Nenda kwa yaliyomo

Enoch Sontonga

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Picha yake halisi.

Enoch Mankayi Sontonga (1873 hivi – 18 Aprili 1905) alikuwa mtunzi wa nyimbo nchini Afrika ya Kusini.

Wimbo wake maarufu zaidi alioandika ni "Nkosi Sikelel' iAfrika" (1897) au Mungu ibariki Afrika katika lugha ya Kiswahili.

Maisha ya awali[hariri | hariri chanzo]

Enoch Sontonga alitokea katika kabila maarufu la Waxhosa na alizwaliwa katika mji wa Uitenhage, mashariki mwa jimbo la Cape Colony, ambako pia ni nyumbani kwa Nelson Mandela.

Alikuwa akifanya kazi ya ualimu na baadaye alikuwa kiongozi wa kwaya.

Sontonga alioana na Diana Mngqibisa na mke wake huyo alifariki mwaka 1929.

Nkosi Sikelel' iAfrika[hariri | hariri chanzo]

Nyimbo nyingi za Enoch Sontonga zilikuwa nyimbo za huzuni kuhusu maisha magumu ya Wafrika chini ya utawala wa Wazungu waliokuwa wanawakandamiza Wafrika katika bara lote. Wimbo wake, Nkosi Sikelel' iAfrika, ulitokana na maumivu hayo ya Wafrika ingawa pia ulikuwa wimbo wa kuwapa tumaini kwamba hawako peke yao. Mungu yuko nao, au yuko nasi, ingawa tunaumia na tunateswa na wanaotutawala kwa mabavu.

Alitunga wimbo huo kama wimbo wa Kanisa katika lugha yake ya Kixhosa kama ni wimbo wa bara lote. Ndiyo maana alisema Nkosi Sikelel' iAfrika, God Bless Africa, si God Bless South Africa.

Alipotunga wimbo huo mwaka wa 1897, haukuimbwa hadharani mpaka mwaka wa 1899. Uliimbwa kanisani kwa mara ya kwanza mwaka huo. Halafu, baada ya miaka kumi na tatu, uliimbwa kwenye mkutano wa kwanza wa South African Native Congress mwaka wa 1912 uliofanyika Bloemfontein kuanzisha chama hicho kugombea haki za Wafrika.

Kuanzia mwaka 1925 wimbo wake ulikuwa ukitumika kama wimbo wa wapigania uhuru wa chama cha African National Congress kilipokuwa kinapambana na ukandamizaji wa Makaburu, na kufikia mwaka 1994 wimbo huo ulianza kutumika rasmi kama wimbo wa taifa la Afrika ya Kusini.

Katika nyimbo za mataifa ya Afrika, hakuna wimbo mwingine unaojulikana kama wimbo huo. Umeimbwa pia katika nchi nyingine, kwa mfano Zambia, Zimbabwe na Namibia, na labda hata Botswana, Lesotho, Eswatini na Malawi kwa miaka mingi. Hata katika nchi za Afrika Magharibi, watu wengi wanajua Nkosi Sikelel' iAfrika ni wimbo gani na unamaanisha nini. Ukienda Misri, Algeria na nchi nyingine huko, utawakuta watu wengi wanaojua kuhusu Nkosi Sikelel' iAfrika.

Katika kipindi cha kuelekea kupata uhuru, inasemekana Padre Stanslaus, mmisionari wa Kanisa Katoliki kutoka Tanganyika kipindi hicho, aliKWenda Afrika Kusini kwa shughuli za kitume, ndipo alipokuta Wazulu wanauimba wimbo huo na hivyo kuvutiwa na maudhui yake. Aliporejea Tanganyika alikuja na nota za wimbo huo. Aidha, alipokutana na Mwalimu J. K. Nyerere kumshirikisha na kumshawishi kuichukuwa "rhythm" hiyo na kutafuta wataalamu wa kubuni na kuhariri maneno ili kuendana na maudhui ya Tanganyika. Wimbo huo uliimbwa wakati wa Uhuru wa Tanganyika na baada ya Muungano (Tanganyika na Zanzibar - 26 Aprili 1964). Wimbo huo ulihaririwa na kuthibitishwa kama Wimbo wa Taifa la Tanzania. [1]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Maelezo haya ni kwa mujibu wa Padre Boniface Chitala - Mwafrika wa asili ya Zaire (sasa DRC) wa Jimbo la Sumbawanga. Padre huyu alikuwa mtaalam wa muziki akiwa mchezaji maarufu wa chombo cha muziki kiitwacho "Accordion". Alimpa maelezo hayo David Malilo Mashenene katika Parokia ya Katandala, Sumbawanga mwaka 1996.
Makala hii kuhusu mwanamuziki fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Enoch Sontonga kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.