Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Maandamano wa JWTZ wakati wa sikukuu ya Mapinduzi ya Zanzibar, 2000
Askari wa King's African Rifles mnamo 1944

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) (ing. Tanzania People's Defense Force TPDF) ni jeshi lililoanzishwa mnamo mwezi wa Septemba katika mwaka wa 1964. Ilichukua nafasi ya jeshi la Tanganyika Rifles lililorithiwa na ukoloni wa Kiingereza.

Historia ya awali[1][hariri | hariri chanzo]

Chanzo cha jeshi nchini Tanzania kilikuwa jeshi la kikoloni la Uingereza katika Afrika ya Mashariki. Mwaka 1919 Uingereza ilikabidhiwa utawala juu ya Tanganyika na Shirikisho la Mataifa. Waingereza walipanusha mfumo wa King's African Rifles waliowahi kuanzishwa Kenya hadi Tanganyika. Jeshi la Kings African Rifles ilikuwa na vikosi (battalions) 6 ambazo viwili vilikuwepo Kenya, vitatu Tanganyika na kimoja huko Uganda. Katika kikosi cha sita cha King's African Rifles kilichoanzishwa mwaka 1917 kwa kuajiri askari kutoka Tanganyika walikuwepo pia askari wa awali wa jeshi la Kijerumani la Schutztruppe waliowahi kukamatwa kama wafungwa na kukubali kuendelea upande wa Waingereza.

Baada ya uhuru mwaka 1961 vikosi vya Kings African Rifles katika Tanganyika vilibadilishwa jina na kuwa Tangayika Rifles (TR). Pamoja na kubadilika jina Tanganyika Rifles ilikuwa na muundo sawa na Kings African Rifles (KAR). Maafisa wenye mamlaka bado walikuwa Waingereza, pamoja na Waafrika watano waliopandishwa cheo wakati wa uhuru na kupokea mafunzo katika vyuo vya kijeshi vya Kiingereza. Jeshi jipya lilipangwa katika vikosi viwili vyenye makao makuu huko Dar es Salaam na Tabora. Afisa mkuu alikuwa Brigedia Jenerali Patrick Sholto Douglas.

Mgomo na uasi wa Tanganyika Rifles[hariri | hariri chanzo]

Kwa jumla kulikuwa na hali ya kutoridhika kati ya askari wa TR. Sababu yake ilikuwa matumaini ya kwamba uhuru ungeleta mabadiliko makubwa zaidi na nafasi za kupanda cheo baada ya kuondoka kwa maafisa wazungu. Lakini maafisa Waingereza waliendelea kuajiriwa na serikali ya Nyerere na tofauti kubwa katika mapato na hali ya makazi ya Wazungu na Waafrika ziliendelea. Hata kinyume askari waliowahi kuwa na mshahara wa juu kulingana na watumishi Waafrika wengine ya serikali waliona ya kwamba mapato yao hayakupanda ilhali mishahara kwa jumla iliongezeka zaidi. Zaidi ya hapo, serikali ya TANU ilituma vijana kutoka Umoja wa Vijana wa TANU kwa mafunzo ya kijeshi huko Israeli na baada ya kurudi walipewa ajira jeshini na wengine wao kupandishwa vyeo kupitia askari waliowahi kuhudumia miaka mingi.

Katika Januari 1964 matokeo mawili yalijadiliwa sana kati ya askari moja ilikuwa tangazo la Nyerere alikotamka mwisho wa siasa ya "Africanization" katika utumishi wa serikali[2]. Tangazo hili lilisababisha viongozi wa umoja wa wafanyakazi kulalamika. Tukio lingine likawa habari za mapinduzi ya Zanzibar yaliyoanza tar. 12 Januari 1964.

Tarehe 20 Januari 1964, bado wakati wa usiku, kikosi cha kwanza cha TR kwenye kambi la Colito Barracks mjini Dar es Salaam kiliasi na kujipatia silaha kutoka ghala. Maafisa Waingereza walikamatwa na kufungwa lakini mkuu Douglas aliweza kujificha. Waasi walivamia kituo cha redio, uwanja wa ndege, ikulu na ofisi ya posta na simu. Maafisa Waingereza na Waafrika wasioshiriki na waasi walisafirishwa Kenya. Rais Nyerere alienda mafichoni katika kanisa moja la kikatoliki ng'ambo ya bandari akamwachia waziri Oskar Kambona[3] kazi ya kuwasiliana na wanajeshi. Madai ya wanajeshi yalikuwa kuachishwa kwa maafisa Waingereza na kupandishwa kwa mishahara. Siku za kwanza ya mgomo wa jeshi ilifuatwa na vipindi vya fujo mjini vilivyobadilika na vipindi vya kimya, mashambulizi dhidi ya maduka ya Wahindi na kukamatwa kwa Wazungu wachache. Hata mbalozi wa Uingereza alikamatwa kwa kipindi kifupi.

Waziri Kambona alianza kujadiliana na wanajeshi na kuwaahidi ongezeko la mapato na kutoa vyeo vya juu kwa Waafrika kadhaa. Nyerere alirekodi hotuba iliyotangazwa redioni alipokosoa wanajeshi na kudai utulivu. Askari walirudi kwenye kambi lakini kurudi mjini siku iliyofuata. Pia huko Nairobi na Kampala ulitokea uasi wa wanajeshi -wote askari wa KAR wa awali. Maraisi Milton Obote na Jomo Kenyatta hawakusita kuomba vikosi wa jeshi la Uingereza vilivyokuwa bado na vituo kwa kuzimisha ghasia. Hatimaye Nyerere alianza mawasiliano na Uingereza iliyotuma manowari na wanajeshi kutoka Aden kuelekea Daressalaam.[4] Polisi ya siri ya Tanzania ilianza kupata habari ya kwamba pia kati ya askari ya Field Force unit majadiliano yalikuwa yameanza kuunga mkono na juhudi za wanajeshi, pia harakati kati ya wafanyakazi bandarini na hofu ilikuwa ya kwamba sehemu ya viongozi wa umoja wa wafanyakazi walikuwa na mipango ya kujiunga nao.

Tarehe 24 Januari serikali ya Tanzania iliomba rasmi Uingereza kuingia kati na kuzimisha uasi. Asubuhi ya 25 Januari kikosi kidogo cha wanajeshi wa Kiingereza waliondoka kwenye meli iliyokwepo karibu na Dar es Salaam kwa njia ya helikopta. Walivamia kambi la Colito barracks na jenerali Douglas alidai kwa kipazia sauti wanajeshi wajisalimishe. Mwanzoni walikataa lakini baada ya mashambulio mafupi walio wengi walijisalimisha wengine wakakimbia. Viongozi walikamatwa, na pia askari wa Dodoma na Nachingwewa waliowahi kujiunga na uasi walijisalimisha bila upinzani kwa askari Waingereza wachache.

Wakazi wengine wa Daressalaam walikuwa na hofu ya kwamba Uingereza ulikuwa umerudi ili kurudisha ukoloni lakini baada ya kusita masaa machache Nyerere alieleza kwa njia ya redio ya kwamba kuingilia kwa Uingereza ulifuata ombi la serikali yake.

Watu wengi walikamatwa baada ya matukio haya na kufanyiwa utafiti kama walikuwa na uhusiano na uasi.[5]

Askari Waingereza waliondoka kwenye Aprili 1964 na nafasi yao ilichukuliwa na kikosi kutoka Nigeria iliyofika kwa niaba ya Umoja wa Afrika kufuatana na ombi la serikali ya Tanganyika. [6]

Kuanzisha jeshi jipya[hariri | hariri chanzo]

Baada ya uasi, jeshi la TR lilivunjwa. Askari wote waliachishwa. Sehemu ya askari wa Dodoma waliajiriwa tena katika jeshi jipya lakini hao wa Dar es Salaam hawakurudishwa. Maafisa Waafrika ambao kwa jumla walisimama upande wa serikali na kutoshiriki katika uasi waliajiriwa tena.

Jeshi jipya lilijengwa kwa kuajiri hasa wanachama wa umoja wa vijana wa TANU. Jeshi hili jipya liliwekwa chini ya usimamizi ya chama cha TANU (baadaye CCM) kwa kufuata mtindo wa nchi kama Urusi na China. Kamanda wa kwanza alikuwa Mrisho Sarakikya aliyewahi kusimama upande wa serikali wakati wa uasi akapandishwa cheo kutoka luteni hadi kanali, baadaye kuwa jenerali.

Mwanzoni JWTZ ilikuwa jeshi ndogo lenye askari chache kuliko TR lakini hadi 1967 lilipanushwa kuwa na vikosi 4.

Askari wa JWTZ wakivaa kofia za UM

Mpangilio wa JWTZ wa kisasa[hariri | hariri chanzo]

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limegagiwa kwa matawi matatu:

 • Kamandi ya Nchi Kavu
 • Kamandi ya Jeshi la Majini
 • Kamandi ya Jeshi la Anga.

Nchi Kavu[hariri | hariri chanzo]

Mnamo mwaka 2012 Jeshi la Nchi Kavu la JWTZ lina vikosi vifuatavyo:

 • 5 × brigedi za askari wa miguu
 • 1 × brigedi ya vifaru
 • 3 × batalioni ya mizinga
 • 2 × batalioni za mizinga ya ulinzi wa hewani
 • 1 × batalioni ya mizinga ya mortar
 • 2 × batalioni za kupambana na vifaru
 • 1x rejimenti ya uhandisi
 • 1 × kundi la logistic na akiba

Vyeo katika JWTZ[hariri | hariri chanzo]

Amiri jeshi mkuu wa JWTZ ni rais wa Tanzania.

Maafisa[hariri | hariri chanzo]

Cheo Alama kwenye sare
Jenerali
Luteni Jenerali
Meja Jenerali
Brigedia Jenerali
Kanali
Luteni Kanali
Meja
Kapteni
Luteni
Luteni Usu

Vyeo vya chini[hariri | hariri chanzo]

Cheo Alama kwenye sare
Afisa Mteule Daraja la Kwanza
Afisa Mteule Daraja la Pili
Sajinitaji
Sajenti
Koplo
Koplo Usu

Wajibu wa JWTZ[hariri | hariri chanzo]

Wajibu wa JWTZ ni rasmi[7]:

 • Kulinda Katiba na Uhuru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 • Ulinzi wa mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 • Kufanya mafunzo na mazoezi ili kujiweka tayari kivita wakati wote.
 • Kufundisha umma shughuli za ulinzi wa Taifa.
 • Kushirikiana na mamlaka za kiraia katika kutoa misaada ya kibinadamu na uokoaji wakati wa
 • Kutoa huduma mbalimbali za kijamii.
 • Kukuza elimu ya kujitegemea na uzalishaji mali kupitia Jeshi la Kujenga Taifa.
 • Kushiriki ulinzi wa amani kimataifa.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

 1. Linganisha "Historia ya JWTZ" kwenye tovuti rasmi (yenye makosa madogo, kama kuchanganya Vita Kuu ya kwanza na ya pili)
 2. Nyerere alitangaza ya kwamba wananchi wote wangetumiwa kulingana na elimu na uwezo wao kama ni Waafrika wazalendo au Wazungu au Wahindi waliochagua uraia wa Tanganyika, bila kujali rangi ya ngozi. Linganisha Race, Nation, and Citizenship in Post-Colonial Africa: The Case of Tanzania, by Ronald Aminzade, uk. 86 (google books, tazamiwa Juni 2015
 3. Kambona alishika ofisi mbili za mambo ya nje na ulinzi wa taifa
 4. Tanganyika Mutini stirs British action; Pittsburgh Post-Gazette - 21. Jan. 1964
 5. [ https://books.google.com/books?id=b-wWAwAAQBAJ&pg=PA68&lpg=PA68&dq=tanganyika+mutiny&source=bl&ots=Z1izRjQYtE&sig=TdFOGyNb_gPUg4nfNQgBDxmEFqg&hl=de&sa=X&ei=f62BVYuNCcWesgG_obqYBg&ved=0CBwQ6AEwADgU#v=onepage&q=tanganyika%20mutiny&f=false The Military Intervenes: Case Studies in Political Development ed. Henry Bienen, uk. 68, footnote 43 (google book search, ilitazamiwa Juni 2015)]
 6. Life in Tanganyika in the Fifties , by Godfrey Mwakikagile; uk. 83 (google books, ilitazamiwa Juni 2015)
 7. Tovuti la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]

Vyanzo kuhusu uasi wa 1964[hariri | hariri chanzo]Flag-map of Tanzania.svg Makala hii kuhusu maeneo ya Tanzania bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.