Nenda kwa yaliyomo

Korongo-nyangumi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Balaeniceps)
Mwari
Korongo-nyangumi akitembea juu ya uoto wa maji
Korongo-nyangumi akitembea juu ya uoto wa maji

Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Aves (Ndege)
Oda: Pelecaniformes (Ndege kama wari)
Familia: Balaenicipitidae (Ndege walio na mnasaba na korongo-nyangumi)
Jenasi: Balaeniceps
Gould, 1850
Spishi: B. Rex
Gould, 1850
Msambazo wa korongo-nyangumi
Msambazo wa korongo-nyangumi

Korongo-nyangumi ni ndege kubwa anayefanana na korongo wa familia Ciconiidae. Jina lake linatoka kwa umbo la kichwa chake pamoja na domo lake. Kwa sababu ya mfanano ndege huyu aliainishwa zamani katika oda ya Ciconiiformes, lakini utafiti wa kijeni ulionyesha nasaba na wari na kwa hivyo anaainishwa sasa katika Pelecaniformes.

Ndege huyu ni mrefu wenye urefu wa kawaida wa sm 110 hadi 140 na baadhi ya violezo hufikia hadi sm 152. Urefu kutoka mkia hadi domo unaweza kuanzia sm 100 hadi 140. Uzito umeripotiwa kuwa kati ya kg 4 hadi 7[1][2]. Dume ana uzito wa wastani wa kg 5.6 na ni mkubwa kuliko jike wa kawaida wa kg 4.9[3]. Mabawa ni mapana yenye urefu pamoja wa sm 230 hadi 260, bora kwa kupaa.

Sifa bainifu ya spishi hiyo ni domo lake kubwa na nono, ambayo ina rangi ya ubua mkavu na alama kijivu zisizo sahihi. Kigongo chake kilichofunuliwa (au kipimo kilicho juu ya mandibuli ya juu) ni sm 18.8 hadi 24, domo la tatu kwa urefu kati ya ndege waliopo baada ya wari na korongo wakubwa. Spishi hii inaweza kuwashinda wari katika mzunguko wa domo, hususa ikiwa domo linachukuliwa kuwa sehemu ngumu yenye keratini kama mfupa[3]. Kama wari walio nayo, mandibuli ya juu ina kigongo kali na kuishia kwa kulabu kali.

Miguu ya rangi nyeusi ni mirefu kiasi, na urefu wa tarsi kutoka sm 21.7 hadi 25.5. Miguu ya korongo-nyangumi ni mikubwa ya kipekee: kidole cha kati kinafikia urefu wa sm 16.8 hadi 18.5, ambayo huenda kusaidia spishi hiyo kusimama juu ya uoto wa majini wakati wa kuwinda. Shingo ni fupi na nene kulingana na ndege wengine wenye miguu mirefu wanaotembea majini kama vile koikoi na korongo.

Manyoya ya ndege wapevu yana rangi ya samawatikijivu huku manyoya ya kuruka ni kijivu iliyoiva kama grife. Kidari kina manyoya marefu kadhaa ambayo yana mashina meusi. Kinda ana rangi sawa ya manyoya, lakini ni kijivu iliyoiva yenye mng'ao kahawia.[3] Mara wanapozaliwa korongo-nyangumi huwa na domo la ukubwa kiasi zaidi ambalo mwanzoni lina rangi ya kijivufedha. Domo linakuwa kubwa zaidi wakati makinda wanapokuwa na umri wa siku 23 na kukua vyema kwa siku 43[3].

Korongo-nyangumi huweka mabawa yake mabapa akipaa na, kama ilivyo kwa wari, huruka na shingo iliyopindika. Kasi yake ya kupiga mabawa, kwa makadirio ya mipigo 150 kwa dakika, ni baini ya kasi ndogo zaidi ya ndege yoyote, isipokuwa spishi kubwa za korongo. Ruwaza ni kupishana mizunguko ya kupiga na kupaa ya takriban sekunde saba kila mmoja, ambayo inaweka umbali wake wa kupaa kati ya ule wa korongo wakubwa na tumbusi ya Andes (Vultur gryphus). Wakipeperushwa korongo-nyangumi hujaribu kuruka si zaidi ya m 100 hadi 500[3]. Miruko mirefu ni nadra na ni miruko michache tu zaidi ya umbali wake wa chini wa kutafuta chakula wa m 20 ambayo imerekodiwa.

Msambazo na makazi

[hariri | hariri chanzo]

Korongo-nyangumi anasambazwa katika vinamasi vya maji baridi vya katikati mwa Afrika ya kitropiki, kutoka kusini mwa Sudani na Sudani Kusini kupitia sehemu za mashariki mwa JK Kongo, Rwanda, Uganda, magharibi mwa Tanzania na kaskazini mwa Zambia. Spishi hii ni nyingi zaidi katika jimbo la West Nile na Sudani Kusini (hususa Sudd, ngome kuu ya spishi hiyo); pia ni muhimu katika maeneo manyevu ya Uganda na magharibi mwa Tanzania. Rekodi zaidi za pekee za korongo-nyangumi zimeripotiwa nchini Kenya, Jamhuri ya Afrika ya Kati, kaskazini mwa Kameruni, kusini-magharibi mwa Ethiopia na Malawi. Violezo vya uzururaji kuelekea Bonde la Okavango, Botswana na sehemu ya juu ya Mto Kongo pia zimeonekana. Msambazo wa spishi hii inaonekana kwa kiasi kikubwa sanjari na ule wa mafunjo na kambare mamba, chakula chake kikuu. Mara nyingi hupatikana katika maeneo ya uwanda wa mafuriko yaliyoingiliwa na mafunjo na matete yasiyosumbuliwa. Wakati korongo-nyangumi yuko kwenye eneo lenye maji ya kina kirefu, kitanda cha mimea inayoelea ni sharti. Pia hupatikana mahali ambapo kuna maji yenye oksijeni duni. Hii husababisha samaki wanaoishi ndani ya maji kutoka ili kupumua mara nyingi zaidi, na hivyo kuongeza uwezekano wa korongo-nyangumi kuwakamata kwa mafanikio[4]. Korongo-nyangumi haihami na ina miondoko midogo ya msimu kutokana na mabadiliko ya makazi, upatikanaji wa chakula na usumbufu wa wanadamu[3].

Michoro juu ya majabali kutoka Oued Djerat, mashariki mwa Aljeria, inaonyesha kwamba korongo-nyangumi alitokea zaidi upande wa kaskazini katika maeneo manyevu ambayo yalifunika Jangwa la Sahara la kisasa wakati wa Holocene ya Mapema[5].

Korongo-nyangumi hutokea katika vinamasi vya maji baridi vinavyofunika maeneo makubwa. Takriban maeneo manyevu yote yanayovutia spishi hiyo yana sehemu zisizosumbuliwa za Cyperus papyrus na za Phragmites na Typha. Ingawa msambazo wake kwa kiasi kikubwa unaonekana kuendana na msambazo wa mafunjo katika Afrika ya Kati, spishi hii inaonekana kuepuka vinamasi vyenye mafunjo tu na mara nyingi huvutiwa na maeneo yenye mchanganyiko ya mimea. Mara chache tu, spishi hiyo imeonekana ikitafuta chakula katika mashamba ya mpunga na mashamba yaliyofurikika[3].

Mwenendo na ekolojia

[hariri | hariri chanzo]

Korongo-nyangumi anajulikana kwa miendo yake ya polepole na tabia ya kukaa tuli kwa muda mrefu, ambayo inatokeza maelezo ya spishi kuwa "kama sanamu". Wako nyeti sana kwa usumbufu wa kibinadamu na wanaweza kuacha (kiota|viota) vyao wakitafishwa na watu. Hata hivyo, wakati wa kutafuta chakula, ikiwa uoto mnene unasimama kati yake na watu, ndege huyu anaweza kukaa. Anavutiwa na maji yenye oksijeni duni kama vile kinamasi|vinamasi na mabwawa ambapo samaki huibuka mara kwa mara ili kupumua. Kipekee kwa ndege mkubwa kama huyu, korongo-nyangumi mara nyingi husimama na kukaa kwenye mimea inayoelea, ambayo inafanya aonekane na sile-maua mkubwa, ingawa pondagundi mkubwa (Ardea goliath), ambaye ana ukubwa sawa na kutokea mahali pamoja mara kwa mara, pia anajulikana kusimama kwenye mimea ya majini. Korongo-nyangumi, ambaye ni kiwa, hutafuta chakula kwa umbali wa m 20 au zaidi kutoka kwa wengine hata mahali ambapo kuna idadi kubwa. Spishi hii hunyemelea mawindo yake kwa subira kwa jinsi ya polepole na ya kuvizia. Akiwinda, korongo-nyangumi hupiga hatua polepole sana na mara nyingi haisogei. Tofauti na ndege wengine wakubwa, spishi hii huwinda kwa kutumia macho tu na hajulikani kujihusisha na uwindaji wa kugusa. Mawindo yanapoonekana, huanzisha mgomo mkali wa haraka. Walakini, kulingana na ukubwa wa mawindo, wakati wa kushughulikia baada ya mgomo unaweza kuzidi dakika 10. Takriban 60% ya migomo hutoa mawindo. Mara kwa mara maji na mimea hunyakuriwa wakati wa mgomo na kumwagika kutoka kwenye kingo za mandibuli. Shughuli ya viboko inaweza kufaidisha korongo-nyangumi bila kukusudia, kwani viboko walio chini ya maji mara kwa mara huwalazimisha samaki kuibuka[3].[

Korongo-nyangumi hula samaki kwa kiasi kikubwa lakini ni mbuai waliohakikishiwa wa aina mbalimbali za vertebrata wa ardhioevu. Spishi za mbuawa zinazopendelea zimeripotiwa kuwa pamoja na kambaremamba-chui (Protopterus aethiopicus)[6] na samakimagamba kijivu (Polypterus senegalus)[7] na spishi mbalimbali za Tilapia na kambale[8], hizi za mwisho haswa katika jenasi Clarias. Mbuawa wengine walioliwa na ndege huyu ni pamoja na vyura, nyoka wa maji[9], mburukenge (Varanus niloticus)[10] na mamba wachanga. Mara chache zaidi makobemaji, konokono, wagugunaji na ndege wadogo wa maji wameripotiwa kuliwa[11] More rarely, the shoebill will consume snails, rodents, and small waterfowl.[12]. Kuna ripoti moja isijathibitishwa ya korongo-nyangumi waliojilisha na ndama wa lechwe kusi (Kobus leche). Kwa kuzingatia domo lake kubwa lenye kingo kali na achamo mpana, korongo-nyangumi anaweza kuwinda mbuawa wakubwa, mara nyingi akilenga mbuawa wakubwa kuliko wanaochukuliwa na ndege wengine wakubwa wanaotembea majini. Samaki wanaoliwa na ndege huyu kwa kawaida huwa katika urefu wa sm 15 hadi 50 na wana uzito wa takriban g 500, ingawa kambaremamba wa hadi m 1 wameshambuliwa. Nyoka wanaowindwa huwa na urefu wa sm 50 hadi 60 kwa kawaida. Katika Vinamasi vya Bangweulu nchini Zambia mbuawa wakuu waliolishwa kwa makinda na wazazi walikuwa kambale mumi (Clarias gariepinus)[13] na nyoka wa maji. Nchini Uganda kambaremamba na kambale walilishwa haswa kwa makinda[3]. Wakati mwingine domo kubwa hutumiwa kuchimba kwenye matope ya chini ya mabwawa ili kutoa kambaremamba kutoka kwa mashimo yao ya kuokoka majira ya ukame.

Kwa kawaida korongo-nyangumi huwa kimya, lakini hufanya maonyesho ya kugonganisha domo kwenye kiota. [3] Wakati wa kushiriki katika maonyesho haya, ndege wapevu pia wamejulikana kutamka 'muu' kama ng'ombe pamoja na milio ya juu. Makinda na wapevu wote hujishughulisha katika kugonganisha domo wakati wa msimu wa kulea kama njia ya mawasiliano. Makinda wakiomba chakula, huita kwa sauti isiyo ya kawaida kama chechevu za kibinadamu. Katika kisa kimoja ndege mpevu aliyeruka alisikika akitoa mikoromo minene, ambayo inaonekana kama ishara ya uchokozi kwa korongo marabu (Leptoptilos crumeniferus).[14]

Kuzaliana

[hariri | hariri chanzo]

Hali ya upweke ya korongo-nyangumi inaenea hadi tabia zao za kuzaliana. Kwa kawaida viota hutokea kwa chini ya viota vitatu kwa km ya mraba, tofauti na koikoi, minandi, wari na korongo ambao hujenga viota katika makoloni kwa kiasi kikubwa. Jozi ya kuzaliana hutetea kwa nguvu eneo la km2 2 hadi 4 dhidi ya korongo-nyangumi wengine. Ujenzi wa kiota mara nyingi huanza karibu na mwisho wa majira ya mvua ili mayai yatatoa makinda karibu na mwanzo wa majira ya mvua yanayofuata. Wazazi wote wawili hushiriki katika kujenga kiota kwenye jukwaa linaloelea baada ya kuondoa eneo la takriban m 3 kwa upana. Jukwaa kubwa na bapa la kutagia mara nyingi huzamishwa kwa kiasi ndani ya maji na linaweza kuwa na kina cha m 3. Kiota chenyewe kina upana wa m 1 hadi 1.7. Kiota na jukwaa zote mbili hutengenezwa kwa mimea ya majini. Mayai meupe 1-3 hutagwa. Mayai haya hupima mm 80 hadi 90 kwa 56 hadi 61 na yana uzito wa karibu g 164. Uatamiaji huchukua takriban siku 30. Wazazi wote wawili huatamia, kuweka kivuli, kulinda na kulisha kinda, ingawa majike labda huwa wasikivu zaidi. Vipande vya chakula hutapikwa kutoka kwa koromeo moja kwa moja katika domo la kinda. Korongo-nyangumi hulea zaidi ya kinda mmoja mara chache, lakini wataangua zaidi. Kwa kawaida makinda wachanga hufa na hulengwa kama "kisaidizi" ikiwa kinda mkubwa atakufa au ni dhaifu. Kuondoka kiota hufikiwa kwa takriban siku 105 na ndege mchanga anaweza kuruka vizuri kwa siku 112. Walakini, bado analishwa kwa mwezi au zaidi baada ya hii. Itachukua ndege mchanga miaka mitatu kabla ya kukomaa kikamilifu kingono.[14]

Korongo-nyangumi hupatikana kwa ugumu wakati wa kukaa kwenye kiota, kwa hivyo ni lazima kamera ziwekwe ili kuwatazama kutoka mbali ili kukusanya data za tabia. Kuna faida kwa ndege ambao wanaanza kuzaa mapema, kwani makinda hutunzwa kwa muda mrefu.[18]

Hali na hifadhi

[hariri | hariri chanzo]

Idadi ya ndege hawa inakadiriwa kuwa kati ya ndege 5,000 na 8,000, wengi wao wakiishi katika vinamasi vya Sudani Kusini, Uganda, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia[14]. Pia kuna idadi kubwa katika ardhioevu ya Malagarasi nchini Tanzania[15]. BirdLife International imemwainisha kuwa na Hali ya Hatari huku matishio makuu yakiwa uharibifu wa makazi, usumbufu na uwindaji. Ndege huyu ameorodheshwa chini ya Kiambatisho II cha Mkataba wa Biashara ya Kimataifa ya Spishi zilizo Hatarini za Wanyama na Mimea ya Porini (CITES)[16]. Uharibifu na udhalili wa makazi, uwindaji, usumbufu na ukamataji haramu ni mambo yanayochangia kupungua kwa spishi hii. Kilimo na malisho ya ng'ombe pia yamesababisha upotezaji mkubwa wa makazi. Jamii za kiasili zinazozunguka makazi ya korongo-nyangumi hukamata mayai na makinda wao kwa ulaji wa kibinadamu na kwa biashara. Mioto ya mara kwa mara kusini mwa Sudani iliyowekwa kwa ajili ya kupata malisho inachangia kupoteza makazi. Hatimaye, maji ya vinamasi nchini Sudani yanachururishwa kwa ajili ya ujenzi wa mfereji wa karibu unaoruhusu udhibiti wa njia za maji zilizo karibu[17].

  1. "Balaeniceps rex" (kwa Kijerumani). 19 Julai 2011. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 19 Julai 2011. Iliwekwa mnamo 6 Mei 2020. {{cite web}}: More than one of |accessdate= na |access-date= specified (help); More than one of |archivedate= na |archive-date= specified (help); More than one of |archiveurl= na |archive-url= specified (help)CS1 maint: date auto-translated (link)
  2. Stevenson, Terry; Fanshawe, John (2002). Field guide to the birds of East Africa : Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi. London: T & A D Poyser. ISBN 0-85661-079-8. OCLC 47150215.
  3. 3.0 3.1 3.2 3.3 3.4 3.5 3.6 3.7 Hancock, James A.; Kushan (1992). Storks, ibises and spoonbills of the world. London: Academic Press/Harcourt Brace Jovanovich, Publishers. ISBN 0-12-322730-5. OCLC 26933579.
  4. Steffen, Angie. "Balaeniceps rex (shoebill)". Animal Diversity Web (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 6 Mei 2020.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  5. Oeschger, E. (2004). "Sahara - Algeria - Rock Art in Oued Derat and the Tefedest Region" (PDF). Adoranten (kwa English). 2004: 5–19.{{cite journal}}: CS1 maint: unrecognized language (link)
  6. "Shoebill - Facts, Diet, Habitat & Pictures on Animalia.bio".
  7. "Shoebill - Facts, Diet, Habitat & Pictures on Animalia.bio".
  8. "Shoebill - Facts, Diet, Habitat & Pictures on Animalia.bio".
  9. "Balaeniceps rex shoebill". animaldiversity.org.
  10. "Shoebill - Facts, Diet, Habitat & Pictures on Animalia.bio".
  11. https://animaldiversity.org/
  12. "Shoebill - Facts, Diet, Habitat & Pictures on Animalia.bio".
  13. Tomita, Julie (2014). "Challenges and successes in the propagation of the Shoebill Balaeniceps rex: with detailed observations from Tampa's Lowry Park Zoo, Florida". International Zoo Yearbook. 48 (1): 69–82. doi:10.1111/izy.12038.
  14. Williams, John G.; Arlott, N (1980). A field guide to the birds of East Africa (tol. la Rev.). London: Collins. ISBN 0-00-219179-2. OCLC 7649557.
  15. John, Jasson; Nahonyo, Cuthbert; Lee, Woo; Msuya, Charles (Machi 2013). "Observations on nesting of shoebill Balaeniceps rex and wattled crane Bugeranus carunculatus in Malagarasi wetlands, western Tanzania". African Journal of Ecology. 51 (1): 184–187. doi:10.1111/aje.12023.{{cite journal}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  16. "Appendices I, II and III". Convention on International Trade in Endangered Species of Wild Flora and Fauna. 14 Oktoba 2010. Iliwekwa mnamo 20 Desemba 2019.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  17. Muir, A.; King, C. E. (Januari 2013). "Management and husbandry guidelines for Shoebills Balaeniceps rex in captivity: Shoebill: Management and Husbandry Guidelines". International Zoo Yearbook (kwa Kiingereza). 47 (1): 181–189. doi:10.1111/j.1748-1090.2012.00186.x.{{cite journal}}: CS1 maint: date auto-translated (link)