Sayari kibete
Sayari kibete (kwa Kiingereza dwarf planet) ni kiolwa cha angani kinachofanana na sayari ndogo lakini hakitimizi tabia zote za sayari kamili. Masi yake yanatosha kufikia umbo la tufe sawa na sayari kamili, lakini haikusafisha obiti yake kwa kujivutia sehemu kubwa sana za violwa vya angani vidogo vinavyozunguka kwenye obiti hiyohiyo.
Idadi ya sayari kibete haijulikani. Kufikia 2021, vitu 9 vinavyojulikana vinafikiriwa kuwa vibete, 8 kati yao katika obiti zaidi ya Neptuni.
Historia ya istilahi
[hariri | hariri chanzo]Sayari kibete (dwarf planet) ni jina jipya katika mafundisho ya astronomia. Lilianzishwa mwaka 2006 baada ya kugundua violwa mbalimbali vinavyozunguka jua letu ambavyo ni vikubwa kuliko asteoridi zilizojulikana hadi wakati ule lakini hazifai kuitwa "sayari" kamili. Azimio la kuyaita "sayari kibete" lilifanywa kwenye mkutano wa mwaka huo wa Umoja wa kimataifa wa wanaastronomia.[1]
Sababu ya kuanzisha utaratibu mpya wa sayari kibete ilikuwa kutambuliwa kwa Eris mwaka 2005. Wataalamu walio wengi hawakuwa tayari kuikubali kama sayari ya kumi. Lakini ilhali Eris ni kubwa kiasi kushinda Pluto (iliyohesabiwa kati ya sayari hadi wakati ule) yalitokea majadiliano kati ya wataalamu na kitengo kipya cha "sayari kibete" kilianzishwa. Pamoja na hayo Pluto haikuhesabiwa tena kuwa sayari kamili bali sayari kibete.[2]
Ufafanuzi wa sayari kibete
[hariri | hariri chanzo]Kufuatana na azimio la Umoja wa kimataifa wa wanaastronomia
- sayari kibete ni kiolwa kinachozunguka jua chenye ukubwa wa kutosha kupata umbo la tufe kwa njia ya graviti yake yenyewe lakini haikusafisha violwa vingine kutoka njia yake.[3]
Tabia za Sayari kibete
[hariri | hariri chanzo]Tabia za sayari kibete ni hizi nne:[4]
- 1 ni gimba linalozunguka jua letu
- 2 ukubwa wake unaunda graviti ya kutosha ili kulazimisha maada yake kuchukua umbo kama wa mpira
- 3 ukubwa wake haukutosha kufyeka mazingira ya njia yake ya kuzunguka jua kwa kuvuta kwake magimba madogo mengine
- 4 si gimba linalozunguka sayari nyingine (= yaani si satelaiti = mwezi wa sayari)
Tabia za 1) na 2) ni sawa na sayari. Tabia kuu ya kufanana na sayari ni umbo la tufe. Umbo hili linatokana na graviti ya gimba lenyewe kama masi yake au ukubwa wake unatosha kujifinyanga masi hii katika umbo la tufe. Kama masi ni ndogo zaidi graviti ya gimba haitoshi kufikia umbo la tufe.
Tofauti muhimu ni tabia no. 3: sayari kamili zina ukubwa na uvutano wa kutosha kujivutia magimba mengine madogo; yaani katika njia ya dunia yetu au sayari nyingine hakuna vitu vidogo tena vinavyozunguka hapa pamoja na sayari. Yote yameshaangukia duniani kutokana na uvutano. Magimba yaliyobaki ni yale ambayo yanazunguka kama mwezi au kama bangili ya Zohari ambayo yana mwendo imara.
Tofauti nyingine muhimu ni no. 4: kuna magimba makubwa kushinda Pluto yanayolingana na masharti ya 1-3 lakini huzunguka sayari za Mshtarii na Zohali kama miezi yake. Kwa mfano Ceres, mwezi wa Zohali, ina kipenyo cha km 5,150. Io ina kipenyo cha km 5,200 (karibu sawa na Utaridi) lakini ni mwezi wa Mshtarii, haifai kuitwa sayari wala sayari kibete.
Orodha ya sayari kibete
[hariri | hariri chanzo]Kwa sasa katika mfumo wa jua letu kuna magimba 9 yanayotambuliwa kama sayari kibete:
- Ceres
- Orkus (Orcus)
- Pluto
- Salasia (Salacia)
- Haumea
- Kwaoar (Quaoar)
- Makemake
- Gonggong' (Gonggong)
- Eris
- Sedna
Pluto ilikuwa ikitajwa kama sayari ya jua letu tangu kutambuliwa mara ya kwanza mwaka 1930 lakinimwaka 2006 iliwekwa kwenye kundi la sayari kibete.
Jina | Kipenyo (linganifu na Mwezi) |
Kipenyo (kilomita) |
Masi (linganifu na Mwezi) |
Masi (×1021 kg) |
Densiti (g/cm3) |
Graviti usoni mwake (m/s2) |
Muda wa mzunguko (siku za dunia) |
Miezi | halijoto usoni (K) |
---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|
Ceres | 27% | 946 | 1.3% | 0.94 | 2.17 | 0.29 | 0.38 | 0 | 167 |
Pluto | 68% | 2380 | 17.8% | 13.05 | 1.87 | 0.58 | −6.39 | 5 | 44 |
Haumea | ≈ 36% | 1240 | 5.5% | 4.01 | 2.6–3.3 (?) | 0.44 | 0.16 | 2 | 32 |
Makemake | 41% | 1430 | ? | ? | > 1.4[5] | 0.32 | 1 | ≈ 30 | |
Eris | 67% | 2326 | 22.7% | 16.7 | 2.5 | ≈ 0.8 | ≈ 1 (0.75–1.4) | 1 | ≈ 42 |
Kuna uwezekano wa kuwepo kwa sayari kibete nyingine katika mfumo wa jua lakini hadi sasa hakuna taarifa za kutosha zinazoruhusu azimio kuwa gimba kubwa lina tabia zote za sayari kibete.
Kwa mfano, 4 Vesta na 2 Pallas katika ukanda wa asteroidi wanakaribia kuwa sayari kibete, lakini hawalingani kabisa na ufafanuzi huo.
Vilevile magimba kadhaa katika eneo nje ya obiti ya Neptuni, kama vile Varda, Iksion au Varuna, yanatazamwa kama wagombea wa kuahidi wa cheo cha sayari kibete. Lakini, kwa sasa zinadhaniwa kuwa sio mnene wa kutosha (kwamba zana nafasi tupu za utupu ndani).
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ RESOLUTION B 5 (2) Definition of a Planet in the Solar System, azimio la Mkutano Mkuu wa 2006 wa Umoja wa kimataifa wa astronomia (IAU) , iliangaliwa Mei 2017
- ↑ Azimio la Mkutano Mkuu wa 2006 wa Umoja wa kimataifa wa astronomia (IAU), RESOLUTION B6 Pluto
- ↑ Azimio la Mkutano Mkuu wa 2006 wa Umoja wa kimataifa wa astronomia (IAU) RESOLUTION B 5 (2), iliangaliwa Mei 2017
- ↑ Azimio la Mkutano Mkuu wa 2006 wa Umoja wa kimataifa wa astronomia (IAU) RESOLUTION B 5 (2), iliangaliwa Mei 2017
- ↑ M.E. Brown 2013 "On the size shape and density of dwarf planet Makemake"
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Pluto and the Developing Landscape of Our Solar System. (kuhusu sayari kibete), tovuti ya Ukia, iliangaliwa Julai 2017
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Sayari kibete kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |