertility mwaka 1995.[14] "Justisse" ilianzishwa mwaka 1987 huko Edmonton, Kanada.[15] Mashirika hayo yote yasiyo ya kidini yanafundisha mbinu ya dalili za joto. Ingawa mashirika ya Kikatoliki yanayoeneza uelewa wa uzazi ni makubwa sana kuliko hayo ya wanaharakati yasiyo ya kidini, walimu wasiotegemea dini wamezidi kuongezeka katika miaka ya 1990 na milenia mpya.

Maendeleo ya sasa

Ustawi wa mbinu za ufahamu wa uwezo wa kushika mimba unaendelea. Mwishoni mwa miaka ya 1990, "Taasisi ya Afya ya Uzazi" katika Chuo Kikuu cha Georgetown ilianzisha mbinu mbili mpya.[16][17] Mbinu ya Siku Mbili, inayotegemea ute tu, na CycleBeads, ambayo inafuata mbinu ya Siku Sanifu na ina pia toleo la kieletroniki, iCycleBeads), zimeundwa ili kuwa na ufanisi na urahisi mkubwa zaidi katika kufundisha, kujifunza, na kutumia.

Ishara za uwezo wa kushika mimba

Mizunguko mingi ya hedhi huwa na siku kadhaa za mwanzo ambapo mimba haiwezi kupatikana (muda wa kutoshika mimba kabla ya kudondosha kijiyai), halafu siku ambazo mimba inaweza kutungika, na kisha siku kadhaa tu kabla ya hedhi ambazo mimba haiwezi kutungika ( muda wa kutoshika mimba baada ya kijiyai kudondoshwa). Siku ya kwanza ya kuvuja damu inahesabiwa kuwa siku ya kwanza ya mzunguko wa hedhi. Mbinu mbalimbali za kufahamu uwezo wa kushika mimba huhesabu kwa njia tofauti kidogo kipindi ambapo kuna uwezekano wa kupata mimba, yaani hutumia ishara za msingi za uwezekano huo, historia ya mzunguko, au zote mbili.

Ishara za msingi za kuweza kupata mimba

Ishara tatu za msingi za uwezekano wa kushika mimba ni joto msingi la mwili, ute wa uke na mkao wa seviksi. Mwanamke anayetumia dalili hizo ili kujua uwezo wake wa kupata mimba anachagua kutumia ishara moja, mbili, au zote tatu pamoja. Wanawake wengi hung'amua pia ishara nyingine za ziada kulingana na mzunguko wa hedhi, kama vile maumivu na uzito tumboni, maumivu mgongoni, ulaini wa matiti na maumivu ya kudondosha kijiyai.

Joto la msingi la mwili

Joto la msingi la mwili ni joto la mwili wa mtu linalopimwa wakati wa kwanza anapoamka asubuhi (au baada ya usingizi wa muda mrefu zaidi katika siku). Miongoni mwa wanawake, kudondoshwa kijiyai husababisha joto kupanda kwa 0.3°C hadi 0.9° C (0.5°F hadi 1.6°F) na kubakia hivyo kipindi chote hadi wakati wa hedhi ijayo. Mabadiliko hayo ya joto yanaweza kutumika kubaini mwanzo wa kipindi cha kutoweza kutungika mimba kabla ya kudodosha kijiyai.

Ute wa uke

Ute wa uke

Kuonekana kwa ute wa uke na mwasho wake ni ishara zinazoelezwa kwa kawaida pamoja kama njia za kubaini ishara hiyohiyo. Ute wa uke huzalishwa na seviksi, ambayo huunganisha mji wa mimba na mfereji wa uke. Ute wa uke wenye uwezo wa kushika mimba hukuza maisha ya manii kwa kupunguza uasidi wa uke, na husaidia kuongoza manii kupitia seviksi na kuelekea ndani ya mji wa mimba. Uzalishaji wa ute wa uke wenye uwezo wa kupata mimba husababishwa na homoni ileile (istrojeni) ambayo huandaa mwili wa mwanamke kwa udondoshwaji wa kijiyai. Kwa kuangalia ute wa uke wake, na kuzingatia hisia pindi unapopita ukeni, mwanamke anaweza kubaini wakati mwili wake unapojiandaa kudondosha kijiyai, na wakati ambapo udondoshwaji wa kijiyai umepita. Kijiyai kikidondoshwa, uzalishwaji wa istrojeni hupungua na projesteroni huanza kuongezeka. Kupanda kwa kiwango cha projesteroni husababisha mabadiliko maalumu katika wingi na hali ya ute wa uke.[18]

Mkao wa seviksi

Seviksi hubadilisha mkao kutokana na homoni zilezile zinazosababisha ute wa uke kutolewa na kukauka. Wakati mwanamke yuko katika awamu ya kutoshika mimba katika mzunguko wa hedhi, seviksi hushuka chini katika mfereji wa uke, ikiguswa huwa ngumu (kama ncha ya pua ya mtu), na upenyu (mlango wa seviksi) unakuwa mdogo ukilinganishwa na wakati mwingine, au umefungika. Kadiri mwanamke anavyozidi kuwa na uwezo wa kushika mimba ndivyo seviksi inavyopanda juu katika mfereji wa uke, inakuwa laini ikiguswa (kama mdomo wa mtu), na upenyu unakuwa wazi zaidi. Baada ya kudondoshwa kwa kijiyai, seviksi itarejea mkao wake wa wakati usio wa kushika mimba.

Historia ya mzunguko

Mbinu zinazotegemea kalenda hubainisha uwezekano wa kutopata mimba kabla na baada ya kudondosha kijiyai kulingana na historia ya mzunguko. Zinapotumika vizuri kuzuia mimba, mbinu hizo si madhubuti kama mbinu zinazotegemea dalili, hata hivyo umadhubuti wake unalingana na mbinu zuizi kama vile kiwambo na kizibo cha seviksi.

Mbinu za kuepuka mimba zinazotegemea ute wa uke na joto la mwili kubainisha uwezo wa kutunga mimba baada ya kijiyai kudondoshwa, hushindikana mara chache sana zinapotumika vizuri.[19] Hata hivyo, mbinu hizo huwa na upungufu fulani katika kubaini uwezo wa kutotunga mimba kabla ya kudondosha kijiyai. Rekodi ya joto la mwili pekee haitoi mwongozo kuhusu uwezekano wa mimba kutungwa au kutotungwa kabla ya kijiyai kudondoshwa. Kubaini uwezekano wa kutoshika mimba kabla ya tukio hilo kunaweza kufanywa kwa kuchunguza ute wa uke; hata hivyo, njia hii inafanikiwa kwa kiwango cha chini kuliko ule unaoshuhudiwa katika kipindi baada ya kudondosha kijiyai.[20] Kutegemea uchunguzi wa ute pekee pia ina maana kwamba tendo la ndoa haliruhusiwi wakati wa hedhi, kwa sababu ute wowote hautakuwa dhahiri.[21]

Matumizi ya sheria fulani za kalenda katika kutambua urefu wa kipindi cha kutoweza kutunga mimba kabla ya kijiyai kudondoshwa huruhusu siku chache za ngono mwanzoni mwa mzunguko wa hedhi huku kukiwa na kiwango cha chini sana cha uwezekano wa kupata mimba.[22] Kwa kutumia mbinu ya ute pekee, kuna uwezekano wa kukosea kwa kudhani ni hedhi damu inapotoka katikati ya mzunguko wa hedhi au wakati ambapo kijiyai halikudondoshwa. Kuweka chati sahihi ya joto la msingi la mwili huwezesha utambuzi wa hedhi, wakati ambapo sheria za kalenda kuhusu kipindi kabla ya kudondosha kijiyai zinaweza kutumiwa kwa usahihi.[23] Katika mbinu za joto pekee, sheria ya kalenda inaweza kutegemewa pale tu kutambua uwezekano wa kutoshika mimba kabla ya kudondosha kijiyai. Katika mbinu za joto na ishara, sheria ya kalenda huthibitishwa na rekodi za ute: uchunguzi wa ute wa uke unaoashiria uwezo wa kupata mimba unapewa kipaumbele kuliko mbinu yoyote ya kalenda ya kubainisha uwezo wa kushika mimba.[22]

Sheria za kalenda zinaweza kuweka idadi mahsusi ya siku, ikibainisha kwamba (kulingana na urefu wa mizunguzo iliyopita ya hedhi ya mhusika) siku tatu hadi sita za kwanza katika kila mzunguko wa hedhi huchukuliwa kuwa hazina uwezo wa kupata mimba.[24] Au, sheria ya kalenda inaweza kuhitaji hesabu, kwa mfano lazima iwe kwamba urefu wa kipindi kisicholeta uzazi kabla ya kudondosha kijiyai ni sawa na urefu wa mzunguko mfupi zaidi wa mwanamke huyo ukiondoa siku ishirini na moja.[25] Badala ya kutegemea urefu wa mzunguko, sheria ya kalenda inaweza kuhakikishwa kutokana na siku ya mzunguko ambapo mwanamke ameshuhudia badiliko la joto la mwili. Mfumo mmoja unasema urefu wa kipindi cha kutoweza kutunga mimba kabla ya kudondosha kijiyai unalingana na siku ya kwanza ambapo mwanamke alishuhudia kupanda joto la mwili ondoa siku saba.[26]

Mbinu nyingine

Vifaa vya kubashiri udondoshwaji wa kijiyai (kwa Kiingereza Ovulation predictor kits = OPKs) vinaweza kutambua udondoshwaji unaokaribia kutokea kwa kutegemea wingi wa homoni ya kuandaa ukuta wa chupa ya kizazi (kwa Kiingereza "lutenizing hormone" = LH) katika mkojo wa mwanamke. Kwa kawaida ubashiri wa kufana wa undondoshwaji huo hufuatiwa na udondoshwaji ndani ya saa 12-36.

Uchunguzi wa mate kwa hadubini, ukifanyika kwa usahihi, unaweza kugundua vijidutu maalum katika mate ambavyo hutangulia udondoshwaji wa kijiyai. Vijidutu hivyo kwa kawaida huonekana siku tatu kabla ya udondoshwaji na kuendelea mpaka udondoshwaji utokee. Katika kipindi hiki, vijidutu hivyo hutokea katika ute wa uke pamoja na mate.

Vichunguza uzazi vya kieletroniki vinapatikana kwa majina mbalimbali ya kibiashara. Vichunguzi hivyo vinaweza kutumia mifumo ya Joto la Msingi la Mwili pekee, au kuchambua vitepe vya kupimia mkojo, au kufuatilia dalili mchanganyiko au kuchunguza ukinzani umeme wa mate na ugiligili wa uke, au kwa pamoja baadhi ya mambo hayo mbalimbali .

Manufaa na mapungufu

Ufahamu wa uwezo wa kushika mimba una kiwango fulani cha sifa bainifu:

 • Ufahamu wa uwezo wa kushika mimba unaweza kutumika kudhibiti afya ya uzazi. Mabadiliko katika mzunguko wa hedhi yanaweza kumtahadharisha mtumiaji kuhusu kujitokeza kwa matatizo ya kiginakolojia. Ufahamu wa uwezo wa kushika mimba pia unaweza kutumika kusaidia katika kuagua matatizo yanayojulikana ya kijinakolojia kama vile kutoweza kushika mimba.
 • Ufahamu wa uwezo wa kushika mimba ni uwanda mpana: unaweza kutumika kuzuia mimba au kusaidia katika kutunga mimba.
 • Ufahamu wa uwezo wa kushika mimba unaweza kutumiwa na wanawake wote katika kipindi chote cha uzazi, bila kujali ikiwa anakaribia kumaliza kuzaa, ananyonyesha, au anapata mzunguko wa hedhi usio wa kawaida kwa sababu zingine.
 • Matumizi ya ufahamu wa uwezo wa kushika mimba unaweza kutoa ufahamu kuhusu jinsi mwili wa mwanamke unavyofanya kazi, na unaweza kuwaruhusu wanawake kuwa na udhibiti mkubwa wa uzazi wao wenyewe.
 • Aina fulani ya mbinu za ufahamu wa uwezo wa kushika mimba zinazotegemea dalili ya uzazi zinahitaji uchunguzi au kugusa ute wa uke, matendo ambayo baadhi ya wanawake hawafurahii. Baadhi ya wahudumu wanapendelea kutumia neno "majimaji ya seviksi" badala ya ute wa uke, katika juhudi ya kuwafanya wanawake kama hao kuhisi huru kidogo.
 • Baadhi ya dawa, kama vile ya kupunguza kupaliwa mapafuni, yanaweza kubadili ute ya kizazi. Kwa wanawake wanaotumia dawa hizi, ishara ya ute huenda isionyeshe kisahihi uwezo wa kutunga mimba .[27]
 • Baadhi ya mbinu zinazotegemea dalili huhitaji ufuatiliaji wa joto la kimsingi ya mwili. Kwa sababu usingizi usiokuwa na utaratibu unaweza kuvuruga usahihi wa joto la kimsingi la mwili, wafanyakazi wa kubadilisha zamu na walio na watoto wadogo sana, kwa mfano, huenda wasiweze kutumia mbinu hizo.[27]

Kama njia ya kupanga uzazi

Kwa kufanya tendo kamili la ndoa siku zile tu ambapo katika mzunguko wa hedhi mimba haiwezi kutungwa, maharusi wanaweza kuzuia mimba isipatikane. Wakati ambapo katika mzunguko wa hedhi mimba inaweza kutungwa, wanaweza wakaacha ngono ili kuwa na hakika ya kutoitunga. Wengine siku hizo wanatumia mbinu mbadala za kuzuia mimba ingawa pengine hazifai kwa sababu mbalimbali. [28] Kinyume chake maharusi wanaweza kulenga uzazi kwa hakika zaidi wakifanya tendo la ndoa kwa kutumia vizuri siku zinazouwezesha.

Manufaa

 • Katika kutumia ufahamu wa uwezo wa kushika mimba hakuna madhara yanayotokana na teknolojia inayotumiwa na mbinu nyingine. Kwa jumla hakuna madhara yoyote ya utumiaji, isipokuwa yanayoweza kutokea kwa kuingiza vidole ndani ya uke ili kuchunguza seviksi (kama inavyopendekezwa na baadhi ya mbinu).
 • Ufahamu wa uwezo wa kushika mimba unaweza ukatumika pamoja na vifaa vya kuzuia mimba ili kuendelea kujamiiana katika kipindi ambapo kuna uwezekano wa kupata mimba. Tofauti na utumiaji wa vifaa hivyo bila ufahamu wa uwezo wa kushika mimba, ufahamu huo unawezesha kutumia vizuiamimba siku chache tu, na hivyo kupunguza madhara yanayoletwa navyo.
 • Ufahamu wa uwezo wa kushika mimba hauna gharama au ni nafuu sana. Watumiaji wanaweza wakahitaji kununua chati, kalenda, kipimajoto, au tarakilishi, au pengine kumlipa mkufunzi. Kwa vyovyote gharama ni ya chini ikilinganishwa na mbinu nyingine.
 • Tofauti na mbinu nyingine mbalimbali ambazo zina athari za muda mrefu, ufahamu wa uwezo wa kushika mimba unawezesha kubadili mara moja kutoka uamuzi wa kuzuia mimba hadi ule wa kuilenga.

Mapungufu

 • Wasipotumia vifaa vya kizuia mimba katika kipindi ambapo mimba inaweza kutungwa, wanandoa wanalazimika waache ngono. Ila kupunguza uwezekano wa kupata mimba uwe chini ya 1% kwa mwaka, katika kila mzunguko kuna takriban siku 13 ambapo lazima waache ngono.[29] Kwa wanawake wenye mzunguko unaobadilikabadilika sana - kama ilivyo kawaida wakati wa kunyonyesha, karibu na hedhi kwisha kabisa, au kwa wenye magonjwa ya homoni (kama vile Polycystic ovary syndrome = PCOS) kuacha kujamiiana au kutumia vizuizi kunaweza kuhitajika miezi mfululizo. Wengi hawana motisha au nidhamu ya kutosha wafanye hivyo kwa muda mrefu. Wanaposhindwa kufuata masharti, ni rahisi kupata mimba isiyopangwa.
 • Ufahamu wa uwezo wa kushika mimba haukingi dhidi ya maradhi ya zinaa.[30]Ndiyo maana inafaa zaidi kati ya watu ambao ni waaminifu wao kwa wao, kama watu wa ndoa.

Ufanisi

Ufanisi wa ufahamu ya uzazi, kama ulivyo kwa mbinu nyingi za uzazi wa mpango, unaweza kutathminiwa kwa njia mbili zifuatazo. Kwa kawaida mfumo wa Pearl Index hutumika kukokotoa viwango vya ufanisi, lakini baadhi ya tafiti hutumia majedwali ya mapunguzo.[31]Kwa kawaida viwango hupimwa katika mwaka wa kwanza wa matumizi.[32] Viwango vya matumizi kamili ni kwa wale tu wanaofuata sheria zote, wakitambua kwa usahihi kipindi ambapo kuna uwezekano wa kutunga mimba, na wanaacha ngono isiyo na kinga siku walizotambua kuna uwezekano wa kuitunga. Viwango vya matumizi halisi au matumizi ya kawaida ni kwa wale wote wanaotegemea ufahamu wa uwezo wa kushika mimba ili kuizuia, wakiwa ni pamoja na wasioweza kutimiza vigezo vya "matumizi kamili".

Kiwango cha kufeli kwa ufahamu wa uwezo wa kushika mimba hutofautiana pakubwa kulingana na mbinu iliyotumika kubaini uwezekano wa kupata mimba, njia ya mafundisho, na idadi ya wanaotafitiwa. Baadhi ya tafiti zimekuta viwango halisi vya kufeli vya 25% kwa mwaka au zaidi.[33][34][35] Angalau utafiti mmoja umepata kiwango cha kufeli cha chini ya 1% kwa mwaka kukiwa na mafundisho endelevu na mapitio ya kila mwezi,[36] na tafiti kadhaa zimegundua viwango vya kufeli halisi vya 2-3% kwa mwaka.[29][37][38][39]

Inapotumika kwa usahihi, na kuandamana na mafundisho endelevu ya mara kwa mara, baadhi ya tafiti zimeonyesha kuwa mbinu fulani za ufahamu wa uwezo wa kushika mimba huwa na 99% za ufanisi,[36][40][41][42]

Kitabu Teknolojia ya Uzazi kinaripoti hivi:[43]

 • Mbinu za baada ya kudondosha kijiyai (yaani kuacha ngono kuanzia wakati wa hedhi mpaka baada ya kudondoshwa) inafeli kwa 1% kwa mwaka.
 • Mbinu ya dalili na joto la mwili inafeli kwa 2% kwa mwaka.
 • Mbinu ya ute wa uke pekee inafeli kwa 3% kwa mwaka.
 • Mbinu ya urari wa kalenda inafeli kwa 9% kwa mwaka.
 • Mbinu ya Siku Wastani inafeli kwa 5% kwa mwaka.

Sababu za ufanisi mdogo katika matumizi ya kawaida

Sababu kadhaa zinachangia kufanya ufanisi wa matumizi ya kawaida uwe wa chini kuliko ule wa matumizi kamili:

 • watumiaji kutotii kwa makusudi maelezo (kushiriki ngono bila kinga siku ambapo wanajua mimba inaweza kutungwa): ndiyo sababu ya kawaida zaidi[29][42]
 • makosa ya watoa maelezo ya jinsi ya kutumia mbinu (mkufunzi kutoa taarifa isiyo sahihi au isiyo kamili)
 • makosa ya mtumiaji (kutoelewa sheria, kutunza kumbukumbu vibaya)

Kama njia ya kupata mimba

Ufahamu wa uwezo wa kushika mimba unaweza kutumika pia kwa lengo la kupata mimba kwa urahisi zaidi.

Kupanga wakati wa kujamiiana

Utafiti uliofanywa na Barrett na Marshall umeonyesha kuwa vitendo vya ngono visivyopangwa huwa na uwezekano wa 24% kutungisha mimba katika mzunguko wa hedhi. Utafiti huo pia uligundua kuwa ngono inayolenga wakati maalumu kulingana na ufahamu unaotokana na mbinu ya joto la msingi la mwili pekee huongeza viwango vya mimba hadi 31% -68%.

Utafiti wa mbinu ya ute wa uke umegundua viwango vya mimba vya 67%-81% katika mzunguko wa kwanza ikiwa kujamiiana kutatokea katika Siku ya Kilele cha ishara za ute.[44][45]

Kwa sababu ya viwango vya juu vya mimba kutoka mapema sana (25% za mimba hupotea katika wiki sita za kwanza tangu hedhi ya mwisho ya mwanamke), mbinu zinazotumika kuchunguza uwepo wa mimba zinaweza kusababisha upendeleo katika viwango vya utungaji mimba. Mbinu tofauti na hizo zinaweza kuonyesha viwango vya chini kwa sababu tu huwa zinakosa kugundua mimba zilizotoka mapema. Utafiti mmoja nchini China kati ya wanaoshiriki ngono bila mpangilio ili kutungisha mimba ulitumia mbinu bora za kugundua mimba, ikapata kiwango cha 40% cha kutungwa mimba kwa kila mzunguko katika kipindi cha utafiti cha miezi 12.[46]

Uchunguzi wa tatizo

Mizunguko ya kawaida ya hedhi wakati mwingine huchukuliwa kuwa ushahidi kwamba mwanamke anadondosha vijiyai kawaida, na mizunguko isiyo ya kawaida kuwa ushahidi kuwa udondoshaji wa kijiyai si wa kawaida.[47] Hata hivyo, wanawake wengi ambao mizunguko yao si ya kawaida hudondosha vijiyai kama kawaida, na baadhi ya wenye mizunguko ya kawaida kwa kweli hawadondoshi vijiyai au wana matatizo katika utayarishaji wa ukuta wa chupa cha uzazi. Hasa rekodi za joto la msingi la mwili, lakini pia rekodi za ute wa uke na mkao wake, zinaweza kutumika kwa usahihi kung'amua ikiwa mwanamke anadondosha kijiyai, na kama urefu wa kipindi cha baada ya kudondosha kijiyai cha mzunguko wa hedhi unatosha kwa ujauzito.

Ute wa uke unaoweza kutunga mimba ni muhimu katika kujenga mazingira ambayo yanaruhusu manii kupiti mlango wa uzazi na katika viriba vya falopu ambako husubiri kudondoshwa kwa kijiyai.[48] Chati za uwezo wa kupata mimba zinaweza kusaidia kugundua ute hasimu kwa mimba kutungwa, ambao ni sababu ya kawaida ya kutopata mimba. Ikiwa hali hii itagunduliwa, baadhi wanapendekeza matumizi ya guaifenesini katika siku chache kabla ya udondoshwaji wa kijiyai ili kupunguza uzito wa ute.[49]

Upimaji mimba na umri wa ujauzito

Vipimo vya ujauzito si sahihi mpaka wiki 1-2 baada ya kudondoshwa kijiyai. Kujua tarehe inayokisiwa ambayo kijiyai kitadondoka kunaweza kukamzuia mwanamke asipate matokeo yasiyo sahihi kutokana na upimaji wa mapema mno. Pia, siku 18 mfululizo za joto la juu zinamaanisha mwanamke ni mjamzito karibu bila shaka.[50]

Makadirio ya tarehe ya kudondosha kijiyai kutokana na chati za uwezo wa kuzaa ni njia sahihi zaidi ya kukadiria umri wa ujauzito kuliko mbinu za jadi za kupima mimba au mbinu ya kuchunguza hedhi ya mwisho katika utaratibu wa kufuatilia hedhi.[51]

Kama njia ya kupanga jinsia ya mimba

Ufahamu wa uwezo wa kushika mimba unaweza kutumika pia kwa lengo la kupata mimba ya jinsia inayotamaniwa zaidi.[52] Maharusi wanaweza kuchagua mtoto wa kiume au wa kike kwa 85% ya hakika wakifanya tendo la ndoa kwa kupanga kulingana na ute wa uke kuwa wa kuvutika na kuteleza au siyo. Ni kwamba jinsia ya mimba inategemea tu kromosomu za mbegu za baba ambazo ni nusunusu: X kwa kuzaa watoto wa kike na Y kwa kuzaa watoto wa kiume. Mbegu zenye kromosomu X ni dhaifu kidogo nazo huogelea polepole, lakini zinaishi muda mrefu. Kumbe zenye kromosomu Y zina nguvu zaidi na kuogelea upesi, lakini hufa upesi.

Ili kupata mtoto wa kiume

Kwa kuzingatia tabia hizo mbili tofauti, maharusi wakitaka mtoto wa kiume wanatakiwa kufanya tendo la ndoa siku ya kwanza baada ya kilele (kujisikia kuteleza) na kuendelea kwa miandamo 6 ya hedhi. Kama mwanamke hajapata mimba baada ya miandamo 6, waanze kuonana siku ya kilele na siku inayofuata. Kama mwanamke amekosa siku ya kilele, yaani kama utelezi wa ute unaendelea siku inayofuata, waonane tena siku inayofuata. Kwa njia hiyo mbegu zenye kromosomu Y tu zitafikia kijiyai kilichochopoka, kwa sababu mbegu zenye kromosomu X zinaogelea polepole tu.

Ili kupata mtoto wa kike

Kinyume chake, wakitaka mtoto wa kike wanatakiwa kufanya tendo la ndoa siku ya kwanza ya ute wa uzazi. Halafu wapumzike mpaka siku ya nne baada ya kilele. Waendelee hivyo kwa miandamo michache. Kama mwanamke hajapata mimba baada ya miezi michache, wafanye tendo la ndoa siku ya kwanza na ya pili ya ute wa uzazi halafu wapumzike mpaka siku ya nne baada ya kilele. Waendelee hivyo kwa miandamo michache. Kama mwanamke hajapata mimba baada ya miezi michache, wafanye tendo la ndoa pia siku ya tatu ya ute wa uzazi halafu wapumzike mpaka siku ya nne baada ya kilele. Waendelee hivyo kwa miandamo michache. Kwa njia hiyo mbegu zenye kromosomu Y zitakufa kabla ya kuweza kuungana na kijiyai, na hivyo zitabaki zenye kromosomu X kuwa na nafasi hiyo. Siku nzuri ya kupata mtoto wa kike ni kufanya tendo la ndoa siku mbili kabla ya kilele.

Tazama pia

Tanbihi

 1. Weschler, Toni (2002). Taking Charge of Your Fertility (toleo la Revised). New York: HarperCollins. ku. 52. ISBN 0-06-093764-5.
 2. "Medical Eligibility Criteria for Contraceptive Use:Fertility awareness-based methods". Fourth edition. World Health Organization. 2010. Iliwekwa mnamo 2012-12-11. {{cite journal}}: Cite journal requires |journal= (help)
 3. Saint, Bishop of Hippo Augustine (1887). A Select Library of the Nicene and Post-Nicene Fathers of the Christian Church, Volume IV. Grand Rapids, MI: WM. B. Eerdmans Publishing Co. ku. On the Morals of the Manichæans, Chapter 18. {{cite book}}: Unknown parameter |coauthors= ignored (|author= suggested) (help)
 4. 4.0 4.1 Yalom, Marilyn (2001). A History of the Wife (toleo la First). New York: HarperCollins. ku. 297–8, 307. ISBN 0-06-019338-7.
 5. "A Brief History of Fertility Charting". FertilityFriend.com. Iliwekwa mnamo 2006-06-18.
 6. 6.0 6.1 Singer, Katie (2004). The Garden of Fertility. New York: Avery, a member of Penguin Group (USA). ku. 226–7. ISBN 1-58333-182-4.
 7. 7.0 7.1 7.2 Hays, Charlotte. "Solving the Puzzle of Natural Family Planning". Holy Spirit Interactive. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2017-12-12. Iliwekwa mnamo 2012-02-15. {{cite journal}}: Unknown parameter |dead-url= ignored (|url-status= suggested) (help)
 8. [18] ^ Moral Questions Affecting Married Life: Addresses given October 29, 1951 to the Italian Catholic Union of midwives Archived 6 Desemba 2010 at the Wayback Machine. 26 Novemba 1951 to the National Congress of the Family Front and the Association of Large Families, National Catholic Welfare Conference, Washington, DC.
 9. Billings, John (2002). "THE QUEST — leading to the discovery of the Billings Ovulation Method". Bulletin of Ovulation Method Research and Reference Centre of Australia. 29 (1): 18–28. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2007-02-19. Iliwekwa mnamo 2007-03-18. {{cite journal}}: Unknown parameter |dead-url= ignored (|url-status= suggested) (help); Unknown parameter |month= ignored (help)
 10. "About us". Family of the Americas. 2006. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2007-02-13. Iliwekwa mnamo 2007-03-18.
 11. "About the Institute". Pope Paul VI Institute. 2006. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2012-03-12. Iliwekwa mnamo 2012-02-21.
 12. Singer (2004), p.xxiii
 13. "About us". Fertility Awareness Center. 2006. Iliwekwa mnamo 2007-03-18.
 14. Weschler (2002)
 15. "About Us". Justisse. 2002. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2006-11-16. Iliwekwa mnamo 2007-03-18.
 16. Arévalo M, Jennings V, Sinai I (2002). "Efficacy of a new method of family planning: the Standard Days Method" (PDF). Contraception. 65 (5): 333–8. doi:10.1016/S0010-7824(02)00288-3. PMID 12057784. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2019-09-07. Iliwekwa mnamo 2010-11-30. {{cite journal}}: Unknown parameter |dead-url= ignored (|url-status= suggested) (help)CS1 maint: multiple names: authors list (link)
 17. Jennings V, Sinai I (2001). "Further analysis of the theoretical effectiveness of the TwoDay method of family planning". Contraception. 64 (3): 149–53. doi:10.1016/S0010-7824(01)00251-7. PMID 11704093.
 18. James B. Brown (2005). "Physiology of Ovulation". Ovarian Activity and Fertility and the Billings Ovulation Method. Ovulation Method Research and Reference Centre of Australia. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2005-12-24. Iliwekwa mnamo 2010-11-30.
 19. Kippley (2003), uk.121-134, 376-381
 20. Kippley (2003), uk.114
 21. Evelyn, Dr. Billings, Ann Westinore, (1998). The Billings Method: Controlling Fertility Without Drugs or Devices. Toronto: Life Cycle Books. uk. 47. ISBN 0-919225-17-9.{{cite book}}: CS1 maint: extra punctuation (link) CS1 maint: multiple names: authors list (link)
 22. 22.0 22.1 Kippley (2003), uk.108-113
 23. Kippley (2003), uk.101 sidebar na Weschler (2002), uk.125
 24. Kippley (2003), uk.108-109 na Weschler (2002), uk.125-126
 25. Kippley (2003), uk.110-111
 26. Kippley (2003), uk.112-113
 27. 27.0 27.1 "How to Observe and Record Your Fertility Signs". Fertility Friend Handbook. Tamtris Web Services. 2004. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2005-05-28. Iliwekwa mnamo 2005-06-15.
 28. Manhart, MD; Daune, M; Lind, A; Sinai, I; Golden-Tevald, J (Januari–Februari 2013). "Fertility awareness-based methods of family planning: A review of effectiveness for avoiding pregnancy using SORT". Osteopathic Family Physician. 5 (1): 2–8. doi:10.1016/j.osfp.2012.09.002.{{cite journal}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
 29. 29.0 29.1 29.2 Frank-Herrmann P, Heil J, Gnoth C; na wenz. (2007). "The effectiveness of a fertility awareness based method to avoid pregnancy in relation to a couple's sexual behaviour during the fertile time: a prospective longitudinal study". Hum. Reprod. 22 (5): 1310–9. doi:10.1093/humrep/dem003. PMID 17314078. {{cite journal}}: Explicit use of et al. in: |author= (help)CS1 maint: multiple names: authors list (link)
 30. "Fertility Awareness Method". Brown University Health Education Website. Brown University. 2012. Iliwekwa mnamo 2012-12-11.
 31. Kippley, John (1996). The Art of Natural Family Planning (toleo la 4th addition). Cincinnati, OH: The Couple to Couple League. ku. 141. ISBN 0-926412-13-2. {{cite book}}: Unknown parameter |coauthors= ignored (|author= suggested) (help)
 32. Hatcher, RA (2000). Contraceptive Technology (toleo la 18th). New York: Ardent Media. ISBN 0-9664902-6-6. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2008-05-31. Iliwekwa mnamo 2010-11-30. {{cite book}}: Unknown parameter |coauthors= ignored (|author= suggested) (help); Unknown parameter |dead-url= ignored (|url-status= suggested) (help)
 33. Wade ME, McCarthy P, Braunstein GD; na wenz. (1981). "A randomized prospective study of the use-effectiveness of two methods of natural family planning". American journal of obstetrics and gynecology. 141 (4): 368–376. PMID 7025639. {{cite journal}}: Explicit use of et al. in: |author= (help); Unknown parameter |month= ignored (help)CS1 maint: multiple names: authors list (link)
 34. Medina JE, Cifuentes A, Abernathy JR; na wenz. (1980). "Comparative evaluation of two methods of natural family planning in Colombia". American journal of obstetrics and gynecology. 138 (8): 1142–1147. PMID 7446621. {{cite journal}}: Explicit use of et al. in: |author= (help); Unknown parameter |month= ignored (help)CS1 maint: multiple names: authors list (link)
 35. Marshall J (1976). "Cervical-mucus and basal body-temperature method of regulating births: field trial". Lancet. 2 (7980): 282–283. doi:10.1016/S0140-6736(76)90732-7. PMID 59854. {{cite journal}}: Unknown parameter |month= ignored (help)
 36. 36.0 36.1 Evaluation of the Effectiveness of a Natural Fertility Regulation Programme in China Archived 27 Aprili 2007 at the Wayback Machine.: Shao-Zhen Qian, et al. Reproduction and Contraception (English edition), in press 2000.
 37. Frank-Herrmann P, Freundl G, Baur S; na wenz. (1991). "Effectiveness and acceptability of the sympto-thermal method of natural family planning in Germany". American journal of obstetrics and gynecology. 165 (6 Pt 2): 2052–2054. PMID 1755469. {{cite journal}}: Explicit use of et al. in: |author= (help); Unknown parameter |month= ignored (help)CS1 maint: multiple names: authors list (link)
 38. Clubb EM, Pyper CM, Knight J (1991). "A pilot study on teaching natural family planning (NFP) in general practice". Proceedings of the Conference at Georgetown University, Washington, DC. Archived from the original on 2007-03-23. https://web.archive.org/web/20070323160200/http://www.fertilityuk.org/nfps822.html. Retrieved 2010-11-30.
 39. Frank-Herrmann P, Freundl G, Gnoth C; na wenz. (Juni–Septemba 1997). "Natural family planning with and without barrier method use in the fertile phase: efficacy in relation to sexual behavior: a German prospective long-term study". Advances in Contraception. 13 (2–3): 179–189. doi:10.1023/A:1006551921219. PMID 9288336. {{cite journal}}: Explicit use of et al. in: |author= (help)CS1 maint: date format (link) CS1 maint: multiple names: authors list (link)
 40. Ecochard, R.; Pinguet, F.; Ecochard, I.; De Gouvello, R.; Guy, M.; Huy, F. (1998). "Analysis of natural family planning failures. In 7007 cycles of use". Fertilite Contraception Sexualite. 26 (4): 291–6. PMID 9622963.
 41. Hilgers, T.W.; Stanford, J.B. (1998). "Creighton Model NaProEducation Technology for avoiding pregnancy. Use effectiveness". Journal of Reproductive Medicine. 43 (6): 495–502. PMID 9653695.
 42. 42.0 42.1 Howard, M.P.; Stanford, J.B. (1999). "Pregnancy probabilities during use of the Creighton Model Fertility Care System". Archives of Family Medicine. 8 (5): 391–402. doi:10.1001/archfami.8.5.391. PMID 10500511.
 43. James Trussell et al. (2000) "Contraceptive effectiveness rates", Contraceptive Technology - 18 Edition, New York: Ardent Media. On-press.
 44. Ryder R (1993). ""Natural family planning": effective birth control supported by the Catholic Church". BMJ. 307 (6906): 723–6. doi:10.1136/bmj.307.6906.723. PMC 1678728. PMID 8401097.
 45. Hilgers T, Daly K, Prebil A, Hilgers S (1992). "Cumulative pregnancy rates in patients with apparently normal fertility and fertility-focused intercourse". J Reprod Med. 37 (10): 864–6. PMID 1479570. {{cite journal}}: Unknown parameter |month= ignored (help)CS1 maint: multiple names: authors list (link)
 46. Wang X, Chen C, Wang L, Chen D, Guang W, French J (2003). "Conception, early pregnancy loss, and time to clinical pregnancy: a population-based prospective study". Fertil Steril. 79 (3): 577–84. doi:10.1016/S0015-0282(02)04694-0. PMID 12620443.{{cite journal}}: CS1 maint: multiple names: authors list (link)
 47. "Nakala iliyohifadhiwa". womenshealth.gov, U.S. Department of Health and Human Services, Office on Women's Health. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2012-11-02. Iliwekwa mnamo 2012-12-11. {{cite journal}}: |contribution= ignored (help); Cite journal requires |journal= (help); Unknown parameter |dead-url= ignored (|url-status= suggested) (help). "Some signs that a woman is not ovulating normally include irregular or absent menstrual periods."
  "Adult Health Advisor". 2012. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2010-12-29. Iliwekwa mnamo 2014-08-22. {{cite journal}}: |contribution= ignored (help); Cite journal requires |journal= (help); Unknown parameter |dead-url= ignored (|url-status= suggested) (help). "A woman who is not ovulating normally may have irregular or missed menstrual periods."
  "JustMommies.com". 2007. {{cite journal}}: |contribution= ignored (help); Cite journal requires |journal= (help). "If you have an irregular cycle there is a good chance you are not ovulating normally."
 48. Ellington, Joanna (2004). "Sperm Transport to the Fallopian Tubes". Frequently Asked Questions with Dr. E. INGfertility Inc. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2008-08-28. Iliwekwa mnamo 2008-04-27.
 49. Weschler (2002), uk. 173.
 50. Weschler (2002), uk.316
 51. Weschler (2002), uk.3-4 ,155-156, Insert p.7
 52. Ursula Birgitta Schnell OSB (2011). Uimarishaji wa Familia - Mpango wa uzazi kwa njia ya asili Billings Ovulation Method (toleo la 15th). Ndanda, Tanzania: Benedictine Publication Ndanda-Peramiho. ISBN 9976-63-132-4.

Marejeo

Kwa Kiswahili

Kwa Kiingereza