Nenda kwa yaliyomo

Mtunduru

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Mtunduru ni kata ya Wilaya ya Ikungi katika Mkoa wa Singida, Tanzania yenye msimbo wa posta 43609.

Katika sensa ya mwaka 2022 wakazi wa kata walihesabiwa 22,292 [1]. Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 17,056 waishio humo.[2]

Kata inakaliwa na kabila la Wanyaturu au Warimi ambao wamesambaa karibu wilaya yote ya Ikungi na mkoa wa Singida kwa ujumla.

Historia ya kijiji cha Mtunduru

[hariri | hariri chanzo]

Jina la kijiji cha Mtunduru kwa lugha ya Kinyaturu linatamkwa Mutrunduu na limetokana na mti wenye miiba. Kijiji hicho kimezungukwa na vijiji vya Musimi kwa upande wa kaskazini, Kintandaa mashariki, Kipunda na Misule kwa upande wa kusini na magharibi kijiji cha Ndulungu na Masweya.

Pamoja na Mtunduru kuwa kata iliyoanzishwa mwaka 2012, pia ni kijiji kikongwe kilichoanzishwa rasmi mwaka 1974 katika kipindi ambacho kulikuwa na hamasa ya kitaifa juu ya uanzishwaji wa vijiji vya Ujamaa. Aidha, kabla ya kuanzishwa rasmi, kijiji kilikuwa na jina la Mtunduru. Hapo miaka mingi iliyopita maeneo ya Mtakuja kulikuwa na visima vilivyokuwa maarufu sana ambavyo vilizungukwa na miti hiyo.

Hata hivyo, pengine kijiji hiki kingepewa jina la Malang'u kutokana na nyoka mkubwa aliyekuwa anaishi katika mapango makubwa ya mti wa mbuyu ulioko kaskazini mwa kijiji. Inasemekana nyoka huyo alikuwa mkubwa sana mwenye rangi nyeupe inayong'aa ambapo kila mara wanakijiji walikuwa wanatambika maeneo hayo ili kufanya maombi mbalimbali ya kimila.

Uongozi wa kijiji

[hariri | hariri chanzo]

Miongoni mwa viongozi wa mwanzo kabisa walikuwa ni Manangwa (cheo hiki kinaweza kulinganishwa na Mtendaji wa Kata - WEO). Miongoni mwa Manangwa wa kijiji hiki walikuwepo Muna Msuta, Mubi Mdida na wengineo.

Baada ya kuanzishwa vijiji vya Ujamaa, Yohana Dule alikuwa mwenyekiti wa kwanza, akifuatiwa na Jackson Mwanja, Hamisi Mughenyi, Jumanne Lissu Mdida na sasa ni Andrea Joseph Mangu.

Makatibu waliowahi kuongoza ni pamoja na Rajabu Ng'imba na Juma Mughenyi. Baadaye kada hiyo ilifutwa na kuanza kuongozwa na Makatibu wa CCM Tawi.

Shughuli za uchumi

[hariri | hariri chanzo]

Shughuli za uchumi ni kilimo na ufugaji.

Miongoni mwa mazao ya chakula yanayolimwa ni pamoja na uwele, mtama, mahindi, ulezi, mbaazi, maharage na mazao mengine ambayo hayalimwi kwa wingi.

Mazao ya biashara ni pamoja na alizeti, pamba na ufuta.

Masuala ya elimu

[hariri | hariri chanzo]

Hapo mwanzo kijiji kilikuwa na shule moja ya msingi ambayo ilikuwa inachukua wanafunzi kutoka Mtunduru yenyewe pamoja na vitongoji vya wakati huo ambavyo ni Masweya, Kipunda, Mahola na Mtakuja. Miaka ya karibuni, baada ya vitongoji kukua na kufikia hadhi ya vijiji, zilianzishwa shule katika vitongoji hivyo na kijiji kubaki na shule moja ya Mtunduru.

Ufaulu wa Shule ya Msingi Mtunduru ni mzuri na mara nyingi imekuwa ikishika nafasi nzuri kimkoa na hata kitaifa. Pia, kutokana na ukubwa wa kijiji na kupewa hadhi ya kata, wananchi waliungana kwa pamoja na kuanzisha shule ya sekondari Mtunduru ambayo inachukua wanafunzi waliofaulu katika maeneo ya kata ambayo ni Mtunduru yenyewe, Kintandaa, Masweya, Kipunda na Misule.

Kijiji cha Mtunduru ni miongoni mwa vijiji ambavyo vina wasomi wenye idadi ya wastani ukilinganisha na vijiji vya mikoa mingine. Miongoni mwa wasomi wa mwanzo waliokuwa na Stashahada ya juu (Advanced Diploma) alikuwa ni Muhidini Muna Msuta, Martini Nkumbi Kisuda Msaghaa: hawa walisomea masuala ya Utawala. Waliosoma Diploma miaka ya 1980 ni Mwangi Mpahi Kaunda - Diploma ya Misitu, Aroni Labia - Diploma ya Afya, Shabani Muhuri kidamui - Diploma ya Ardhi, Jumanne NKhambi - Diploma ya Ualimu. Aidha, baadaye wakaibuka vijana ambao wamesoma mpaka Shahada ya Uzamili (Master Degree) kama Jumanne Muna Msuta. Wapo wengine wengi ambao wamemaliza miaka ya karibuni katika shahada ya kwanza.

Kijiji kina wataalamu mbalimbali Wazawa wa Kijiji hiki katika fani za Ualimu, Afya, Mifugo, TEHAMA, Kilimo, Sanaa ya Uchoraji, Sheria,Ufundi sanifu katika masuala ya Mawasiliano na masuala ya Uhasibu. Vijana wengi wa kijiji hiki wako katika ajira Serikalini kama askari, JWTZ ,Utawala wa Sheria,Ualimu,Uhasibu na ajira nyingine nyingi.

Masuala ya afya na huduma za jamii

[hariri | hariri chanzo]

Kijiji hiki pia hakiko nyuma katika masuala ya afya kwani kina kituo cha Afya cha Mtunduru ambacho kinahudumia wakazi wa kijiji hicho na maeneo jirani.

Pia kijiji hiki kinapata huduma ya maji safi na salama kupitia mradi wa maji ambao serikali imechimba kisima na kusambaza mabomba ya maji katika mitaa mbalimbali ya kijiji hicho.

Kata za Wilaya ya Ikungi - Mkoa wa Singida - Tanzania

Dung'unyi | Ighombwe | Iglansoni | Ihanja | Ikungi | Irisya | Isseke | Issuna | Iyumbu | Kikio | Kituntu | Lighwa | Makilawa | Makiungu | Mang'onyi | Mgungira | Minyughe | Misughaa | Mkiwa | Mtunduru | Muhintiri | Mungaa | Mwaru | Ntuntu | Puma | Sepuka | Siuyu | Unyahati

Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Singida bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Mtunduru kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Usitaje majina ya madiwani na viongozi au maafisa wengine wa sasa maana wanabadilika haraka mno.