Nenda kwa yaliyomo

Kidudu-gurudumu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kidudu-gurudumu
Mfano wa kidudu-gurudumu (Habrotrocha rosa)
Mfano wa kidudu-gurudumu (Habrotrocha rosa)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia
Nusuhimaya: Eumetazoa
Faila ya juu: Platyzoa
Faila: Rotifera
Cuvier, 1798
Ngazi za chini

Ngeli za juu 2, ngeli 3:

Vidudu-gurudumu (Kiing. rotifer, yaani mbeba (fer) gurudumu (rota)) ni wanyama wadogo sana wa faila Rotifera ambao wanabeba nywele fupi sana au silio kuzunguka kinywa zinazofanana na gurudumu linalodura zikisogea. Takriban spishi zote huonekana chini ya hadubini tu, hata hivyo ni viumbe vyenye seli nyingi.

Maumbo mbalimbali ya vidudu-gurudumu.
Nyekundu - kichwa, buluu - kiwiliwili, nyeupe - mguu.

Vidudu-gurudumu wana ulinganifu wa pande mbili na aina za maumbo tofauti. Mwili wao umegawanyika katika kichwa, kiwiliwili na mguu, na kwa kawaida una umbo la mcheduara. Kuna kutikula iliyokua vizuri na inayoweza kuwa nene na ngumu, ambayo inampatia mnyama umbo la sanduku, au kinamo, ambayo inampatia umbo la mnyoo. Vidudu-gurudumu kama huo huitwa loricate na illoricate mtawalia. Kutikula ngumu mara nyingi huundwa na sahani nyingi na inaweza kubeba miiba, matuta au mapambo mengine. Kutikula yao haina khitini lakini imeundwa kwa protini zilizoimarishika.

Sifa mbili bainifu zaidi za vidudu-gurudumu wa kike wa spishi zote ni kuwepo kwa corona (taji) kichwani, muundo unaobeba silio katika jenasi zote isipokuwa Cupelopagis, na kuwepo kwa mastaksi au koromeo ya kutafuna. Katika spishi za zamani zaidi taji huunda mviringo sahili wa silio kuzunguka kinywa ambalo kutoka kwake mstari wa ziada wa silio huenea nyuma ya kichwa. Katika idadi kubwa ya vidudu-gurudumu, hata hivyo, hii imebadilika kuwa muundo tata zaidi.

Marekebisho ya mpango wa msingi wa taji ni pamoja na mabadiliko ya silio katika nywele ngumu au sekini kubwa na ama upanuzi au kupoteza kwa mstari wenye silio kuzunguka kichwa. Katika jenasi kama vile Collotheca taji limerekebishika kuunda faneli inayozunguka kinywa. Katika spishi nyingi, kama zile za jenasi Testudinella, silio kuzunguka kinywa zimetoweka na kuacha tu mistari miwili midogo ya duara kichwani. Katika Bdelloidea mpango huu umerekebishika zaidi na ukanda wa juu ukigawanyika katika magurudumu mawili yanayoduru na yaliyoinuka juu ya kiweko kinachotokeza kutoka kwenye uso wa juu wa kichwa.[1]

Kiwiliwili huunda sehemu kuu ya mwili na hufunika viungo vingi vya ndani. Mguu unatokeza kutoka kwa nyuma ya kiwiliwili na kwa kawaida ni nyembamba zaidi, ambayo inampatia mwonekano wa mkia. Kutikula juu ya mguu mara nyingi huunda miviringo, ambayo inafanya uonekane kuwa na pingili, ingawa muundo wa ndani ni sare. Vidudu-gurudumu wengi wanaweza kurudisha mguu kwa sehemu au kabisa katika kiwiliwili. Mguu huishia kwa vidole kutoka kimoja hadi vinne, ambavyo, katika spishi zilizokaa na kutambaa, huwa na tezi za wambiso ili kumwambatisha mnyama kwenye uso wa chini. Katika spishi nyingi zinazoogelea huru ukubwa wa mguu kwa ujumla umepunguka na mguu unawezza kutokuwapo.[1]

Vidudu-gurudumu wa kiume ni wadogo sana kuliko majike, hadi mara kumi wadogo zaidi. Hawali na kwa hivyo hawana taji wala mkundu, hata hivyo, kuna mfumo wa mmeng'enyo wa chakula usio na kazi.

Uzazi na mzunguko wa maisha

[hariri | hariri chanzo]

Vidudu-gurudumu ni wa kike au wa kiume na kwa hivyo wana uzaziwenza (dioecy). Huzaa kingono au kwa pathenojenesisi. Wanaonyesha udimofi wa kijinsia huku majike wakiwa wakubwa kila wakati kuliko madume. Katika spishi fulani hii ni kiasi kidogo, lakini kwa wengine jike anaweza kuwa hadi mara kumi ya ukubwa wa dume. Katika spishi za kipathenojenesisi, madume wanaweza kuwepo tu nyakati fulani za mwaka au kutokuwepo kabisa.[1]

Mfumo wa uzazi wa jike huwa na ovari moja au mbili kila moja ikiwa na tezi ya kiiniyai ambacho mayai huhitaji. Pamoja, kila ovari na tezi ya kiiniyai huunda muundo wa seli moja yenye viini vingi katika sehemu ya mbele ya mnyama na unafungua kupitia kirijaova ndani ya kloaka.[1]

Kwa kawaida madume hawana mfumo wa mmeng'enyo wa chakula unaofanya kazi na kwa hivyo huishi kwa muda mfupi. Mara nyingi huwa na uwezo wa uzazi mara tu wakizaliwa. Wana pumbu moja na kirijamanii zinazounganishika na jozi ya miundo ya tezi inayojulikana kama vibofushahawa (visivyohusiana na kibofushahawa cha vertebrata). Kirijamanii hufunguka katika gonopor kwenye sehemu ya nyuma ya mnyama ambayo kwa kawaida hurekebishika kuunda mboo. Gonopori ina homolojia na kloaka ya majike, lakini katika spishi nyingi haina mwunganisho na utumbo.[1]

Faila Rotifera huambatanisha ngeli tatu ambazo huzaa kwa njia tatu tofauti: Seisonidea huzaa tu kingono; Bdelloidea huzaa kipathenojenesisi bila ngono tu; Monogononta huzaa kwa kupishana mifumo hii miwili ("pathenojenesisi kwa mzunguko" au "heterogonia")[2]. Pathenojenesisi bila muunganisho wa gameti hutawala mzunguko wa maisha wa Monogononta na hivyo inasaidia ukuaji wa haraka wa idadi yao na kuingia kila mahali. Katika awamu hii madume hawapo na majike hutaga mayai ya diploidi kupitia mitosisi ambayo hukua kipathojenesisi kuwa majike walio wapachisho wa mama wao[2]. Baadhi ya majike hawa wanaweza kuzaa majike ambao watataga mayai ya haploidi kupitia meiosisi. Hii husababishwa na aina tofauti za vichocheo kulingana na spishi. Mayai ya haploidi hukua kuwa madume kibete wa haploidi iwapo hayatatungishwa na kuwa "mayai ya kupumzika" ya diploidi (au "mayai yanayotua ukuaji") ikiwa yatatungishwa na madume.

Utungisho ni wa ndani. Madume ama huingiza uume wao kwenye kloaka ya jike au kuutumia kupenya ngozi yake na kuingiza shahawa katika uwazi wa mwili. Yai hutoa ganda na linaunganishwa ama kwenye uso wa chini, mimea ya karibu, au kwenye mwili wa jike mwenyewe. Spishi chache, kama vile wana wa Rotaria, huangua mayai tumboni kabla kuzaa wachanga.[1]

Takriban spishi zote huanguliwa kama matoleo madogo ya mpevu. Spishi zinazokaa chini, hata hivyo, huzaliwa wakiwa lava wanayoogelea huru ambao hufanana kwa karibu na wapevu wa spishi zinazohusiana nao na zinazoogelea huru. Majike hukua haraka na kufikia ukubwa wao wa wapevu ndani ya siku chache, huku madume kwa kawaida wasipokua kwa ukubwa kabisa.[1]

  1. 1.0 1.1 1.2 1.3 1.4 1.5 1.6 Barnes, Robert D. (1982). Invertebrate Zoology. Philadelphia, PA: Holt-Saunders International. ku. 272–286. ISBN 978-0-03-056747-6.
  2. 2.0 2.1 Nogrady, T., Wallace, R.L., Snell, T.W., 1993. Rotifera vol.1: biology, ecology and systematics. Guides to the identification of the microinvertebrates of the continental waters of the world 4. SPB Academic Publishing bv, The Hague.