Mashua

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Boti)
Mashua karibu na Lamu
Jahazi karibu na Doha
Boti la polisi huko Venezia, Italia.
Boti la kuokolea uhai huko Ufalme wa Muungano.

Mashua ni jina la jumla la vyombo vya kusafiri kwenye maji. Zinaweza kuendeshwa kwa njia mbalimbali, kama makasia, matanga na injini. Mashua zenye injini huitwa boti kwa kawaida na zilizo kubwa sana huitwa meli. Ikiwa injini inafanya kazi kwa mvuke, mashua inaitwa merikebu.

Mashua hutengenezwa kwa maada mbalimbali, kama mbao, mafunjo, plastiki au feleji. Zinasafiri kwenye bahari, maziwa na mito, na kubeba watu au mizigo au yote. Mashua ambazo hutumiwa kuvuka mito huitwa feri au vivuko. Zile zinazoweza kwenda chini ya maji huitwa manowari.

Huko pwani ya Afrika ya Mashariki, aina mbili za mashua kubwa kiasi za mbao zenye (ma)tanga ni za kawaida[1]. Jahazi ndilo kubwa zaidi na linatumika kwa biashara katika pwani na kuelekea Uarabuni na Uhindi. Mashua hapa ni chombo kidogo zaidi cha mbao ambacho hutumiwa mara nyingi kwa uvuvi. Aina hizi zote mbili zimejengwa kwa miunda ya mbao.

Aina nyingine mbili za mashua zimetengenezwa kwa magogo ya miti yaliyotemuliwa. Sahili zaidi ni mtumbwi, unaotumika karibu na pwani na kwenye komeo za bahari na mito. Unasukumwa kwa kafi au upondo. Kwa ujumla huwa na urefu wa m 2 au 3 lakini unaweza kuwa hadi m 6. Mitumbwi midogo inaitwa hori na hutumika kwa usafiri kati ya ufuko na mashua kubwa zaidi.

Aina nyingine ni ngalawa, ambayo ni kubwa kuliko mtumbwi. Ingawa awali zilitengenezwa kutoka kwa gogo kubwa la mti, sasa mara nyingi hutengenezwa kwa mbao. Kwa kawaida hubeba tanga. Inatofautishwa na mashua kwa gubeti yake iliyoinuliwa na shetri iliyochongoka (mashua ina shetri ya mraba).

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Nakala iliyohifadhiwa. Jalada kutoka ya awali juu ya 2021-12-09. Iliwekwa mnamo 2021-11-30.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:


Makala hii kuhusu mambo ya uchumi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mashua kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.