Nenda kwa yaliyomo

Chama cha Jamhuri cha Marekani

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Republican Party)
Chama_cha_Jamhuri_cha_Marekani
Chama_cha_Jamhuri_cha_Marekani

Chama cha Jamhuri cha Marekani (kwa KiingerezaRepublican Party” au "Grand Old Party") ni chama cha kisiasa nchini Marekani.

Ni kimoja kati ya vyama viwili vya kisiasa vinavyoongoza siasa ya Marekani tangu karne ya 20 kikishindana na Chama cha Kidemokrasia katika mfumo wa vyama viwili.

Chanzo kama chama cha kupinga utumwa

[hariri | hariri chanzo]

Kilianzishwa mwaka wa 1854 kwa lengo la kupinga utumwa[1] na mgombea wake wa urais Abraham Lincoln alishinda uchaguzi wa mwaka 1860; wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Marekani (1861-1865) wabunge wa chama hicho walibatilisha utumwa kisheria[2].

Shabaha za kisiasa

[hariri | hariri chanzo]

Mwelekeo wa chama ulibadilika katika historia yake; mwanzoni kilitazamiwa kusimama zaidi upande wa shabaha za kimaendeleo[3] kama haki za watumwa wa awali, kubana athira ya makampuni makubwa na kulinda maeneo makubwa kama hifadhi ya taifa. Sehemu kubwa ya chama ilisimama pia upande wa haki ya wanawake ya kupiga kura iliyopitishwa mwaka 1920.

Katika karne ya 20 mwelekeo wa chama ulibadilika. Siku hizi siasa yake inalenga kutetea soko huria yaani ubepari bila vikomo, kupinga mabadiliko ya utamaduni kama kutambua haki za mashoga, kutetea familia ya kimapokeo, kupinga kupandishwa kwa kodi kwa kulipa taasisi ya umma na nafasi kubwa ya serikali katika maisha ya watu. Kinapinga siasa ya kijamii inayotaka kuwasaidia maskini kupitia vyombo vya dola kikikazia wajibu wa kila mtu kujitegemea na kuwasaidia wengine kwa hiari. Chama kilisimama upande wa biashara huria ya kimataifa lakini tangu kupotea kwa tasnia nyingi kimebadilisha msimamo huo.

Katika miaka ya mwisho, hasa chini ya rais Donald Trump, Chama cha Jamhuri kimepata kura hasa ya Wakristo wa Kievangelical wanaohofia mabadiliko ya kiutamaduni na wafanyakazi weupe wanaohofia kunyimwa haki na mapato kutokana na kupotea kwa tasnia nyingi, kusogea mbele kwa wahamiaji wapya kutoka Amerika Kusini pamoja na matumizi ya pesa kwa ajili ya watu Weusi.

Kulikuwa na Marais kumi na wanane kutoka Chama cha Jamhuri, kuanzia Abraham Lincoln (1861-1865) hadi George W. Bush (2001-2009).

Kuanzia tarehe 20 Januari 2017, Donald Trump alikuwa rais wa 19 kutoka chama hicho. Alichaguliwa baada ya kupokea asilimia 46,1 pekee za kura za wananchi lakini kutokana na mfumo wa uchaguzi wa rais alipata kura nyingi za wawakilishi wa kura (electoral college)[4].

  1. "Republican National Political Conventions 1856-2008 (Library of Congress)", tovuti ya www.loc.gov. Archived from the original on February 20, 2019. Retrieved March 12, 2019.
  2. Klein, Christopher. "Congress Passes 13th Amendment, 150 Years Ago", tovuti ya history.com, archived from the original on March 30, 2019. Retrieved March 12, 2019.
  3. Skocpol, Theda (1993). "America's First Social Security System: The Expansion of Benefits for Civil War Veterans". Political Science Quarterly. 108 (1): 85–116. doi:10.2307/2152487. JSTOR 2152487.
  4. Final Popular Vote Total Shows Hillary Clinton Won Almost 3 Million More Ballots Than Donald Trump, tovuti ya Huffington Post ya 22.12.2016, iliangaliwa Oktoba 2020