Nenda kwa yaliyomo

Kunta Kinte

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Riwaya ya Roots inasimulia habari za Kunta Kinte

Kunta Kinte ni jina la mhusika katika riwaya ya Roots: Saga of American Family iliyotolewa mwaka 1976 na Alex Haley aliye mwandishi wa Marekani. Kuanzia mwaka 1977 masimulizi ya kitabu yalikuwa msingi wa mfululizo wa filamu za runinga.

Mhusika wa kitabu na filamu

[hariri | hariri chanzo]

Haley alimwaza mhusika Kunta Kinte kutokana na mmoja wa mababu zake: mwenyeji wa Gambia aliyezaliwa mnamo 1750, alikamatwa na kuuzwa kama mtumwa na kupelekwa Marekani alipofariki mnamo 1822. Kufuatana na Haley simulizi lake ya maisha ya Kunta ni mchanganyiko wa ukweli na habari za kubuniwa. [1]

Hadithi ya maisha ya Kunta Kinte ilionyeshwa katika mifululizo miwili ya filamu za runinga: Roots ya 1977 [2] na Roots ya 2016. Katika mfululizo wa kwanza, mhusika alionyeshwa kama kijana na mwigizaji LeVar Burton na kama mtu mzima na John Amos. Katika marudio ya 2016, mwigizaji alikuwa Malachi Kirby. [3]

Wasifu katika riwaya ya Roots

[hariri | hariri chanzo]

Kulingana na kitabu Roots, Kunta Kinte alizaliwa mnamo 1750 huko Jufureh, kijiji cha Wamandinka nchini Gambia. Alilelewa katika familia ya Waislamu. [4] [5] Mnamo 1767, wakati Kunta alikuwa akiokota kuni, wanaume wanne walimkamata na kumchukua mateka. Kunta aliamka na kujikuta amefunikwa macho, na kufungwa mdomo na mikono. Yeye na wengine waliwekwa kwenye jahazi la biashara ya watumwa Lord Ligonier kwa safari ya miezi minne kwenda Amerika Kaskazini.

Huko Marekani Kunta aliuzwa kwa John Waller (Reynolds katika filamu ya 1977), mmiliki wa shamba katika jimbo la Virginia aliyemwita jina la Toby. Alikataa jina alilopewa na wamiliki wake akakataa kuzungumza na wengine. Alijaribu kutoroka mara nne, lakini alikamatwa tena kila mara. Baada ya kunaswa mara ya nne washikaji wake walimpa chaguo: atahasiwa au kukatwa unyayo. Akachagua kukatwa mguu wakakata nusu ya mbele ya kanyagio lake la kulia. Kadiri miaka ilivyopita, Kunta, aliyemilikiwa sasa na kaka wa John, Dk. William Waller, alinyamaza kuhusu hatima yake akaanza kuwasiliana wazi zaidi na watumwa wenzake, bila kusahau asili yake.

Kunta alimwoa mwanamke mtumwa aliyeitwa Belle Waller na walikuwa na binti aliyeitwa Kizzy (Keisa kwa Kimandinka), ambayo kwa lugha mama ya Kunta inamaanisha "kaa ulipo", kwa maana ya kwamba asichukuliwe na kuuzwa penginepo. Wakati Kizzy alikuwa na umri wa kukaribia miaka 20, aliuzwa kwenda North Carolina wakati William Waller alipogundua kwamba alikuwa ameandika pasi bandia ya kusafiria kwa kijana mtumwa, Noah, ambaye alikuwa akimpenda. Alikuwa amefundishwa kusoma na kuandika kwa siri na Missy Anne, mpwa wa mmiliki wa shamba. Mmiliki mpya wa Kizzy alikuwa Thomas Lea (Moore katika filamu ya 1977), aliyembaka mara moja akamzaa mtoto wa kiume na kumwita George. George ambaye ni babu wa Alex Haley, aliendelea kuitwa "Chicken George", kwa sababu majukumu yake aliyopewa yalikuwa kuchunga kuku za bwana wake.

Katika riwaya, Kizzy haendelei kusikia tena habari za wazazi wake akibaki maisha yake yote kama mfanyakazi wa shamba huko North Carolina.

Katika filamu ya 1977, Kizzy anaongozana na mabwana hadi kutembelea tena shamba la Reynolds. Hapo anagundua kuwa mama yake aliuzwa kwa shamba lingine na kwamba baba yake alikufa kwa huzuni kubwa miaka miwili baadaye, mnamo 1822. Anakuta kaburi lake, ambako anakata mstari kwenye jina Toby na badala yake anaandika jina lake halisi Kunta Kinte. Kizzy anaendelea kuona uhuru baada ya mwisho wa utumwa nchini Marekani manmo 1865.

Sehemu ya mwisho ya kitabu hicho inaelezea vizazi kati ya Kizzy na Alex Haley, ikielezea mateso yao, changamoto na hatimaye jinsi walivyojenga maisha yao huko Marekani.

Alex Haley alijidai kuwa kizazi cha saba baada ya Kunta Kinte. [6]

Usahihi wa kihistoria

[hariri | hariri chanzo]

Haley alidai kuwa vyanzo yake kuhusu asili ya Kinte vilikuwa masimulizi katika familia yake pamoja na mtu aliyekutana naye alipotembelea Gambia.[7]

Baada ya kitabu na filamu kufaulu na kupata umaarufu, wachambuzi mbalimbali walichungulia ukweli wa madai ya Haley wakakuta kasoro mbalimbali. Inaonekana kwamba Haley, alipotembelea Gambia, alikuwa akiwaambia watu wengi juu ya Kunta Kinte kwamba alipata kusikia maneno yake mwenyewe yakirudiwa kwake. [8]

Vilevile mwandishi na mwanahistoria Harold Courlander alibaini kuwa sehemu za kitabu zinazoelezea maisha ya Kinte zilichukuliwa kutoka riwaya ya mwenyewe Courlander, The African. Haley mwanzoni alikataa mashtaka hayo, lakini hatimaye alikubali kuwa kitabu cha Courlander kilikuwa chanzo akakubali kumlipa $ 650,000[9].

Hata hivyo, wachambuzi wengine wa historia waliona uwezekano mkubwa kwamba Kunta Kinte alikuwa mtu halisi. [10]

  1. The Roots of Alex Haley". BBC Television Documentary. 1997..
  2. Bird, J.B. "ROOTS". Museum.tv. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2013-04-10. Iliwekwa mnamo Novemba 21, 2007.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  3. Campbell, Sabrina (Mei 30, 2016). "Malachi Kirby is Kunta Kinte in 'Roots' Remake". NBC News. Iliwekwa mnamo Januari 3, 2017.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  4. Thomas, Griselda (2014). "The Influence of Malcolm X and Islam on Black Identity". Muslims and American Popular Culture. ABC-CLIO. ku. 48–49. ISBN 9780313379635.
  5. Hasan, Asma Gull (2002). "Islam and Slavery in Early American History: The Roots Story". American Muslims: The New Generation Second Edition. A&C Black. uk. 14. ISBN 9780826414168.
  6. "The Kunta Kinte – Alex Haley Foundation". Kintehaley.org. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo Septemba 27, 2007. Iliwekwa mnamo Novemba 11, 2007.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  7. Alex Haley, "Black history, oral history, and genealogy", pp. 9–19, at p. 18.
  8. Wright, Donald R. (1981). "Uprooting Kunta Kinte: On the Perils of Relying on Encyclopedic Informants". History in Africa. 8: 205–217. doi:10.2307/3171516. JSTOR 3171516.
  9. https://www.chicagotribune.com/news/ct-xpm-1993-03-10-9303190620-story.html
  10. Kunta Kinte’s World

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]