Ngeli

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Ngeli ni makundi ya kisarufi ya majina katika lugha ya Kiswahili na lugha nyingine za Kibantu.

Kwa maneno mengine, ngeli za nomino ni utaratibu unaotumika kuweka nomino katika matabaka au makundi yanayofanana.

Mifano
 1. Maji yakimwagika hayazoleki
 2. Mayai yaliyooza yananuka sana
 3. Yai lililooza linanuka sana
 4. Maji lililomwagika hayazoleki

Katika mifano hiyo juu tunaona kwamba sentensi a, b na c ziko sahihi wakati sentensi d si sahihi, kwa sababu imekiuka upatanisho wa kisarufi. Kwa maana hiyo sentensi ‘a’ ipo katika ngeli ya YA-YA na sentensi b na c zipo katika ngeli ya LI-YA. Sentensi d si sahihi kwa sababu nomino maji haina umoja, kwa hiyo haiwezi kuingia katika ngeli ya LI-YA. Kwa msingi huo ngeli za nomino huzingatia sana upatanisho wa kisarufi.

Kwa ujumla, ngeli za Kiswahili huainishwa kulingana na viambishi mbalimbali ambavyo nomino tofauti huchukua katika umoja na wingi.

Mipangilio na idadi yake[hariri | hariri chanzo]

Jedwali lifuatalo linaonesha ngeli za nomino kwa misingi ya upatanisho wa kisarufi.

Ngeli Ufafanuzi Mifano
A-WA Ngeli hii inahusisha majina ya viumbe hai kama vile watu, wanyama, ndege, wadudu n.k Sungura mjanja ameumia

Sungura wajanja wameumia

Mkuu anawasili

LI-YA Majina yenye kiambishi awali li- katika umoja na ya- katika wingi huingia katika ngeli hii Jambia la babu limepotea

Majambia ya babu yamepatikana

KI-VI Ni ngeli ya majina ya vitu visivyo hai, yanayoanza kwa KI- au CH- (umoja); na VI- au VY- (wingi). Pia ngeli hii hujumuisha majina ya vitu vingine katika hali ya udogo k.v, kijito, kilima Chakula kimekwisha

Vyakula vimekwisha

Kijito kimekauka

Vijito vimekauka

U-I Huwakilisha majina ya vitu visivyo hai, yaanzayo kwa sauti M- (umoja) na MI- (wingi). Pia majina ya baadhi ya viungo vya mwili huingia humu, kwa mfano mkono, mguu, mkia n.k Mlima umeporomoka

Milima imeporomoka

Mkono umevunjika

Mikono imevunjika

Mto huu una mamba wengi

Mito hii ina mamba wengi

U-ZI Hurejelea majina ambayo huanza kwa U- (umoja) na huchukua ZI- kama kiambishi kiwakilishi cha ngeli katika wingi. Majina yenye silabi tatu au zaidi hubadilishwa kwa wingi kwa kutoa sauti /u/' k.v ukuta-kuta. Majina ya silabi mbili huongezewa /ny/ katika wingi. k.v ufa - nyufa Ukuta umebomoka

Kuta zimebomoka

Wimbo huu unavutia

Nyimbo hizi zinavutia

Ufa umeonekana

Nyufa zimeonekana

I-ZI Hutumiwa kwa majina yasiyobadilika kwa umoja wala kwa wingi lakini huchukua viambishi viwakilishi tofauti: I- (umoja) na ZI- (Wingi). Nyumba imejengwa

Nyumba zimejengwa

Salam imefika

Salam zimefika

U-YA Ngeli hii inajumuisha nomino ambazo zina kiambishi awali u- katika umoja na ma- katika wingi. Ukuu umekuponza

Makuu yamekuponza

Unyoya unapepea

Manyoya yanapepea

KU Majina yanayotokana na vitenzi yanayoanza na ku- (vitenzi-jina) Kusoma kwako kumekusaidia

Kuchelewa kumemponza

PA/MU/KU- Huonesha mahali Amekaa pale palipo na wadudu wengi

Amelala mule mulimojaa siafu.

Amepita kule mbali

Matumizi ya ngeli[hariri | hariri chanzo]

Hapa tunaona dhima ya matumizi yake.

 • Hutumika kupanga majina ya lugha katika makundi yaliyoshikamana na kutofungamana kutokana na kigezo muhimu.
 • Hutumika kutambulisha maumbo ya umoja na wingi katika majina na vivumishi.
 • Hutumika katika upatanishi wa kisarufi katika sentensi.
 • Hutumika katika kuonyesha uhusiano uliopo baina ya lugha za Kiswahili na lugha nyingine.

Dhana ya O-rejeshi[hariri | hariri chanzo]

O-rejeshi ni kiambishi kinachotumiwa kurejelea nomino ambayo huwa imetajwa kabla ya kitenzi chenyewe kutajwa. Viambishi hivyo ndivyo vinavyosababisha utegemezi katika sentensi.

Dhima kuu ya muundo wa O-rejeshi[hariri | hariri chanzo]

Hutumika kama kirejeshi. Kwa mfano:

 • Mtu aliyepigwa jana na wananchi ni mfanyabiashara wa Mwanza.
 • O-rejeshi hudokeza mahali. Kwa mfano; rudisha ulipokitoa!
 • O- rejeshi hudokeza wakati. Kwa mfano; Alipokuja alinikuta nimelala.
 • Vilevile hutumika kama kiunganishi. Kwa mfano; Alikuja. Nilikuwa nimelala (alipokuja alinikuta nimelala)
 • Hudokeza namna. Mfano; Kila mtu anashangaa alivyoumia.

Kwa jumla, ngeli za Kiswahili huainishwa kulingana na viambishi mbalimbali ambavyo nomino tofauti huchukua katika umoja na wingi.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]