Zimbabwe African People's Union
Zimbabwe African People's Union (ZAPU) ni chama cha kisiasa nchini Zimbabwe.
Iliundwa mwaka 1961 na Joshua Nkomo katika Rhodesia Kusini (baadaye Zimbabwe) ikapigwa marufuku MWAKA 1962 na serikali ilikuwa mikononi mwa walowezi Wazungu. ZAPU iliendelea kupinga serikali kwa njia ya vita ya msituni kupitia mkono wake wa kijeshi "Zimbabwe People's Revolutionary Army" (ZIPRA).
Nkomo alimteua Robert Mugabe kuwa Katibu Mkuu akaendelea na nafasi hii hadi 1963. Mwaka ule Nkomo alihamisha makao makuu ya chama kwenda Tanzania akasimamisha viongozi kadhaa waliowahi kumpinga, pamoja na Mugabe na Ndabaningi Sithole aliyejitenga na ZAPU na kuanzisha ZANU (chama kilichoongozwa baadaye na Mugabe).
Wakati wa vita ya msituni ya Rhodesia jeshi la ZIPRA kuanzia mwaka 1966 ilikuwa na makambi yake Zambia na ZAPU ilipokea misaada kutoka Urusi wakati ZANU ilipokea misaada na mwongozo wa kiitikadi kutoka China.
ZAPU ilianzishwa kama chama cha kitaifa lakini katika kipindi cha vita Washona walikaa zaidi upande wa ZANU ilhali ZAPU ilibaki na wafuasi upande wa Wandebele, kabila la Nkomo.
Mwaka 1980, baada ya mapatano ya Lancaster House na mwisho wa vita ya msituni kulikuwa na uchaguzi huru ya kwanza nchini. ZAPU iligombea kwa jina la Patriotic Front - ZAPU (PF-ZAPU) lakini ilipata kura za Wandebele tu ilhali Washona walio wengi walileta ushindi kwa ZANU.
Nkomo na ZAPU waliingia katika serikali ya umoja wa Zimbabwe wakajiona wanabagubuliwa na Mugabe na ZANU; mapigano yalitokea baina ya wanajeshi wa ZIPRA na ZANLA (jeshi la ZANU). Hatimaye Mugabe alimfukuza Nkomo serikalini akatuma Brigedi ya Tano, kikosi cha jeshi lake lililokuwa na Washona pekee, kutafuta wapinzani na brigedi hii ilitekeleza mauaji ya watu wanaokadiriwa kuwa 20,000 kati ya Wandebele.
Nkomo alikimbia Zimbabwe mwaka 1963 akarudi 1987 akikubali maungano ya vyama vya ZANU na ZAPU kuwa ZANU-PF. Alikuwa makamu wa rais Mugabe. Alishtakiwa na wafuasi kadhaa kusaliti chama na watu wake akajieleza kuwa alitafuta amani hii kwa kusudi la kumaliza mauaji ya Wandebele na wanachama wa ZAPU.
Makala hii kuhusu mambo ya siasa bado ni mbegu. Unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuongezea habari. |