Telegrafu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Telegrafu ya kihistoria nchini Ujerumani ilitumia alama za mikono ya ubao kwa kuonyesha herufi

Telegrafu (ing. telegraph; kutoka gir. τῆλε tele "mbali", na γράφειν graphein "andika") ni njia ya kupeleka habari andishi kwa mpokeaji wa mbali bila kubeba barua kwake.

Telegrafu zilizotumiwa wakati wa karne za 19 na 20 zilipitisha ujumbe kwa mkondo wa umeme uliopitia kwenye waya. Telegrafu za zamani zaidi zilitumia alama za nuru au kwa alama nyingine zilizoonekana kwa mbali.

Alfabeti ya Morse ilikuwa msingi kwa uenezaji wa telegrafu

Kwa njia hii herufi za alfabeti zilitafsiriwa kwa alama zilizoweza kupitishwa kirahisi.

Baada ya majaribio mbalimbali mbinu wa Samuel Morse ulifaulu mwaka 1844 na kusababisha uenezaji wa teknolojia hii kote duniani. Morse alitafsiri kila herufi katika mfumo wa alama fupi au ndefu zinazoweza kuandikwa kama mfuatano wa nukta na mstari au kutumwa kama alama fupi au ndefu ya nuru, sauti au umeme na kadhalika. Mashine ndogo ilitafsiri alama hizi katika mishtuko ya umeme iliyoweza kuchora tena alama katika mashine upande mwingine wa waya ambako sumaku ya umeme uliweza kusukuma kalamu juu ya karatasi. [1]

Mawasiliano kwa telegrafu yaliwezesha mara ya kwanza kutuma habari kote duniani katika muda mfupi. Magazeti na makampuni makubwa ya kiuchumi yalitangulia kutumia teknolojia hii, na serikali na jeshi zilifuata. Nyaya kubwa zilipitishwa kutoka nchi hadi nchi na pia kwenye tako la bahari kwa mawasiliano baina mabara. Katika karne ya 20 yalianza pia matumizi ya simu za upepo kwa habari za telegrafu.

Makampuni ya telegrafu zilipokea ujumbe ulioitwa "telegramu" kutoka wateja na kuzituma kwa mi au nchi nyingine; pale ziliandikwa tena kwenye karatasi na kupelekwa kwa mtu aliyeandikiwa. Makampuni yale yalipokea pesa kwa kila herufi iliyowasilishwa hivyo ujumbe ulikuwa mfupi.

Tangu kupatikana kwa simu matumizi ya telegrafu yalipungua lakini bado zilitumwa hadi kupatikana kwa simu za mkononi na barua pepe. Katika nchi mbalimbali huduma zilifungwa kuanzia mwaka 2000 hivi, katika nchi nyingine huduma bado iko. [2]

Mwanamaji anatumia taa ya pekee kwa ujumbe wa nuru akitumia alama za Morse


Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Telegraph. 150.si.edu (2007 [last update]). Iliwekwa mnamo November 26, 2011.
  2. Siegel, Robert (February 2, 2006). Western Union Sends Its Last Telegram : NPR. npr.org. Iliwekwa mnamo November 26, 2011.
Commons-logo.svg
Wikimedia Commons ina media kuhusu: