Telegramu
Telegramu (kutoka Kigiriki tele: mbali na gramma: andiko, herufi) ni ujumbe wa kuandikwa unaopitishwa na huduma ya posta au kampuni ya telegrafu kwa njia ya umeme na waya. Upande wa kupokea telegramu unaandikwa kwenye karatasi na kutumwa kwa mpokeaji.
Telegramu zilikuwa njia ya kuwasilisha ujumbe haraka kuanzia katikati ya karne ya 19 hadi mwisho wa karne ya 20. Zilitumiwa sana kwa sababu simu za binafsi hazikuwa kawaida. Siku hizi huduma hii imeshasimamishwa katika nchi mbalimbali kwa sababu hazihitajiki tena kutokana na uenezaji wa simu za mkononi na barua pepe.
Pale mwanzoni huduma ya telegrafu ilitumia mfumo wa Samuel Morse ambako mtumishi aligonga kifaa kilichotuma mishtuko mifupi na mirefu ya umeme kupitia waya kwa mtumishi mwingine. Kila herufi iliwakilishwa kwa ufuatano wa mishtuko hizi, mfano mshtuko mrefu na mfupi kama –· kwa "a" au ufuatano wa mishtuko mirefu na mifupi miwili-miwili kama ––·· kwa "z". Mtumishi upande wa kupokea ama alisikia mishtuko hii kama sauti au aliziona kama ufuatano wa nukta na mistari uliotoka katika mashine ndogo iliyoweza kuchora alama hizi kwenye karatasi. Baadaye kazi hii ilirahisishwa kwa mashine ya taipu zilizoweza kubadilisha maandishi kwa mishtuko ya umeme na kinyume.
Pale mwanzoni teknolojia hii ilitumiwa na makampuni ya reli, baadaye pia kati ya miji kama huduma za posta. Tangu mwaka 1850 nyaya za kwanza zilitandazwa pia chini ya bahari na kuwezesha mawasiliano ya haraka ya kimataifa. Mnamo mwaka 1870 nchi nyingi za Dunia ziliunganishwa na mtandao wa telegrafu.
Teknolojia iliyopatikana iliweza kuwasilisha maneno hadi 50 pekee kwa dakika kwa sababu matini ilipaswa kutumwa kwa mkono herufi kwa herufi. Gharama za telegramu zilikuwa juu kutegemeana na idadi ya maneno na hii ilisababisha kutokea kwa lugha ya mafupisho.
Kwa upande wa kupokea mtumishi aliandika ujumbe kwenye fomu ya telegramu iliyowekwa katika bahasha na kwa kawaida kupelekwa kwa mpokeaji kwa njia ya tarishi aliyetumia baisikeli, pikipiki au gari. Kulikuwa pia na huduma za kumsomea mpokeaji ujumbe kwa njia ya simu.