Leo Tolstoy

Lev Nikolayevich Tolstoy (1828–1910) alikuwa mwandishi wa Kirusi na mmoja wa waandishi mashuhuri zaidi katika fasihi ya dunia. Anajulikana zaidi kwa riwaya zake kubwa War and Peace (1869) na Anna Karenina (1877), ambazo zinachukuliwa kuwa kazi bora za fasihi kutokana na undani wake, uendelezaji wa wahusika na uchunguzi wa mada tata kama maadili, imani, upendo, na asili ya historia. Uandishi wa Tolstoy ulionyesha imani zake za kifalsafa na kiroho zilizobadilika kadri ya maisha, na ambazo baadaye zilikuwa za ukosoaji mkubwa kwa dini zilizoandaliwa, vurugu, na mali ya kidunia. Kazi zake mara nyingi huunganisha uhalisia na tafakuri ya kifalsafa, na ushawishi wake unavuka mipaka ya fasihi hadi katika maadili na fikra za kisiasa.
Katika miaka yake ya baadaye, Tolstoy alipitia mabadiliko ya kiroho, akikumbatia anarchism ya Kikristo na kutetea amani, maisha ya kujinyima, na upinzani usio wa vurugu. Imani hizi ziliwahi kuhamasisha viongozi kama Mahatma Gandhi na Martin Luther King, Jr. Alikana hadhi na mali zake za kifahari, na badala yake akachagua kuishi maisha ya unyenyekevu na maadili madhubuti. Licha ya umaarufu wake duniani na mafanikio yake ya kifasihi, Tolstoy alikumbwa na migogoro ya ndani na matarajio ya jamii ya wakati wake. Urithi wake unaendelea kuishi kupitia riwaya na insha zake, pamoja na harakati ya Kitolstoy ambayo ililenga kuishi kwa kufuata mafundisho yake ya kimaadili.
Familia na urithi
[hariri | hariri chanzo]Tolstoy alizaliwa katika familia ya makabaila kwenye kijiji cha Yasnaya Polyana karibu na mji wa Tula. Familia yake ilikuwa na undugu na makabaila wengi na Aleksander Pushkin alikuwa binamu yake.
Mapema Tolstoy alibaki yatima kutokana na kifo cha wazazi wake, akalelewa na dada yake mkubwa.
Alianza kusoma lugha za Kiasia halafu sheria, lakini alipofikia umri wa miaka 20 aliacha masomo akaenda kuishi kwenye mashamba ya familia yake. Hapo alijikuta kama bwana wa familia za wakulima maskini aliokuwa amewarithi kama sehemu ya mali yake, wakiwa kama nusu watumwa jinsi ilivyokuwa kawaida kwa wakulima wengi wa Urusi wa siku zile, kumbe akajitahidi kuboresha maisha yao.
Mwanajeshi, mpenda amani, mla mboga
[hariri | hariri chanzo]Kama mwanajeshi alishiriki katika vita vya Urusi kwenye Kaukazi na vita vya Krimea.
Alirudi kwake kama adui wa vita akaendelea kulaumu vita na mabavu kati ya watu akijenga imani yake kwenye mfano wa Yesu Kristo.
Imani hiyo ilileta baadaye ugomvi na Kanisa rasmi la Urusi (Waorthodoksi) lililotumia imani ya Ukristo kwa kubariki jeshi la taifa, wakati Tolstoy alikataa kushiriki vita tena.
Aliendelea kukataa kila aina ya kuua, kwa hiyo alikataa kuchinja wanyama na kula nyama. Aliandika:
- Kula nyama ni mabaki ya unyama ndani ya binadamu. Ulaji mboga ni hatua ya kwanza kwenye njia ya mwangaza.
- Ni hatua moja tu kutoka uuaji wa wanyama kwenda uuaji wa binadamu, vilevile kutoka kutesa wanyama kwenda kutesa watu.
- Kama huwezi kuua watu - vizuri! Kama huwezi kuua mifugo au ndege - bora; wala samaki wala wadudu - bora tena! Ujitahidi kusogea mbele, usipoteze muda kutafakari ni nini inayowezekana au haiwezekani. Fanya unachoweza.
Ndoa na kazi ya fasihi
[hariri | hariri chanzo]Mwaka 1862 alimwoa Sofia Andreevna Bers akazaa naye watoto 13.
Kutokana na vitabu vyake juu ya vita vya Krimea alikuwa maarufu nchini Urusi na riwaya kubwa zilizofuata zilijenga sifa zake za kimataifa.
Pamoja na riwaya aliandika pia juu ya dini. Kitabu "Ufalme wa Mungu umo ndani yenu" kiliathiri watu wengi, wakiwa pamoja na Mahatma Gandhi na Martin Luther King.
Mwaka 1910 alikufa kutokana na kifua kikuu akiwa na umri wa miaka 82.
![]() |
Makala hii kuhusu mtu huyo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Leo Tolstoy kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |