Nenda kwa yaliyomo

Tafsiri ya Vishazi na Virai vya Kiingereza kwa Kiswahili

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Vishazi ni vifungu vya maneno vyenye kitenzi na virai ni maneno yasiyo vitenzi au vifungu vya maneno visivyo na kitenzi. Makala hii inafanya kazi ya kupatanisha vile vya Kiingereza na vya Kiswahili ili kuonesha uhusiano kati ya lugha na lugha. Sehemu ya kwanza ya maelezo inatoa ufafanuzi wa maana. Sehemu ya pili ya maelezo inaelekeza jinsi ya kusema (kisawe) kwa ufupi.

Ambiguity ni hali ya neno au kifungu cha maneno kuwa huru kutafsirika/kuwa na fasili zaidi ya moja[1] [2] (kukataza au kulazimisha kutokuwepo kwa hali hii ni kudumaza na kuondoa ladha ya lugha. Mfano: maana za neno kimbiza ni 1. taka kukikamata kiumbe kwa kutumia mbio na maarifa, 2. fukuza, sababisha mtu au kiumbe kihame kutoka kwenye eneo fulani pasipo dhamira hiyo, 3. (kinahau) wahisha hospitali mtu aliyejeruhiwa au mgonjwa sana kwa ajili ya matibabu). Kisawe chake kwa Kiswahili ni utata[3].

Bad luck ni kishazi chenye maana ya kinahau. Huelezea kutokea kwa jambo lenye athari mbaya bila kutarajiwa au kudhamiriwa. Kisawe chake ni bahati mbaya.

Be consistent ni kishazi chenye maana ya kuwa thabiti; usie/asie/kisicho - badilikabadilika (kimsimamo, kifikra, kilivyo, n.k.). Visawe vyake ni kuwa na msimamo, baki vilevile, usiwe kigeugeu.

Challenge ni hali ya kujitokeza kwa jambo jipya na gumu ambalo linahitaji juhudi na maarifa kulitatua. Pia: wito kwa mtu, timu, n.k. ili kujitokeza kwenye pambano la kuamua mshindi. Mfano wa kulingana na maana ya kwanza ni kama, Changamoto Zinazokikabili Kiswahili. Kisawe chake kwa Kiswahili ni changamoto.

Critical thinking ni kufikiri kwa kina kunakoambatana na tafakuri, kujiuliza maswali na kuyatafutia majibu. Pia huhusisha ukosoaji ama kuunga mkono dhana mbalimbali baada ya kujiridhisha. Kisawe chake kwa Kiswahili ni fikra tunduizi.

Declare interest ni kishazi cha Kiingereza chenye maana ya kuweka wazi, kubainisha au kuwaambia wakusikilizao/uwaandikiao kuhusu maslahi yako binafsi juu ya jambo au kitu au mada unayozungumzia. Katika kusema kwa ufupi, tamka: nabainisha maslahi binafsi au naweka wazi maslahi binafsi au nawajulisha kuwa nina maslahi binafsi katika hili na kadhalika.

Delivery report ni hati, ujumbe au arafa inayoonesha kuwa kitu kilichotumwa/safirishwa kutoka sehemu moja hadi nyingine kimefikishwa. Anayepewa ripoti ni mtumaji. Kisawe chake kwa Kiswahili ni hati/arafa ya uwasilishaji [ufikishaji].

Download a file ni mchakato wa kuchukua nakala ya faili (maandishi, taswira, video, n.k.) kutoka sehemu fulani mtandaoni, kuiingiza na kuihifadhi kwenye kifaa chako (simu, kishikwambi, tarakilishi (kompyuta), n.k.). Kishazi kisawe: pakua faili.

Explain in detail: ni kishazi chenye maana ya kuelezea kwa kuangalia au kugusia kila kipengele cha mtu au kitu (mf. mwonekano, tabia, utendaji kazi, taratibu za kukiendesha, n.k.). Kisawe chake kwa Kiswahili ni elezea kinagaubaga - kwa kina.

Good governance ni kirai kinachotaja utawala upasao wa serikali. Hujumuisha utawala wa sheria, kuwa na mipango sahihi ya kuleta maendeleo, kuimarisha demokrasia, kupinga ufisadi, kusikiliza watu, ushirikishi, ukweli na uwazi, n.k. Kisawe chake cha Kiswahili ni utawala bora.

Insurance ni kirai cha nomino. Ni utaratibu unaomwezesha mtu kupata fidia baada ya kufikwa na janga lililoainishwa kwenye mkataba wa bima hiyo. Kwa kuwa ni nomino, neno hili haliwekewi kiambishi awali kama vile ku- (isipokuwa pale ambapo wafanyao hivyo wanaelewana kimuktadha ingawa si sanifu). Kisawe chake kwa Kiswahili ni bima.

It is unlucky/unfortunate ni kishazi kinachoelezea kutokea kwa jambo isivyotarajiwa au si la kupendeza au baya na la kushitukiza. Kisawe cha Kiswahili ni si bahati, haikuwa bahati.

Marriage and wedding ceremony: kwa kawaida, baada ya kufunga ndoa hufuata sherehe ya harusi. Harusi ni shamrashamra zinazofuatia kufungwa kwa pingu za maisha. Kisawe chake ni ndoa na sherehe ya harusi.

One-eigth ni kirai cha kivumishi. Hutaja kiasi au sehemu inayopatikana wakati 1 (moja) inapogawanywa kwa 8 (nane). Ingawa moja ya nane ndio kisawe cha Kiswahili kilichozoeleka sana, kisawe kingine ni thumni.

Sweet melodies: ni dhana inayohusiana na muziki. Inataja uzuri wa ladha ya muziki kulingana na hisia na vionjo vya moyoni vya msikilizaji. Kisawe chake kwa Kiswahili ni mkong'osio murua/mtamu.

Tablet ni kirai nomino. Ni neno linalotaja kifaa cha kielekroniki chenye ukubwa zaidi ya simujanja lakini ni kidogo kuliko kompyuta mpakato (tarakilishi mpakato) ya ukubwa wa kawaida. Mfumo wa uendeshaji wa kifaa hicho ni sawa na ule wa simujanja. Kisawe chake cha Kiswahili ni kishikwambi.

Unleash the dragon kwa maana ya neno kwa neno ni kumfungulia au kumwachia huru mnyama wa kidhahania aitwaye dragoni. Maana ya undani ni kujitokeza na kuweka wazi hisia zilizojificha, kutema nyongo, kufanya jambo pevu baada ya kufikia maamuzi kuwa litafanyika, kudhihirisha kipaji, uwezo, n.k. Kisawe cha Kiswahili ni: Vunja ukimya.

Upload a file ni mchakato wa kuingiza faili la kielekroniki (maandishi, taswira, video, n.k.) kwenye sehemu iliyodhamiriwa mtandaoni. Kishazi kisawe chake cha Kiswahili ni pakia faili.

Way back ni ufupisho wa a long way back in time na hutumika kuelezea hali ya kupita kwa siku nyingi au miaka mingi. Kisawe chake cha Kiswahili ni muda mrefu uliopita/zamani sana.[4]

  1. https://dictionary.cambridge.org/dictionary/english/ambiguity
  2. https://www.mwananchi.co.tz/mw/habari/makala/maarifa/utata-wa-tungo-na-namna-ya-kuuepuka-2774450
  3. https://www.wordhippo.com/what-is/the-meaning-of/swahili-word-6b104b68c0b198efe65616010ee8f20bf11e8270.html
  4. "How do I use the phrase "way back" properly?". English Language Learners Stack Exchange (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2024-06-15.
Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Tafsiri ya Vishazi na Virai vya Kiingereza kwa Kiswahili kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.