Nenda kwa yaliyomo

Mtagusano sumakuumeme

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Sumakuumeme)

Mtagusano sumakuumeme (ing. electromagnetic force au electromagnetic interaction) ni moja kati ya kani msingi wa ulimwengu.

Mtagusano huu unasababisha mambo mengi tunayoyaona kila siku kama vile nuru, umeme na usumaku. Ni kani ya kimsingi pia kwa kuamulia tabia za molekuli na atomi.

Jina[hariri | hariri chanzo]

Jina la "sumakuumeme" ni tafsiri ya gir. / ing. "electromagnetic" inayotokana na maneno ya Kigiriki ἢλεκτρον, ēlektron (kaharabu[1]) na μαγνήτης, magnetis (sumaku).

Historia ya uchunguzi wa usumakuumeme[hariri | hariri chanzo]

Umeme na usumaku ni nyuso mbili za jambo lilelile.

Kwa karne nyingi wataalamu waliona umeme na usumaku ni kani mbili tofauti. Tangu mwanzo wa karne ya 19 wanasayansi walitambua uhusiano wa karibu kati ya hizi mbili.

Hans Christian Ørsted aliona mwaka 1820 ya kwamba kutirikika kwa chaji ya umeme katika waya kunavuta sindano ya sumaku na hivyo kunaunda uga wa sumaku.

Wengine waliendelea kujenga juu ya matokeo yake na Mskoti James Clerk Maxwell alieleza misingi ya nadharia ya uga wa sumakuumeme katika hesabu inayoitwa milinganyo ya Maxwell. Alifaulu kuunganisha maelezo kwa ajili ya umeme, usumaku na elimumaonzi kuwa pande mbalimbali za kitu kilekile, yaani uga wa sumakuumeme. Alitabiri kuwepo kwa mawimbi ya sumakuumeme na nuru kuwa umbo mojawapo la mawimbi haya.

1873 alitoa kitabu chake "Treatise on Electricity and Magnetism" (tasinifu kuhusu umeme na usumaku) alipojumlisha maelezo yake. Alionyesha kuwa kuathiriana kwa chaji hasi na chaji chanya kunasababishwa na kani 1 tu akaonyesha matokeo manne makuu kutokana na hii:

  • Chaji za umeme zinavutana au zinawingana kwa kani ya kuwiana kinyume cha mraba wa umbali kati yao. Chaji sawa zinavutana, chaji tofauti zinawiana.
  • Ncha sumaku zinavutana au kuwiana kwa namna hiyohiyo. Ncha sumaku zinapatikana daima kwa jozi: kila ncha sumaku ya kaskazini huwa na ncha sumaku ya kusini.
  • Mkondo wa umeme katika waya unaunda uga wa sumaku mwenye umbo la duara kwenye mwendo wa waya hii. Mwelekeo wake unategemea mwelekeo wa mkondo husika.
  • Mkondo wa umeme unadukizwa (yaani kusababishwa) katika tanzi la waya kama sumaku inapitishwa kukaribia au kwenda mbali na tanzi hili; sawasawa kinyume kama tanzi lenyewe linasogezwa kwenyesumaku au kutolewa kuwa mbali na sumaku.

Hasa tokeo la mwisho lilikuwa msingi kwa kuanzisha mitambo ya kutengeneza umeme kwa mashine kama jenereta.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Kaharabu inaonyesha tabia za umeme baada ya kusuguliwa.