Jumapili
Jumapili ni siku ya kwanza katika juma (wiki) ya siku saba yenye asili ya Kiyahudi-Kikristo. Iko kati ya siku za Jumamosi na Jumatatu.
Kwa Wakristo walio wengi ni siku ya sala za pamoja kanisani.
Kiswahili, Kiarabu na utamaduni wa Kiislamu
[hariri | hariri chanzo]Katika lugha ya Kiswahili jina la siku lina namba "2" ndani yake. Hili ni dokezo la asili ya Kiswahili katika utamaduni ya Kiislamu pasipo athira ya Uyahudi unaoanza hesabu baada ya sikukuu ya Kiislamu ya Ijumaa, siku ya sala ya pamoja: Jumamosi kama siku ya kwanza baada ya Ijumaa, Jumapili kama siku ya pili, Jumatatu kama siku ya tatu n.k.
Tabia hii katika Kiswahili ni ya pekee, hasa kwa sababu Kiarabu, ambacho ni lugha ya Korani takatifu na lugha ya kimataifa ya Waislamu, kinafuata hesabu ya Kiyahudi na kuiita siku "al-ahad" yaani "ya kwanza".
Siku ya jua, siku ya Bwana, siku ya ufufuo
[hariri | hariri chanzo]Katika lugha za Kigermanik siku hii ina jina la "jua". Lugha hizo, kama Kiingereza na Kijerumani, zinaendeleza urithi wa Roma ya Kale na zaidi wa Babiloni ambako kila siku ya wiki ilikuwa chini ya mungu fulani aliyeonekana kama nyota au sayari.
Kundi lingine la lugha linatumia msamiati "siku ya Bwana" yaani "Bwana Yesu Kristo". Ni hasa lugha za Kirumi kama Kifaransa (dimanche), Kiitalia (domenica), Kihispania (domingo) na kadhalika.
Lugha ya Kirusi inaita siku hii "voskresenye" yaani siku ya ufufuko.
Uzoefu wa Kikristo
[hariri | hariri chanzo]Wakristo wa madhehebu mengi (isipokuwa Wasabato) wanatazama Jumapili kama siku ya mapumziko iliyochukua nafasi ya Sabato iliyotajwa kwenye Amri Kumi za Agano la Kale.
Sababu ya badiliko hilo lilitokea tangu karne ya 1 ni umuhimu wa ufufuko wa Yesu uliotokea kwenye siku ya kwanza ya juma kufuatana na habari za Agano Jipya.
Kadiri Wakristo wa mwanzo walivyozidi kushindana na Wayahudi wasiomuamini Yesu, walizidi kuzingatia Jumapili kuliko Jumamosi, hasa baada ya kufukuzwa kutoka masinagogi katika miaka ya 80 BK.
Jumapili katika lugha mbalimbali
[hariri | hariri chanzo]Lugha | Jina/Matamshi | Maana | Maelezo |
---|---|---|---|
Kiebrania | יום ראשון jom rishon |
siku ya mwanzo | |
Kigiriki | Κυριακή kiriaki |
(siku ya) Bwana | |
Kiarabu | أحد al-ahad |
(siku) ya kwanza | |
Kiajemi | :یکشنبه yek-schanbe |
(siku ya) kwanza | |
Kireno | Domingo |
(siku ya) Bwana | |
Kilatini | dies solis | Siku ya jua | |
Kiitalia | domenica | (siku ya) Bwana | |
Kihispania | Domingo | (siku ya) Bwana | |
Kifaransa | dimanche | (siku ya) Bwana | |
Kijerumani | Sonntag | siku ya jua | |
Kiingereza | Sunday | siku ya jua |
Siku za juma (wiki) |
---|
Jumapili - Jumatatu - Jumanne - Jumatano - Alhamisi - Ijumaa - Jumamosi |