Mtaguso wa kwanza wa Nisea
Sehemu ya mfululizo kuhusu |
Mitaguso mikuu ya Kanisa Katoliki |
---|
Mtangulizi (50 hivi) |
Roma ya Kale (325–451) |
Mwanzoni mwa Karne za Kati (553–870) |
Mwishoni mwa Karne za Kati (1122–1517) |
Nyakati za uvumbuzi mwingi (1545–) |
Mtaguso wa kwanza wa Nisea (pia: Nikea[1]) ndio mtaguso wa kwanza kuitwa (tangu mwaka 338) mtaguso wa kiekumeni, yaani mtaguso wa dunia yote au mtaguso mkuu. Ndiyo sababu inashika nafasi ya pekee kati ya mitaguso yote.
Uliitishwa na kusimamiwa na kaisari Konstantino Mkuu, aliyehofia mabishano kati ya raia wake Wakristo kuhusu Yesu Kristo, ambayo yalihatarisha umoja na usalama wa Dola la Roma lililoanza kuelekea kusambaratika. Yeye aliwaalika maaskofu wote wa dola, waliokuwa kama 1000 mashariki na kama 800 magharibi. Washiriki walitokea hata nje ya dola hilo, kama vile Persia na Armenia.
Katika hali hiyo mtaguso ulianza katika mji wa Nikea (leo:Iznik, Uturuki) tarehe 20 Mei 325; washiriki walikuwa kama 318, wengi wao wakitokea upande wa mashariki wa dola hilo. Upande wa magharibi uliwakilishwa na watu 4 kutoka Ulaya na 1 kutoka Afrika. Papa Silvesta I (314-335) aliwakilishwa na mapadri wawili.
Asili ya mabishano ilitokea katika Kanisa la Aleksandria (Misri), ambapo kasisi Arios alikuwa amekanusha umungu wa Yesu, na hivyo alihukumiwa na Sinodi ya Aleksandria ya mwaka 321, iliyoitishwa na askofu Aleksanda wa Aleksandria. Hata hivyo Arios hakuacha mafundisho yake, akakimbilia Palestina kwa rafiki yake Eusebio wa Nikomedia.
Basi, mtaguso ulikiri karibu kwa kauli moja kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu kwa maana ana ousìa (yaani dhati) ileile ya Kimungu aliyonayo Baba. Ndiyo kiini cha Kanuni ya imani ya Nisea iliyopitishwa na mtaguso.
Uamuzi mwingine wa mtaguso ulikuwa kupanga siku ya Pasaka, sherehe kuu ya Kanisa, iwe Jumapili inayofuata mbalamwezi ya kwanza ya majira ya kuchipua, tofauti na kalenda ya Kiyahudi. Pia zilitungwa kanuni 20 kuratibu mambo mbalimbali.
Mtaguso ulipomalizika tarehe 25 Julai 325, Konstantino alifikiri uamuzi juu ya dogma utamaliza mabishano, lakini haikuwa hivyo, kwa sababu Wagiriki wengi, ingawa hawakukubaliana na Arios, hawakuridhika na msamiati uliotumika kuelezea uhusiano wa Baba na Mwana.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Kwa Kiswahili, Wakatoliki wamezoea umbo la "Nisea", Walutheri umbo la "Nikea"
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Hati zote za mtaguso katika lugha mbalimbali
- Atanasi wa Aleksandria, Utetezi wa Tamko la Nisea; • Atanasi wa Aleksandria, Barua ya Sinodi kwa watu wa Afrika
- Eusebio wa Kaisarea, • Eusebio wa Kaisarea, Barua kwa watu wa jimbo lake kuhusu Mtaguso wa kwanza wa Nisea Account of the Council of Nicea; Maisha ya mwenye heri kaisari Konstantino, kitabu III, sura VI-XXI zinahusu Mtaguso wa kwanza wa Nisea
- Eustazio wa Antiokia, Barua iliyorekodiwa katika Historia ya Kanisa iliyoandikwa na Theodoreto 1.7
- Mtaguso wa kwanza wa Nisea katika Catholic Encyclopedia
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Mtaguso wa kwanza wa Nisea kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |