Giovanni da Palestrina

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Giovanni Pierluigi da Palestrina.

Giovanni Pietro Aloisio Sante da Palestrina (Palestrina karibu na Roma, 2 au 3 Februari 1514 au 1515 [1]; Roma, 2 Februari 1594) alikuwa mtunzi wa muziki kutoka nchini Italia anayesifiwa kama mtengenezaji wa muziki wa kiroho wa Ulaya.

Mara nyingi alitajwa kuwa kilele cha muziki wa sauti nyingi wakati wa Renaissance, akawa na athira kubwa kwa maendeleo ya muziki wa Kikristo.

Upande wa dini, alikuwa Mkristo wa Kanisa Katoliki, tena mwanachama wa Utawa wa Tatu wa Mt. Fransisko.

Jina[hariri | hariri chanzo]

Jina la familia lilikuwa Sante; da Palestrina inataja mahali alikotoka. Jina "Giovanni" ni umbo la Kiitalia kwa "Yohane" na Pierluigi ni kifupi cha Pietro Aloisio. Kwa kawaida anatajwa kwa kifupi kama Palestrina tu. Wakati mwingine alitumia umbo la Kilatini la jina lake kuwa Johannes Petraloysius Praenestinus.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Palestrina alizaliwa mjini Palestrina takriban mwaka 1525 kama mwana wa Sante na Palma Pierluigi .

Mwaka 1540 alihamia Roma alipopata masomo ya muziki katika shule ya Claude Goudimel.

Ajira ya kwanza ilikuwa kuanzia 1544 hadi 1551 akiwa mpigakinanda katika kanisa kuu la Palestrina.

Mwaka 1551 alipokea wito kuwa Magister puerorum (mwalimu wa kwaya ya wavulana) kwenye Basilika la Mt. Petro mjini Roma. akaendelea kuwa mkurugenzi wa muziki wa kanisa hilo kubwa kuliko yote duniani, lililokuwa tayari kanisa la Mapapa.

Alipendwa na Papa Julius III na Papa Marcello II, lakini mwandamizi wao Papa Paulo IV alisikitika ya kwamba hakuwa padre, pia alioa, kwa hiyo alipaswa kuondoka katika Basilika hilo la Vatikano.

Hapo aliajiriwa katika Kanisa kuu la Roma, yaani Basilika la San Giovanni huko Laterano na kuanzia mwaka 1561 kwenye basilika lingine la mji huohuo, Santa Maria Maggiore.

Wakati ule alitunga muziki wa sauti nane wa kwaya mbili kwa ajili ya ibada ya Ijumaa Kuu iliyovuta wasikilizaji kiasi kwamba Papa Pius IV aliomba nakala kwa ajili ya kanisa lake mwenyewe.

Kutokana na sifa zake alialikwa kuhudhuria kwenye mikutano ya baraza la kanisa kwa ajili ya muziki kanisani iliyojadili swali la kama muziki wa sauti nyingi ilifaa kutumika kanisani au la. Kwa niaba ya baraza hilo alitunga muziki wa misa tatu ambako alifaulu kuunganisha muziki wa sauti nyingi na kueleweka kwa maneno ya matini ya Biblia yaliyoimbwa.

Mchoro mwingine wa Giovanni Pierluigi da Palestrina.

Mtindo huo uliendelea kwa kazi ya watungaji wengine ukajulikana kama "mtindo wa Palestrina".

Sifa za Palestrina zilileta maagizo ya kazi zake na viongozi wengine kama mtemi wa Mantova, Guglielmo Gonzaga. Huyu alijenga kanisa jipya kwa ikulu yake, "Basilica Palatina di Santa Barbara", akaagiza misa 10 za Palestrina zitungwe kwa kanisa lake jipya, ambazo sasa zinajulikana kwa jina la "misa za Mantova" (Missae Mantovanae).

Mwaka 1571 Palestrina alirudishwa kuwa mkurugenzi wa muziki wa kanisa la Papa.

Aliaga dunia tarehe 2 Februari 1594, akazikwa katika Basilika la Mt. Petro. Maandishi kwenye kaburi lake yanamsifu kuwa Musicae princeps ("Mtemi wa muziki“).

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. kulingana na vyanzo tofauti pia 1524, 1525 au 1529

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu:


Makala hii kuhusu mwanamuziki fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Giovanni da Palestrina kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.