Kiini cha atomi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Muundo wa atomi kwa mfano wa lithi: Mzingo wa Elektroni na Kiini cha atomi atika kitovu chake. Kiini inafanywa na nyutroni (bila chaji) na protoni (chaji chanya).

Kiini cha atomi [1] ni sehemu ya ndani ya atomi inayozungukwa na mzingo elektroni.

Kiini kinajengwa kwa protoni na nyutroni[2] na hizi kwa pamoja huitwa "nyukleoni" [3].

Kiini chenyewe kina karibu masi yote ya atomi ndani yake (mnamo 99.9%, elektroni kwenye mzingo huwa na masi ndogo mno).

Idadi ya protoni katika kiini inafanya namba atomia. Namba ya nyukleoni (protoni na nyutroni kwa pamoja) hufanya namba ya masi. Masi ya atomi thabiti zinazotokea kiasili ziko kati ya 1 (hidrojeni) na 238 (urani). Atomi zenye masi kubwa zaidi hazitokei duniani kiasili maana si thabiti

Ukubwa wa kiini cha atomi ni takriban femtomita 1.6 (10-15 m) (hidrojeni) hadi femtomita 15 (urani).

Ilhali karibu masi yote iko ndani ya kiini nafasi yake ni ndogo na sehemu kubwa ya nafasi ya atomi huchukuliwa na mzingo elektroni.

Kwa hali ya kawaida atomi haionyeshi chaji ya umeme. Ina chaji ndani yake kulingana na idadi ya protoni ambazo ni chanya na elektroni ambazo ni hasi. Katika hali ya kawaida idadi yao ni sawa kwa hiyo chaji zinajibatilishana. Lakini kama elektroni zinaondoka katika mzingo elektroniki hali inabadilika na atomi huonyesha chaji. Kiini cha atomi pekee yake daima ina chaji chanya maana haina elektroni zilizopo kwenye mzingo.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. ing. atomic nucleus
  2. isipokuwa katika atomi ya hidrojeni ambayo ni atomi ndogo kabisa, ina protoni 1 pekee katika kiini
  3. kutoka lat. nucleus = kiini, yaani chembe za kiini