Kifaru (jeshi)
Kwa mnyama tazama hapa: Kifaru
Kifaru (pia: faru) ni mashine ya vita iliyopewa jina lake kutokana na mnyama wa pori. Kimsingi kifaru ni kama gari kubwa lililokingwa kwa mabamba ya feleji likibeba silaha mara nyingi mzinga.
Vifaru vyepesi hutembea kwa matairi lakini vifaru vizito huwa na minyororo. Mashine ndogo na nyepesi yenye kasi kubwa hupewa jukumu la kupeleleza uwanja wa vita na hasa kubeba askari wakielekea penye hatari.
Mashine kubwa na nzito yenye bunduki kubwa mara nyingi hutumiwa dhidi ya vifaru vya adui. Vikiwa na mbio vinaweza kupita hata moto ya mizinga.
Vifaru vingine hupewa kazi kama lori yaani kubeba mizigo ya pekee kwa kazi inayotekelezwa katikati ya mapigano. Mfano wake ni kifaru kinachobeba daraja la kuwekea juu ya mito midogo. Vingine hubeba roketi dhidi ya ndege au kuhudumia kama mashine ya rada.
Historia ya Kifaru
[hariri | hariri chanzo]Vifaru vilitumiwa mara ya kwanza na Ufalme wa Muungano wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia dhidi ya Ujerumani. Machine hizi zilitembea polepole zikawa bado na matatizo mengi lakini zilifaulu kwa sababu pale mwanzoni hapakuwa na silaha maalumu dhidi yao.
Hadi Vita Kuu ya Pili ya Dunia teknolojia iliendelea mbele hasa Ujerumani ilishambulia kwa kutumia vifaru vingi na kushinda majirani yake. Warusi walijenga pia vifaru vingi na vita katika Urusi iliona vifaru maelfu katika mapigano. Hapa udhaifu wa vifaru umeshajulikana na pande zote zilishindana kubuni bunduki maalumu dhidi ya kifaru pamoja na kuboresha kinga chake.
Katika vita hivi ilionekana ya kwamba vifaru havifai kila mahali. Hasa mlimani na penye matope si mahali pake. Katika vita baada ya 1945 vifaru vilikuwa muhimu katika vita kati ya Israeli na majirani zake Waarabu. Tangu kupatikana kwa silaha nyingi za hewani kama vile ndege za kijeshi na helikopta faida ya kifaru imepungua kama adui ana uwezo mkubwa hewani.
Mashindano kati ya kinga na kasi
[hariri | hariri chanzo]Tatizo moja la maendeleo ya vifaru ilikuwa uwiano kati ya kinga na mwendo. Kinga cha chuma au feleji ni nzito kinachelewesha mwendo wa mashine. Mashine inayotembea polepole hushambuliwa kirahisi na mizinga, ndege za kijeshi au vifaru vidogo vyenye mbio kubwa zaidi. Dawa yake ni kuipa injini kubwa zaidi inayoongeza uzani tena. Matumizi ya mashine nzito mno hupungua kwa sababu haupiti tena kwenye ardhi laini baada ya mvua. Vilevile hautembei tena mbali bila kufuatwa na malori yanayobeba mafuta yake kwa sababu mashine nzito hutumia mafuta mengi. Kifaru kinachokwama ni lengo nyepesi kwa maadui.
Majaribio yalifanywa kuongeza feleji mbele kifaru kinapotazama maadui lakini udhaifu wa nyuma ilitambuliwa na maadui waliojificha na kushambulia kwa nyuma. Vilevile mafundi walibuni silaha zilizoweza kukata hata feleji nene na dawa lake ni kuongeza mbio.
Mashindano kati ya malengo ya kasi na kinga kwa vifaru yalikuwa kimsingi sawa na matatizo katika kujenga manowari na yanaendelea. Uzazi mpya wa teknolojia unagundua aina mpya ya kinga lakini hii inafuatwa na aina mpya ya silaha za shambulio inayotoboa kinga.
Viungo vya Nje
[hariri | hariri chanzo]Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Kifaru (jeshi) kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |