Ziwa Kingili

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Ziwa Kingili ni kati ya maziwa madogo ya Tanzania.

Linapatikana katika mkoa wa Mbeya, mpakani mwa Busokelo na Kyela, likizungukwa na vijiji vya Ntaba kwa upande wa kaskazini na kijiji cha Kingili kwa upande wa kusini.

Lina uzuri wa aina yake kutokana na mandhari iliyo nalo ikiwa ni pamoja na uzuri wa maji yake meupe na samaki safi waliomo ndani yake.

Ziwa Kingili linasifika kwa kuwa na maji safi na salama kwa shughuli zote za binadamu kama kunywa, kuoga, kupikia pamoja na shughuli za ufugaji.

Ziwa Kingili ni moja kati ya maziwa yenye samaki wengi na safi kwa ajili ya kula kama kitoweo pamoja na shughuli za biashara: samaki hao ni pamoja na kambale, perege (tilapia), dagaa (usipa), chilingali (rhamphochromis) na wengine wengi.

Ziwa Kingili ni ziwa la pekee sana kutokana na kutokuwa na mto hata mmoja unaoingiza maji ndani yake (tributaries/inlets) pamoja na kukosa mto unaotoa maji kwenye ziwa hili (distributaries/outlets). Ziwa Kingili hutegemea sana maji ya mvua kwa kiasi kikubwa, hii ni kwa sababu ziwa hili kina chake hupungua sana wakati wa kiangazi kutokana na jua kali la kuanzia mwezi Agosti hadi Desemba, na wakati huohuo kina chake huongezeka maradufu zaidi ya kiangazi wakati wa masika au kipindi cha mvua za mwezi Februari hadi Mei na kutengeneza mlango wa kutolea maji kutoka kwenye ziwa hilo kwenda kwenye mashamba ya mpunga yaliyoko upande wa mashariki wa ziwa hilo.

Mifereji hiyo hukauka pindi tu mvua za masika zinapokatika. Ziwa Kingili ni ziwa lililozungukwa na vilima vidogovidogo vilivyofunikwa na misitu myepesimyepesi ambayo ni hifadhi ya wanyamapori aina ya ngedere au tumbili.

Ziwa Kingili ni ziwa lenye mawe mengi makubwa kwa madogo ndani ya maji na kando yake ambayo yamekuwa kivutio kwa wageni na wenyeji wa eneo hilo, hasa lile jiwe kubwa lenye rangi ya chungwa (orange au nkesela kama wenyeji waiitavyo) lililopo upande wa kusini magharibi mwa ziwa hilo, pamoja na mchanga kwa kiasi kikubwa.

Ziwa Kingili lina sifa ya kuwa na maji ya moto au uvuguuvugu wakati wa asubuhi na maji ya baridi wakati wa mchana.

Ziwa Kingili ni moja kati ya maziwa yanayopokea watalii wengi mkoani Mbeya. Ziwa Kingili huzungukwa na vijiji vya Kingili (Kyela) pamoja na Ntaba (Busokelo) na wakazi wake ni Wanyakyusa.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]