Majira ya mvua

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Msimu wa mvua)
Majira ya mvua huko Morogoro, Tanzania.

Majira ya mvua (pia: msimu wa mvua) ni kipindi cha kila mwaka cha mvua nyingi, hasa katika tropiki. Hali ya hewa katika nchi za tropiki inatawaliwa na ukanda wa mvua wa kitropiki, ambao hutoka kaskazini hadi kusini mwa tropiki na kurudi katika kipindi cha mwaka mmoja. Nje ya tropiki, majira ya mvua yanaweza kuwa wakati wa majira ya joto au ya baridi kulingana na tabianchi ya eneo husika.

Ukanda wa mvua wa kitropiki[hariri | hariri chanzo]

Ukanda wa mvua wa kitropiki uko katika nusudunia ya kusini takriban kuanzia Oktoba hadi Machi na kwa hivyo kunanyesha sana pale na takriban siku zote zina mawingu. Kuanzia Aprili hadi Septemba ukanda wa mvua uko katika nusudunia ya kaskazini na kuletea eneo hili mvua nyingi. Kulingana na Uainishaji wa hali ya hewa wa Köppen kwa hali ya hewa ya tropiki, mwezi wa mvua hufafanuliwa kama mwezi ambapo wastani wa mvua ni juu ya mm 60 [1].

Ukanda wa mvua hufika kaskazini takriban kama Tropiki ya Kansa na kusini takriban kama Tropiki ya Kaprikoni. Karibu na latitudo hizo kuna msimu mmoja wa mvua na msimu mmoja wa kiangazi kila mwaka. Kwenye ikweta kuna misimu miwili ya mvua na miwili ya kiangazi, wakati ukanda wa mvua hupita mara mbili kwa mwaka, mara moja kuelekea kaskazini na mara moja kuelekea kusini. Kati ya Tropiki na ikweta maeneo yanaweza kukumbwa na msimu mfupi wa mvua (vuli) na msimu mrefu wa mvua (masika) na kiangazi kifupi na kiangazi kirefu. Jiografia ya maeneo mahususi inaweza kurekebisha mifumo hiyo ya hali ya hewa kwa kiasi kikubwa. Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda na kaskazini mwa Tanzania kuna misimu miwili ya mvua na kusini mwa Tanzania kuna msimu mmoja.

Hulka ya mvua[hariri | hariri chanzo]

Mafuriko huko Jangwani jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Mvua wakati wa majira ya mvua kwa kawaida huwa kubwa zaidi au hudumu kwa muda mrefu zaidi. Hasa kwa vile sayari ya Dunia inazidi kuwa na joto, mvua zinazidi kuwa kubwa huku mvua nyingi za kushangaza zikinyesha kwa muda mfupi. Hii inazidi kusababisha mafuriko makubwa na kuleta nayo kifo na uharibifu. Sababu yake ni kwamba hewa ya joto ina zaidi ya mvuke wa maji, ambayo chini ya hali nzuri hutolewa ghafla.

Mchoro wa Seli ya Hadley.

Mvua katika ukanda wa mvua wa kitropiki husababishwa na joto la Jua, ambalo huwa karibu juu ya kichwa wakati wa majira ya mvua. Hii husababisha kiasi kikubwa cha maji kuyeyuka kutoka bahari, maziwa na hata mimea, hasa misitu. Hewa yenye joto na unyevunyevu huinuka angani na kuenea kaskazini na kusini. Juu angahewani, ambapo halijoto ni ya chini sana, mvuke wa maji hutoneshwa na kuunda mawingu ya vitone. Hivyo vinapofikia ukubwa fulani, haviwezi tena kubaki vikiwa vimening'inia hewani, basi huanguka chini kama mvua. Hewa baridi na kavu inayobaki inasukumwa na hewa ya joto inayoendelea kuinuka kisha kushuka chini ambapo hutiririka kurudi mahali ambapo hewa inainuka (Seli ya Hadley)[2]. Hii inahisiwa kama upepo na inaitwa upepo wa monsuni au wa biashara.

Magonjwa[hariri | hariri chanzo]

Baadhi ya magonjwa yanakuwa ya kawaida wakati wa mvua. Mvua husafirisha uchafu unaobeba vijidudu kutoka ardhini hadi kwenye maji. Unywaji wa maji hayo kwa kukusudia au kwa bahati mbaya baadaye unaweza kusababisha maambukizi ya tumbo na kusababisha kuhara au hata hali mbaya zaidi kama vile homa ya matumbo na kipindupindu. Kwa kuwa hali ya joto inaweza kuwa ya chini, maambukizi ya mfumo wa upumuaji huwa yanaongezeka. Hizi mara nyingi ni mafua ya kawaida lakini pia mabaya zaidi kama homa ya mafua na siku hizi hata Covid-19. Kuloweshwa na mvua kunaweza kusababisha joto la mwili kushuka, jambo ambalo pia huwafanya watu kupatwa zaidi na maambukizi hayo. Majira ya mvua hutengeneza maji mengi zaidi ya wazi, ambayo hutoa fursa zaidi kwa mbu kuzaliana. Kuongezeka kwa idadi yao husababisha kuongezeka kwa magonjwa yanayoenezwa na wadudu kama vile malaria na kidingapopo. Ndiyo asili ya methali ya Kiswahili isemayo: "Hakuna masika bila mbu".

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Updated world Köppen-Geiger climate classification map.
  2. L., Hartmann, Dennis (2016-01-02). Global physical climatology. Elsevier. pp. 165–76. ISBN 9780123285317. OCLC 944522711.