Vita ya Uingereza dhidi ya Zanzibar
Vita ya Uingereza dhidi ya Zanzibar (kwa Kiingereza: Anglo-Zanzibar War) ilikuwa vita ilivyopigwa kati ya Uingereza na Usultani wa Zanzibar tarehe 27 Agosti 1896. Mapigano yote yalidumu kati ya dakika 38 na 45. Hivyo hutajwa mara nyingi kama vita fupi kabisa katika historia ya dunia. Uingereza ilishinda.
Mandharinyuma
[hariri | hariri chanzo]Sababu yake ilikuwa suala la ufuatano kwenye utawala wa Zanzibar. Sultani Hamad bin Thuwaini alifariki tarehe 25 Agosti 1896. Waingereza waliwahi kutangaza Zanzibar kuwa nchi chini ya ulinzi wao na mapatano ya 14 Juni 1890 baina ya Uingereza na Sultani Ali bin Said yaliwapa haki ya kumkubali au kumkataa sultani mpya atakayemfuata mtangulizi wake[1]. Wenyewe walilenga kumwona Hamud bin Muhammed kuwa sultani mpya aliyekuwa mpwa wa marehemu. Kwa umri alikuwa mkubwa kati ya hao walioweza kufuata, na Waingereza walitegemea kuwa na sultani mtiifu.
Seyyid Khalid anatwaa mamlaka
[hariri | hariri chanzo]Sultani Hamad aliaga dunia ghafla asubuhi ya 25 Agosti. Saa chache baadaye binamu yake kijana Seyyyid Khalid bin Barghash alifika kwenye Jumba la Sultani akajitangaza kuwa sultani mpya. Alitambuliwa na kikosi cha askari wa ulinzi na sehemu ya familia ya kifalme. Jioni ya tarehe 25 alikuwa sultani.
Majadiliano kati ya balozi wa Uingereza na Seyyid Khalid
[hariri | hariri chanzo]Kaimu konsuli Mwingereza Basil Cave alifika kwake akamwonya kwamba hataweza kuwa mtawala na hatambuliwi na Uingereza kulingana na mapatano ya 1890. Khalid alianza kukusanya wanamgambo Wazanzibari pamoja na kikosi cha ulinzi wa jumba lake. Jeshi rasmi la Zanzibar lilikuwa chini ya Mwingereza Lloyd Mathews ambaye hakumtambua Khaled kama sultani akaweka kikosi chake kwa ulinzi wa balozi za kigeni.
Ilhali manowari 2 za Uingereza zilikuwepo tayari kwenye bandari ya Zanzibar, siku iliyofuata manowari 2 nyingine zilifika pia pamoja na admirali Rawson, mkuu wa wanamaji Waingereza katika Afrika ya Mashariki[2]. Kaimu Konsuli Cave aliuliza London kwa njia ya telegrafu kama anaruhusiwa kutumia silaha kama Khaliud hatakubali kuondoka akapata jibu kwamba aliruhusiwa kuchukua hatua yoyote lakini asifanye kitu kama hana uhakika kwamba atafaulu.[3]
Admirali Rawson alimwandikia Khalid ujumbe kuwa anapewa nafasi hadi saa 3 asubuhi iliyofuata kuondoka katika jumba la sultani au manowari zake zitaanza kufyatua risasi.
Tarehe 27 Agosti asubuhi kaimu konsuli Cove alituma tena ujumbe wkwa Khalid. Khalid alijibu kwamba hataki kushusha bendera, haamini Waingereza wataanza kumfyatulia risasi. Cove akajibu asingependa lakini atafanya.
Mapigano ya 27 Agosti
[hariri | hariri chanzo]Saa tatu na dakika mbili asubuhi mizinga ya manowari 3 za Waingereza zilianza kurusha mabomu yao kwenye ukingo ambako askari, wanamgambo na watumwa karibu 3000 wa Sultani walikusanyika wakishika silaha zao. Mizinga kadhaa ya sultani ilijaribu kurudisha risasi lakini zilinyamazishwa haraka. Silaha za Waingereza zilikuwa za kisasa ilhali silaha za sultani zilikuwa mkusanyo wa mizinga na bunduki za vizazi vilivyopita.
Meli ndogo ya sultani "Glasgow" ilikwenda katikati ya manowari kubwa za Waingereza ikazifyatulia kwa mzinga mmoja iliokuwa nao ikazamishwa baada ya dakika chache.[4]
Khalid alikimbia akapata kimbilio kwenye ubalozi wa Ujerumani.
Saa tatu na dakika arobaini mizinga ya Waingereza ilinyamaza na wanamaji kutoka meli walifika ufukoni ambako hawakuta tena upinzani. Wazanzibari 500 walikuwa wamekufa, Waingereza walitumia risasi 500 za mizinga, 4,100 za bombomu, na 1,000 za bunduki.
Jioni ya tarehe 27 Agosti Hamud bin Mohammed alisimikwa kama sultani mpya wa Zanzibar. Khalid alikaa siku chache kwenye ubalozi wa Ujerumani hatimaye akachukuliwa na manowari ya Kijerumani akapelekwa Dar es Salaam alipoishi hadi mwaka 1916 katika koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. Wakati Waingereza walipovamia Dar es Salaam wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Khalid alikamatwa nao na kupelekwa Shelisheli halafu Morisi uhamishoni. Baada ya vita kwisha aliweza kurudi akaishi Mombasa hadi kifo chake kwenye mwaka 1927.
Vita iliashiria kumalizika kwa Usultani wa Zanzibar kama nchi huru na kuanza kwa kipindi cha ushawishi mzito wa Waingereza.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Provisional agreement concluded between the Sultan of Zanzibar and Her Britannic Majesty's Agent and ConsulGeneral (subject to the approval of Her Majesty's Government), respecting the British Protectorate of the Sultan's dominions, Succession to the Throne of Zanzibar, Zanzibar 14th June, 1890; in Map of Africa by Treaty, Vol. I. Nos. 1 to 94. BRITISH COLONIES, PROTECTORATES AND POSSESSIONS IN AFRICA (online via archive.org)
- ↑ [yafuatayo kufuatana na kumbukubu ya konsuli Mwingereza katika Zanzibar; Arthur H . Hardinge: A Diplomatist in the East, Jonathan Cape London 1928, uk. 190 f online japa kupitia archive.org
- ↑ “You are authorised to adopt whatever measures you may consider necessary, and will be supported in your action by Her Majesty’s Government. Do not, however, attempt to take any action which you are not certain of being able to accomplish successfully.” [https://medium.com/lessons-from-history/the-shortest-war-in-history-48a30176c2b7 The shortest War in History], tovuti ya Lessons from History
- ↑ "Zanzibar Courage". www.zanzibarhistory.org. Iliwekwa mnamo 2021-03-15.
Vyanzo vya Nje
[hariri | hariri chanzo]- https://www.historic-uk.com/HistoryUK/HistoryofBritain/The-Shortest-War-in-History/ The shortest War in History, tovuti ya historic-uk.com
- https://www.britannica.com/event/Anglo-Zanzibar-War Anglo-Zanzibar War, tovuti ya Britannica
- Appiah, K. Anthony; Gates, Henry Louis, Jr., whr. (1999), Africana: The Encyclopedia of the African and African American Experience, New York: Basic Books, ISBN 978-0-465-00071-5
{{citation}}
: CS1 maint: multiple names: editors list (link). - Ayany, Samuel G. (1970), A History of Zanzibar: A Study in Constitutional Development, 1934–1964, Nairobi: East African Literature Bureau, OCLC 201465.
- Keane, Augustus H. (1907), Africa, juz. la 1 (tol. la 2nd), London: Edward Stanford, OCLC 27707159.
- Scientific American (26 Septemba 1896), "Zanzibar", Scientific American, 42 (1082): 17287–17292
{{citation}}
: CS1 maint: date auto-translated (link).