Nenda kwa yaliyomo

Meridiani

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Meridiani ya sifuri (nyeusi) inapita Greenwich/Uingereza; mstari mwekundu ni mfano wa latitudo ya 30.

Meridiani (kutoka Kiingereza: meridian) ni mstari wa kudhaniwa kwenye uso wa ardhi kutoka ncha ya kaskazini hadi ncha ya kusini ya dunia. Kwa lugha nyingine ni nusuduara kwenye uso wa ardhi.

Kuna mstari unaopita Greenwich (Uingereza) uliokubaliwa kuwa meridiani ya sifuri sanifu inayotumiwa kutaja longitudo ya mahali.

Jina linatokana na Kilatini "meridianus" kinachomaanisha "cha mchana". Ilhali mchana hufafanuliwa kuwa wakati ambako Jua linakaa juu kabisa angani, basi mchana unafika saa ileile kwenye kila mahali pa meridiani ileile.

Kwa maana hiyo "meridiani" fulani iko kwa kila mahali duniani, ni sawa na kusema longitudo ya mahali. Hivyo "meridiani ya Dar es Salaam" ni mstari kutoka ncha hadi ncha unaopitia Dar es Salaam, au mstari wa longitudo 39°17'12.8"E.

Meridiani ya sifuri, Greenwich

[hariri | hariri chanzo]

Zamani kulikuwa na mifumo tofauti ya kuhesabu meridiani au longitudo. Mkutano wa mwaka 1884 ulikubali meridiani inayopita kwenye paoneanga pa Greenwich, Uingereza, kuwa "meridiani ya sifuri" yaani mstari wa marejeo kwa kutaja longitudo ya mahali popote duniani[1].

Nyuzi au digrii

[hariri | hariri chanzo]

Kwa hiyo meridiani ya Greenwich huhesabiwa kuwa "0", halafu kuna nyuzi 180 upande wa mashariki na nyuzi 180 upande wa magharibi. Nyuzi ya 180 ni ya pamoja kinyume cha mstari wa Greenwich.

Nyuzi za longitudo hutajwa ama kwa kuongeza "za mashariki / East" na "za magharibi / West", au kwa kutumia namba chanya kwa nyuzi za mashariki na namba hasi kwa zile za magharibi.

Kila meridiani hukatwa na mstari wa ikweta. Sambamba na ikweta ziko mistari ya duara za latitudo ziinazotajwa kwa nyuzi 1-90 za kaskazini au nyuzi 1-90 za kusini.

  1. Matt Rosenberg: What is the Prime Meridian?, tovuti ya thoughtco ya tar 1-9-2018, iliangaliwa Septemba 2019

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu: