Nenda kwa yaliyomo

Meli

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Merikebu)
Meli kubwa ya shehena ya mafuta ya petroli.
Muundo wa meli ya kisasa.
Jahazi.

Meli ni chombo kikubwa cha kusafiria kwenye maji.

Siku hizi meli huwa na bodi ya chuma ikisogezwa kwa nguvu ya injini inayochoma diseli.

Hadi karne ya 19 meli zilijengwa kwa kutumia mbao zikasongezwa hasa kwa nguvu ya upepo kwa kutumia tanga. Jahazi ziko hadi leo.

Meli hutumiwa hasa kwa kubeba mizigo na abiria. Kuna pia meli za kijeshi zinazoitwa manowari.

Kuna njia mbalimbali za kutofautisha ukubwa wa meli: njia ya kawaida imekuwa tani GT inayotaja mjao wa chombo.

Mkuu na kiongozi kwenye meli anaitwa nahodha. Watu wanaofanya kazi kwenye meli kwa jumla ni mabaharia.

Muundo wa meli

  1. Omo ni sehemu ya mbele ya bodi ya meli
  2. Pua la omo linapunguza ukinzani wa maji wakati wa mwendo na kupunguza matumizi ya mafuta ya injini
  3. Nanga hutiwa hadi chini ya maji na kushika meli ikisimama
  4. Bodi ya meli imetengenezwa kwa mabamba ya feleji
  5. Rafadha (au: jembe) ya meli inasogeza chombo mbele ndani ya maji
  6. Tezi (au: shetri) ni sehemu ya nyuma ya meli
  7. Dohani ni faneli au eksosti kwa hewa chafu ya injini
  8. Vyumba juu ya sitaha ni kama makazi kwa ajili ya mabaharia na abiria, huwa pia na dambra ya kutawala meli
  9. Sitaha ni uso wa juu wa meli; ni dari juu ya bodi ya meli; meli kubwa huwa na sitaha mbalimbali chini ya sitaha ya juu

Historia

Vyombo vya kwanza vya kusafiria majini yalikuwa mashua na maboti madogo kama mtumbwi.

Kuanzia mwaka 4000 KK hivi watu wa Misri ya Kale walianza kutengeneza jahazi ndogo.

Wachina wanajulikana walijenga jahazi kuanzia 2000 KK.

Mnamo 1200 KK watu wa Finisia na Ugiriki ya Kale walijenga jahazi kubwa zaidi yenye urefu wa mita 30. Waroma wa Kale walitengeneza meli iliyobeba watu 1,000.

Katika mazingira ya Mediteranea meli hizi za kwanza zilisogezwa kwa kasia pamoja na tanga. Meli kubwa za Kiroma zilikuwa na kasia kubwa zilizopigwa na watumwa wawili au watatu kwa kila kasia.

Jahazi ziliboreshwa hadi kuvuka bahari kuanzia karne ya 15 BK. Wachina na Wareno ni watu wa kwanza waliovuka bahari za mbali. Ila tu Wachina baada ya kutembelea mara kadhaa pwani za Afrika chini ya Zheng He mnamo mwaka 1400 waliamua kuacha upelelezi huu, lakini Wareno waliendelea kuzunguka Afrika na dunia yote na hatimaye kuanzisha kipindi cha ukoloni cha Ulaya.

Katika karne ya 19 injini ya mvuke ilipatikana hata kwa meli. Meli zikawa kubwa zikaendelea kukua wakati injini ya diseli imepatikana katika karne ya 20.

Aina na idadi ya meli

Bila kuangalia maboti madogo, duniani kuna

  • meli za kibiashara 34,882 zenye ukubwa wa tani GT zaidi ya 1,000; jumla ya meli hizi ni tani bilioni 1.04. (mwaka 2007)
    • meli hizi zilibeba jumla ya shehena (mzigo) tani bilioni 7.4 (mwaka 2006) na kiasi hiki kimekua asilimia 8 kila mwaka.
    • 37.5% za meli hizi zilibeba shehena ya mafuta
    • 35.8% za meli hizi zilibeba shehena zilizofunguka kama vile madini, makaa mawe, nafaka au simiti
    • 10% zilikuwa meli za kontena
    • 10% ni meli zinazochanganya kila aina ya mizigo
  • manowari 1,240 bila kuhesabu maboti madogo ya kijeshi (mwaka 2002)
  • meli za kuvua samaki ni nyingi lakini ziko za kila ukubwa, si rahisi kuzipanga. Kuna vyombo 38,400 zenye tani zaidi ya 100. Nyingi zaidi ni ndogo sana; meli kubwa ya kuvua samaki zafikia tani 3,000 halafu kuna meli za viwanda ambako kundi la meli zinapeleka windo la samaki nao wanakatwa mara moja na kufungwa tayari kwa kuuzwa madukani zikitunzwa katika barafu.