Rhodesia ya Kusini

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search
Mahali pa Rhodesia Kusini (=Zimbabwe) katika Afrika.
Bendera ya Rhodesia Kusini.
Ugawaji wa kimbari wa ardhi katika Rhodesia Kusini mnamo 1965
nyeupe: ardhi ya walowezi wazungu
buluu:ardhi chini ya mamlaka ya makabila ya Kiafrika
nyekundu:ardhi ya binafsi ya Waafrika
kijani: ardhi ya serikali

Rhodesia ya Kusini lilikuwa jina la koloni la Uingereza katika nchi ya Kusini mwa Afrika iliyopata uhuru kwa jina la "Zimbabwe" tangu mwaka 1980.

Kuundwa na Cecil Rhodes[hariri | hariri chanzo]

Koloni liliundwa na Cecil Rhodes aliyetwaa eneo hili pamoja na "Rhodesia ya Kaskazini" au Zambia na kuliweka chini ya Kampuni ya Kiingereza ya Afrika Kusini (British South Africa Company).

Rhodes aliwahi kujaribu kupata mapatano na mfalme Lobengula wa Wandebele kuhusu haki za kuchimba madini katika Matabeleland. Mfalme alikataa hadi 1888 alipokubali mapatano ya Rudd. Lobengula alidanganywa na Charles Rudd kwa njia ya mkataba huo uliokuwa msingi wa kutwaliwa kwa eneo lake kwanza na baadaye Zimbabwe yote.

Uvamizi[hariri | hariri chanzo]

1890 kikosi cha askari 500 wa kampuni kiliingia kutoka Afrika Kusini na kutwaa nchi. 180 kati yao walikuwa walowezi walioapishwa kama askari wa "Pioneer Column" na kupewa ardhi baadaye. 300 walikuwa askari wa Polisi ya Kiingereza kwa Afrika ya Kusini (British South Africa Police) ilikuwa kiini cha polisi na jeshi la koloni ya baadaye. Kwa silaha zao za kisasa hasa bunduki za Maxim walishinda wenyeji. Vita ya Matabele ya 1893-1894 ilikuwa vita ya kwanza iliyoona matumizi ya bunduki ya mtombo ya kisasa duniani. Waingereza 50 waliweza kushinda Wandebele 5,000. Hadi 1897 kampuni iliweza kupambana na upinzani wa kijeshi wa Wandebele na pia Washona ikawashinda.

Serikali ya Uingereza ilikubali ya kwamba kampuni itatawala koloni lote (pamoja na Rhodesia ya Kaskazini) kwa niaba ya Ufalme wa Muungano wa Britania na Eire ya Kaskazini. Hadi vita ya kwanza ya dunia idadi ya walowezi ikaongezeka walioanza kudai madaraka ya kujitawala kama koloni kadhaa za Uingereza zenye walowezi wazungu kwa mfano Afrika Kusini, Kanada au Australia.

Koloni ya kujitawala[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 1922 wawakilishi wa walowezi walidai madaraka ya kujitawala. Wengine walipendelea kuunganishwa na Afrika Kusini. Kura ilifanyika kati ya walowezi 34,000 juu ya swali la kuwa koloni ya Uingrgeza yenye madaraka ya kujitawala au kuwa jimbo la tano la Afrika Kusini. Walio wengi walipendelea kuwa koloni yenye madaraka ya kujitawala.

Tangu 12 Septemba 1923 serikali ya Uinbgereza ilichukua utawala juu ya Rhodesia moja kwa moja ikawa koloni ya Uingereza na kampuni ilibaki na shughuli za kiuchumi. Wazungu walipewa serikali yao pamoja na kiwango cha kujitawala katika mambo ya ndani. Waziri mkuu wa kwanza alikuwa Charles Patrick John Coghlan tangu 1923 akifuatwa 1927 na Howard Unwin Moffat. Idadi ya walowezi wazungu ikaongezeka hasa baada ya vita kuu ya pili ya dunia na kufikia 270,000 mwaka 1970.

Hali ya Waafrika[hariri | hariri chanzo]

Hali ya wenyeji Waafrika ilikuwa ya duni tangu uvamizi. Maeneo mapana yenye rutba yalitwaliwa na walowezi. Wenyeji wa sehemu zile walipaswa ama kukubali kama wafanyakazi kwenye mashamba ya Wazungu au kuhamia katika Rizavu za Waafrika. Hata hivyo umoja wa kisiasa na maendeleo ya kiuchumi zilionyesha pia maendeleo fulani upande wa Waafrika wenyeji kwa kuondoa vita za mara kwa mara na kuleta huduma za kwanza za afya na za elimu. Viongozi wa Wazungu Warhodesia waliamini ya kwamba wakati ujao lakini si karibuni sehemu ya Waafrika wangeanza kushirikiana nao katika uongozi wa koloni. Isipokuwa waliamini ni sharti wenyewe walipaswa kuamua ni lini Waafrika wangekuwa tayari kuanza kushirikana nao.

Wakati huohuo wanasiasa wazungu waliendelea kukaza sheria zilizoongeza uguma kwa Waafrika wengi. Sheria ya ardhi ya 1931 iligawa nchi katika maeneo ya wazungu na Waafrika lakini Waafrika walipata theluthi moja ya ardhi tu. Tangu 1936 kila Mwafrika wa kiume alipaswa kutembea na kitambulisho wakati wa kuzuru nje ya rizavu. Sheria ya 1951 (Native Land Husbandry Act) iliamua ya kwamba Waafrika wangekuwa na kiwango fulani cha ardhi na cha mifugo iliyotegemea mazimgira hasa rutba ya eneo. Lakini matokeo ya sheria yalibana uwezo wa Waafrika werngi kuendelea na kujenga maisha yao hivyo wakaongeza upinzani.

Mapambano ya uhuru kuanza[hariri | hariri chanzo]

Baada ya vita kuu ya pili wazungu wa Rhodesia waliona maendeleo mengi lakini Waafrika walianza kusikitika zaidi. ANC ya Afrika Kusini ilienea hadi Rhodesia. Mwenyekiti wake nchini tangu 1957 alikuwa kijana Joshua Nkomo. ANC ilipopigwa marufuku 1959 Nkomo akaenda Uingereza akarudi 1960 na kuunda National Democratic Party of Zimbabwe (NDP) iliyopigwa marufuku 1961 akaunda ZAPU.

(itaendelea)

Viungo vya Nje:[hariri | hariri chanzo]