Alizeti

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Alizeti
(Helianthus annuus)
Alizeti
Alizeti
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Plantae (mimea)
(bila tabaka): Angiospermae (Mimea inayotoa maua)
(bila tabaka): Eudicots (Mimea ambayo mche wao una majani mawili)
(bila tabaka): Asterids (Mimea kama alizeti)
Oda: Asterales (Mimea kama alizeti)
Familia: Asteraceae (Mimea iliyo mnasaba na alizeti)
Nusufamilia: Asteroideae
Jenasi: Helianthus
Spishi: H. annuus
L.

Alizeti au kifuata-jua au mkabilishamsi (jina la kisayansi: Helianthus annuus) ni mmea wenye ua kubwa unaodumu mwaka mmoja. Asili yake iko Amerika lakini imeenea pande nyingi za dunia.

Umbo na ua[hariri | hariri chanzo]

Mimea ya alizeti hukua kufuata kimo cha mita 1.5, mpaka 3.5. Wanasayansi wameripoti kuwa mwaka 1567, kuna mualizeti ulikuwa kufikia kimo cha mita 12 huko Padua. Mbegu zake zilipopandwa maeneo mengine zilitoa mimea yenye urefu wa mita 8. Hivi karibuni maeneo kama vile Uholanzi na Ontario (Kanada) wamefanikiwa kukuza mimea hiyo yenye urefu wa mita 8.

Ua lake lina upana hadi sentimita 30; hali halisi ni "kichwa" au mkusanyiko wa maua madogomadogo yanayokaa pamoja kama duara juu ya kombe kubwa. Maua madogo ya nje huonekana kama petali juwa kubwa zaidi na kuonyesha rangi ya manjano, wakati mwingine hata ya machungwa. Yale maua petali hayazai mbegu. Kila ua dogo ndani ya duara huwa na mbegu. Mbegu huwa na ganda gumu na ndani yake iko mbegu yenyewe yenye kiwango kikubwa cha mafuta.

Kufuata jua[hariri | hariri chanzo]

Jua linapochomoza maua mengi ya alizeti hugeukia mashariki jua linapotokea, na wakati wa mchana huendelea kulifuata jua mpaka magharibi hurudi katika uelekeo wa mashariki tena. Mwendo huo, "heliotropism", huratibiwa na seli ziitwazo ‘pulvinus’ sehemu iliyo huru kuzunguka chini kidogo tu ya chipukizi. Hatua ya chipukizi inapokwisha shina hukomaa na mmea hupoteza uwezo wake wa kuzunguka kulifuata jua.

Mmea huganda kuelekea (mara nyingi) upande wa mashariki. Majani na shina hupoteza rangi yake ya kijani.

Mimeapori jamii ya alizeti huwa haizunguki kufuata jua, japo majani yake hufuata jua maana yake huelekea upande wowote pindi yanapokomaa.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Mmea huu una asili ya Amerika ya Kati. Wataalamu wamekadiria kuwa ulianza kulimwa sana huko Meksiko, mnamo mwaka 2600 KK na pia huko bonde la mto Mississippi. Mifano ya mimea iliyotolewa Meksiko imeonekana huko Tennessee (Marekani) pia, ikionesha kuwa pale tangu 2300 KK watu wengi walitumia mmea wa alizeti kama ishara ya nguvu na utakatifu wa jua, hasa wale wa Azteki na Otomi wa Meksiko na Amerika ya Kusini.

Francisco Pizarro alikuwa mtu wa kwanza kutoka Ulaya kuuona mmea wa alizeti huko Peru. Taswira ya dhahabu ya mmea na mbegu zake zilichukuliwa na kupelekwa Hispania mnamo karne ya 16. Baadhi ya watafiti wanasema kuwa Hispania iliwekewa vikwazo vingi kilimo cha alizeti kutokana na imani ya dini za jadi iliyoambatana na mmea huo.

Kufikia karne ya 18, matumizi ya mafuta ya alizeti yalikuwa maarufu mno, hasa kwa waumini wa Kanisa la Kiorthodoksi la Urusi kwa sababu mafuta ya alizeti yalikuwa miongoni mwa vitu vichache vilivyokuwa vinaruhusiwa kutumika wakati wa Kwaresima.

Kwa mara ya kwanza, Waingereza walifikiria uzalishaji wa mafuta ya alizeti huko Ulaya: kuna leseni ya Kiingereza ya mwaka 1716 inayoelezea mchakato huu. Walakini, uzalishaji mkubwa wa mafuta ya alizeti ulianza nchini Urusi.

Kilimo na matumizi[hariri | hariri chanzo]

Kukua vizuri kwa mmea wa alizeti unahitaji jua la kutosha. Mbegu hupandwa kwa umbali wa sm 45 na kinaacha 2.5.

Kiasili alizeti inapatikana katika Amerika: huko Waindio walipanda ua katika bustani zao. Wahispania walileta mbegu Ulaya baada ya kufika Amerika na mwanzoni mmea huo ulipandwa kama ua la mapambo kwenye bustani.

Baadaye kiwango kikubwa cha mafuta ndani ya mbegu zake kilitambuliwa kikawa mmea muhimu cha kuzalisha mafuta.

Mbegu ya mmea huu huliwa kama chakula cha kutafuna baada ya kuokwa/kukaushwa, pamoja au bila ya chumvi. Huko Ujerumani hutumika kutengenezea mikate.

Alizeti pia ni chakula cha ndege na hutumika kwenye mapishi moja kwa moja na wakati wa kuandaa saladi.

Mafuta ya alizeti yanayokamuliwa kutoka kwenye mbegu za alizeti hutumika kupikia, mafuta ya kutunzia vitu na huzalisha siagi na dizeli ya mimea. Sababu yana gharama ndogo kuliko mafuta ya zeituni. Kuna mimea mingi ya jamii ya alizeti yenye aina mbalimbali na viwango mbalimbali vya mafuta. Mashudu yanayobaki baada ya kukamua mafuta hutumika kulishia mifugo kama chakula, alizeti pia huweza kuzalisha mpira.

Alizeti pia hutumika kufyonza kemikali hatari kutoka ardhini kama vile urani na ilitumika katika kuondoa madini ya urani ardhini baada ya janga la kinyuklia lililotokea huko Chernobyl.

Alama za utamaduni[hariri | hariri chanzo]

Alizeti iko ndani ya nembo la jimbo la Kansas, huko Marekani, na katika nembo la mji wa Kitakyushu, Japani.
Mmea wa alizeti hutumika kama alama ya ujamaa na demokrasia ya ujamaa. Hutumiwa na wafuasi wa itikadi ya Vegani.
Ua la mmea wa alizeti ndio ua la kitaifa nchini Ukraine.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]