Eujeni Mazenod

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Eujeni wa Mazenod)
Picha ya Mt. Eujeni Mazenod.

Eujeni Mazenod (kwa Kifaransa Eugène de Mazenod au kirefu Charles-Joseph-Eugène de Mazenod) (Aix-en-Provence, 1 Agosti 1782 - Marseille, 21 Mei 1861) alikuwa askofu wa Kanisa Katoliki nchini Ufaransa aliyeanzisha shirika la kimisionari maarufu kwa ufupisho O.M.I. kwa ajili ya kuinjilisha maskini.

Alitangazwa mwenye heri na Papa Paulo VI tarehe 19 Oktoba 1975, halafu mtakatifu na Papa Yohane Paulo II tarehe 3 Desemba 1995.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe aliyoiaga dunia[1].

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Eujeni alizaliwa tarehe 1 Agosti 1782 akabatizwa kesho yake.

Baba yake, Charles Antoine de Mazenod, alikuwa mmoja kati ya wenyeviti wa Mahakama ya Biashara, na mama yake alikuwa Marie Rose Joannis.

Eujeni alianza masomo yake kwenye Chuo Bourbon, lakini hayo yalikatishwa na Mapinduzi ya Kifaransa ambayo yalifilisi familia yake na kuilazimisha kukimbilia Venice, Italia.

Baadaye akawa mwanafunzi wa bweni katika Chuo cha Masharifu huko Torino. Huko alipokea sakramenti ya ekaristi na kipaimara.

Majeshi ya kimapinduzi kutoka Ufaransa yalipovamia Italia, familia ilikimbilia tena Venice, ambapo baba yake alitafuta kazi mbalimbali bila kufanikiwa.

Mama yake alirudi Ufaransa pamoja na binti yake alipoomba talaka kwa lengo la kurudishiwa mali yake iliyokuwa imetaifishwa.

Eujeni alibahatika kukaribishwa na familia Zinelli huko Venice. Padri wa familia hiyo, Bartolo Zinelli, alishughulikia malezi ya mtoto huyo akitumia maktaba kubwa ya nyumbani, ambapo Eujeni alishinda saa kadhaa kwa siku. Padri Bartolo alimuathiri pia sana kiutu na kiroho.

Kwa msukumo wa jeshi tena, Eujeni na baba yake walilazimika kukimbilia kusini, kwanza Naples kwa karibu mwaka mzima, halafu Palermo, Sicilia.

Huko Eujeni aliweza kufuata mtindo wa maisha uliolingana na usharifu wake.

Hatimaye alirudi Ufaransa na kupewa upadrisho huko Amiens mwaka 1811.

Mwaka 1816 alianzisha shirika la Missionary Oblates of Mary Immaculate.[2]

Kati ya miaka 1837 na 1861 alikuwa askofu wa Marseille, akiliangaza jimbo lake kwa maadili, mipango, mahubiri na maandishi[3].

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.