Khalid bin Barghash wa Zanzibar

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Khalid bin Barghash wa Zanzibar.

Sayyid Khalid bin Barghash Al-Busaid (1874 – 1927) (kwa maandishi ya Kiarabu خالد بن برغش البوسعيد) alikuwa mtawala wa 6 wa Usultani wa Zanzibar.

Alikuwa sultani kwa siku tatu pekee kuanzia 25 Agosti hadi 27 Agosti 1896 akaondolewa madarakani na Waingereza kwa nguvu ya kijeshi.

Khalid bin Bargash alikuwa mwana wa kwanza wa Sayyid Barghash bin Said Al-Busaid. Baada ya kifo cha mjomba wake, sultani Hamad bin Thuwaini wa Zanzibar, alitangazwa na sehemu ya viongozi kuwa sultani mpya, lakini wengine walimpinga. Kulikuwa na uvumi ya kwamba alisababisha kifo cha mjomba wake kwa kumsumisha. [1]

Mwakilishi wa Uingereza aliwahi kumkubali mgombea mwingine kutoka familia ya kisultani, Hamud bin Mohammed, hakuwa tayari kumwona Khalid kwenye kiti cha mtawala akirejea mkataba kati ya Uingereza na Zanzibar ya mwaka 1890 iliyowapa Waingereza nafasi ya kumkubali sultani mpya.

Khalid alipewa muda wa kuondoka katika jumba la kifalme akakataa, akakusanya zaidi ya askari 2000 tayari kwa utetezi.

Asubuhi ya 27 Agosti 1896 Waingereza walikuwa na manowari 5 tayari kwenye bandari ya Zanzibar zilizolengesha bunduki zake kwa jumba la sultani. Saa 9.02 zilianza kuipiga jumba la sultani na kikosi cha wanajeshi kilishambulia jumba. Saa 9.40 jeshi la Sultani likajisalimisha baada ya kifo cha Wazanzibari 500. Sultani mwenyewe alikimbia kwenye ubalozi wa Ujerumani kisiwani.

Baadaye Wajerumani walimpeleka kwa siri kwenda Dar es Salaam alipopewa hifadhi katika koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani. [1] Hamud bin Mohammed alipanda kiti cha sultani.

Sultani aliyefukzwa aliishi Dar es Salaam hadi mwaka 1916. Mwaka ule Waingereza walitwaa mji wakati wa vita kuu ya kwanza ya dunia wakamkuta aliyewahi kuwa sultani wa siku 3 wakampeleka kifungoni huko visiwa vya Shelisheli na baadaye Morisi.

Baada ya vita aliruhusiwa kurudi Afrika ya Mashariki.

Aliaga dunia mjini Mombasa mwaka 1926[1][2].

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. 1.0 1.1 1.2 Hernon, Ian (2003). Britain's Forgotten Wars. Stroud, Gloucestershire: Sutton Publishing, 396–404. ISBN 9780750931625. 
  2. BBC h2g2 entry on the Anglo-Zanzibar War
Alitanguliwa na
Hamad bin Thuwaini
Sultani wa Zanzibar
1896
Akafuatiwa na
Hamud bin Muhammad