Nenda kwa yaliyomo

Muda sanifu wa dunia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Muda sanifu)
Kanda muda duniani; namba zinaonyesha tofauti na saa ya Greenwich = meridiani ya sifuri

Muda sanifu wa dunia, kifupi: MSD (kwa Kiingereza UTC kwa "universal time coordinated") ni utaratibu wa kulinganisha saa na nyakati kote duniani. Unarejea wakati kwenye longitudo ya Greenwich karibu na London na longitudo hiyo huitwa pia meridiani ya sifuri.

Hesabu ya muda kulingana na kanda

[hariri | hariri chanzo]

Kutokana na meridiani ya Greenwich dunia imegawiwa katika kanda muda ambazo kwa sasa ni 0. Ndani ya kila kanda muda wa saa ni uleule. Saa ya Greenwich au meridiani sifuri ni wakati wa marejeo. Kutoka mstari wake kila mahali kuna saa yake kama kuongezekewa au kupunguziwa kutoka wakati huo. Wakati wa Afrika ya Mashariki unatangulia saa 3 wakati wa Greenwich.

Kwa mfano mtu anapiga simu ya nje kutoka Tanzania saa 2 usiku atampata mwenzake pia saa 2 usiku kama yuko Kenya, Uganda, Ethiopia, Sudani au Uarabuni maana wote wako katika kanda muda moja. Saa ya marejeo, yaani, Greenwich wakati huohuo ni saa 11 jioni. Lakini akipigia simu mtu wa huko China atapampata mwenzake saa 8 usiku maana huko kunatangulia saa 5; kinyume chake akipigia wakati huohuo New York ya Marekani ataongea na mtu aliye kwenye saa 6 mchana.

Kwa lugha ya muda sanifu wa dunia Mtanzania wetu alipiga simu saa "17.00 UTC+3" yaani saa 11 jioni kwenye meridiani ya sifuri ongeza saa tatu. Wenzake huko Beijing wako kwenye saa "17.00 UTC+8" (mahali pa kuongeza saa 8 kwenye saa ya meridiani ya sifuri) na rafiki huko New York yuko saa "17.00 UTC-5" (mahali pa kutoa saa 5 kwenye saa ya Greenwich). Kwa hiyo tofauti na Dar es Salaam au Nairobi ni saa 8 yaani saa 3 kutoka Afrika ya Mashariki hadi meridiani ya sifuri na tena saa 5 hadi New York. Tukipigia simu mahali mbali zaidi upande wa magharibi, kwa mfano Los Angeles, tofauti huwa kubwa zaidi.

Nchi kubwa kama Urusi na Marekani huwa na kanda muda tofauti ndani ya taifa kati ya mashariki na magharibi; nchi ndogo zaidi kwa kawaida zimepangwa katika kanda ileile.

Sababu za kugawa dunia kwa kanda muda

[hariri | hariri chanzo]

Kanda hizo ni mapatano ya kisiasa kwenye msingi wa kisayansi. Sababu yake ya msingi ni kwamba wakati uleule kuna mchana upande mmoja wa dunia na usiku upande mwingine. Mtanzania anayepiga simu saa mbili usiku yuko gizani lakini mwenzake New York yuko mchana akiona jua juu yake angani.

Ugawaji wetu wa saa za siku na usiku kiasili unafuata mwendo wa jua na nuru. Kuna mstari kuanzia kaskazini hadi kusini mwa dunia unaosogea juu ya uso wake ambako kunakucha wakati huohuo. Kwa kupata saa inayolingana na mwanga na nuru ingekuwa vema kama miji na vijiji vyote vinavyokaa kwenye mstari mmoja wa kucha vingekuwa na wakati huohuo na hivi kama kanda muda moja.

Hapa siasa inaingilia maana watu wanaokaa nchi moja wanapendelea kuwa na saa ileile. Hata kama tofauti ya saa ya kucha kati ya Zanzibar na Kigoma ni karibu saa moja miji yote miwili imepangwa ndani ya kanda muda ileile kwa sababu zote mbili ziko Tanzania.

Zamani hakukuwa muhimu kusanifisha wakati kwa sababu watu walisafiri au waliwasiliana polepole. Hali halisi kila mahali palikuwa na wakati wake; watu waliangalia jua wakasema sasa saa 1 asubuhi au saa 6. Hata baada ya kutokea saa za kwanza vifaa hivyo viliwekwa muda kutokana na mwendo wa jua mahali penyewe.

Ni tangu kuanzishwa kwa usafiri wa reli na mawasiliano ya simu kwamba haja ilitokea kulinganisha muda wa kila mahali. Maana kama zamani mtu alitembea kwa miguu au kupanda farasi kufikisha barua tangu karne ya 19 ujumbe ulifika kwa simu mara moja mahali penye saa tofauti.

Hapo majaribio ya kulinganisha na kusanifisha wakati yalitokea.

Nchi ya kwanza kufanya hivyo ndani ya taifa ilikuwa Uingereza na hapo ni asili ya kipaumbele wake wa kihistoria inayoonekana katika chaguo la Greenwich kama rejeo la meridiani ya sifuri. Greenwich ilikuwa na kituo bora cha kuangalia nyota na kazi ya kupima nyota ni muhimu wa kulinganisha wakati kikamilifu hadi leo.