Zama za Mawe

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mawe yaliyochongwa kuwa na kona kali kwa matumizi kama kisu.
Mtu wa zama za mawe akikata mti.

Zama za Mawe (pia: Mhula wa mawe[1]) zilikuwa kipindi kirefu cha historia ya awali ya binadamu. Jina hilo linatokana na kwamba wakati huo watu walitumia vifaa vya mawe kwa shughuli zao za kila siku.

Utamaduni wa watu mwanzoni mwa zama za mawe[hariri | hariri chanzo]

Mwanzoni watu walikuwa wawindaji-wakusanyaji, yaani walidumisha maisha yao kwa kukusanya matunda, mizizi na kuwinda wanyama.

Kwa umbile na akili yake binadamu ana uwezo wa kuwinda wanyama wakubwa kama chakula na kutumia ngozi yao kama mavazi ya kujikinga dhidi ya baridi.

Lakini meno na makucha yake hayafai kupasua ngozi ya mnyama mkubwa au kukata nyama yake vipande-vipande akitaka kubeba windo hadi mahali penye familia yake. Vilevile makucha hayafai sana kuchimba mizizi kwa chakula.

Hapo binadamu aliweza kutumia vitu vinavyopatikana kiasili katika mazingira: jiwe lenye kona kali, tawi la mti lenye ncha kali pamoja na vipande vya mifupa. Hivyo vyote vilisaidia shughuli za kuchimba, kupasua na kukata.[2]

Kuna mabaki mengi ya mawe yaliyochongwa kwa matumizi kama vifaa na mabaki hayo yamekuwa msingi wa jina "zama za mawe". Vifaa hivyo na mabadiliko yake vinaonyesha maendeleo katika maisha ya binadamu na kuongezeka kwa uwezo wake wa kupambana na mazingira yake.

Kwa hiyo ni kipindi cha matumizi ya mawe yaliyochongwa kuwa vifaa baada ya kipindi ambako watu walitumia fimbo tu au mawe katika hali asilia na kabla ya kipindi ambapo watu walielewa namna ya kutumia metali.

Kifaa cha mawe sahili - zama za mawe ya kale
Shoka la mkononi - bapa pande mbili (mwishoni mwa Zama za mawe ya kale) - inaonyeshwa kutoka mitazamo mbalimbali

Vipindi vya zama za mawe[hariri | hariri chanzo]

Wataalamu wa akiolojia wametambua ya kwamba vifaa vya mawe vinaonyesha tabia tofautitofauti.

  • Kuna vifaa sahili sana kama jiwe lililogongwa mara moja ili kipande kivunjike na ncha kali ipatikane.
  • Kuna pia vifaa vya mawe vinavyoonyesha maendeleo zaidi; vilifanyiwa kazi kwa siku kadhaa kiangalifu ili kunyoshwa, kung'arishwa na kutobolewa kwa kuweka pini.

Kutokana na tofauti kubwa katika hali ya vifaa vya mawe wataalamu wanaona ya kwamba wanaonyesha historia ndefu ya maendeleo ya teknolojia ya kushughulikia jiwe ambako watu walianza kwa vifaa sahili na kuendelea kujifunza zaidi na kuboresha matokeo ya juhudi zao.

Kwa hiyo wataalamu wengi wanatofautisha:

Si tofauti katika ubora wa vifaa pekee, lakini kuna pia dalili nyingine zinazoonyesha ya kwamba watu walibadilisha maisha yao, namna ya kujipatia chakula na makazi.

Kila mtu aliweza kugonga jiwe dhidi ya jiwe hadi ncha kali ilipatikana. Lakini mashoka ya mawe yaliyohitaji siku za kazi makinifu yanaonyesha kuwepo kwa jamii iliyokuwa na mafundi wa pekee walioweza kunyosha ufundi wao wakilishwa na wengine ni pia dalili ya biashara iliyofanywa hasa tukikuta vifaa vya jiwe fulani katika maeneo ambako jiwe hili halipatikani kiasili.

Pamoja na matokeo mengine ya utafiti wa akolojia, kama vile mabaki ya makaburi, vyombo vya ufinyanzi, nyumba na vifaa vingine, wataalamu waliweza kupata picha ya undani zaidi kuhusu maisha na jamii ya watu wa zamani zile.

Teknolojia ya kupunguza jiwe hadi kupata kisu chembamba - zama za mawe ya kati (Levallois)
Matumizi ya ncha ya jiwe kwenye mkuki

Vifaa vya mawe[hariri | hariri chanzo]

Zama za mawe ya kale[hariri | hariri chanzo]

Vifaa vya kwanza vilikuwa mawe yaliyokatwa upande mmoja ili kuwa na kona kali moja. Hatuwezi kujua kwa uhakika tukiona jiwe la aina hii kama kama ilikuwa tokeo la mgongano wa mawe katika mkondo wa maji mtoni au kutokana na kuanguka kwa jiwe kutoka mlimani au kama jiwe limepigwa kwa kusudi kwa jiwe lingine kwa shabaha ya kupata kona kali. Lakini mawe haya yalifaa kutumiwa kwa kukata pia si vigumu kuvitengeneza.

Mifano ya kale kabisa ya mawe yaliyogongwa kwa mawe mengine kwa kusudi la kupata kona kali zimepatikana katika eneo la ziwa Turkana (leo nchini Kenya) yalitegenezwa miaka milioni 3.3 iliyopita[3].

Ngazi iliyofuata ni mawe yaliyofanyiwa kazi zaidi hadi kuwa "shoka la mkononi". Hapo jiwe la kufaa lilipigwa na kupunguzwa pande zote mbili hadi kuwa na bapa pande mbili. Sehemu ya juu ilibaki bila ukali kwa kuishikilia mkononi. Kuna mahali ambako mabaki mengi ya mashoka haya ya mkononi yamepatikana katika hali mbalimbali: mawe yaliyopigwa kiasi, mawe yaliyovunjika vibaya na kutupwa, vipande vidogo vilivyopasuliwa wakati wa kuipa shoka umbo lake na kadhalika. Mahali pale panatazamwa kama karakana au viwanda vya kutengeneza vifaa vya mawe. Mahali mashuhuri katika Afrika ya Mashariki ni bonde la Isimila (karibu na Iringa, Tanzania ya leo).

Zama za mawe ya kati[hariri | hariri chanzo]

Kipindi hiki kinatazamwa kilianza miaka 300,000 iliyopita na kudumu hadi miaka 25,000 - 50,000 [4] iliyopita.

Mabamba makali ya mawe yamefungwa katika ubao wa mundu ya kukatia majani au mazao

Kipindi hiki kinaonyesha maendeleo ya teknolojia. Watu walianza kutumia pia vipande vidogo vikali vilivyopatikana wakati wa kupunguza jiwe. Vibanzi vikali vya mawe vilifungwa sasa kwenye pini ya ubao kwa gundi la miti. Kwa njia hii vifaa kama kisu, chusa au mundu vilipatikana. [5]

Matatizo ya lugha ya "zama za mawe"[hariri | hariri chanzo]

Zama za mawe zilikuwa vipindi virefu sana vya miaka elfu nyingi. Wataalamu wamegawanya zama hizo katika vipindi mbalimbali kama Zama za mawe za kale na Zama za mawe za kati. Tofauti hizo zinaonekana kuwa na msingi, lakini wataalamu wa siku hizi wanaona ya kwamba mgawanyo huu ulitazama zaidi historia ya Ulaya isiyolingana na historia ya sehemu nyingine za dunia.

Tatizo kuu ni kwamba ni kipindi cha teknolojia bila kuangalia pande nyingine za maendeleo ya kibinadamu.

Kwa mfano chuma hakikutumiwa huko Amerika hadi karne ya 16 na huko Pasifiki hadi karne ya 17. Hata hivyo jamii za Amerika kama Azteki au Wainka walikuwa na teknolojia nyingine mbalimbali na waliweza kudumisha miji mikubwa kushinda miji ya Ulaya ya wakati ule.

Basi, lugha ya "zama za mawe" imekuwa kawaida duniani na wataalamu wanaendelea kuitumia wakijua kasoro zake kwa sababu hadi sasa hakuna mawazo ya kufaa zaidi.

Picha[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. "Mhula wa mawe" ni pendekezo la Kamusi ya Historia (TUKI 2004); hata hivyo Zama za Mawe ni neno la kawaida zaidi likiwa istilahi inayofundishwa kwenye shule za msingi za Tanzania.
  2. Uwezo wa kutumia vitu kama fimbo kama kifaa cha kujipatia chakula umetazamwa pia kwa wanyama kadhaa, kwa mfano ndege na sokwe - linganisha Sokwe wanatengeneza na kutumia vifaa na Matumizi ya vifaa na ndege Archived 20 Juni 2015 at the Wayback Machine..
  3. 3.3-million-year-old stone tools from Lomekwi 3, West Turkana, Kenya, katika jarida la Nature 21 May 2015
  4. Katika eneo kubwa la bara Afrika maendeleo yalikuwa tofauti kati ya sehemu mbalimbali. Pamoja na makadirio ya umri ya vifaa vya kale sana hii ni elezo kwa kutaja mwisho wa kipindi hiki kuwa na tofauti ya miaka mielfu kwa bara la Afrika.
  5. • McBrearty, Sally and Alison A. Brooks. 2000. "The revolution that wasn't: A new interpretation of the origin of modern human behaviour" Journal of Human Evolution 39:453–563.

Kujisomea[hariri | hariri chanzo]

  • Barham, Lawrence; Mitchell, Peter (2008). The First Africans: African Archaeology from the Earliest Toolmakers to Most Recent Foragers. Cambridge World Archaeology. Oxford: Oxford University Press. 
  • Belmaker, Miriam (March 2006). Community Structure through Time: 'Ubeidiya, a Lower Pleistocene Site as a Case Study (Thesis). Paleoanthropology Society. Archived from the original on 2011-04-30. Retrieved 2015-04-15. 
  • Clark, J. Desmond (1970). The Prehistory of Africa. Ancient People and Places, Volume 72. New York; Washington: Praeger Publishers. 
  • Deacon, Hilary John; Deacon, Janette (1999). Human beginnings in South Africa: uncovering the secrets of the Stone Age. Walnut Creek, Calif. [u.a.]: Altamira Press. 
  • Piccolo, Salvatore (2013). Ancient Stones: The Prehistoric Dolmens of Sicily. Abingdon (UK): Brazen Head Publishing. 
  • Rogers, Michael J.; Semaw, Sileshi (2009). "From Nothing to Something: The Appearance and Context of the Earliest Archaeological Record". In Camps i Calbet, Marta; Chauhan, Parth R. Sourcebook of paleolithic transitions: methods, theories, and interpretations. New York: Springer. 
  • Schick, Kathy D.; Nicholas Toth (1993). Making Silent Stones Speak: Human Evolution and the Dawn of Technology. New York: Simon & Schuster. ISBN 0-671-69371-9. 
  • Shea, John J. (2010). "Stone Age Visiting Cards Revisited: a Strategic Perspective on the Lithic Technology of Early Hominin Dispersal". In Fleagle, John G.; Shea, John J.; Grine, Frederick E.; Boden, Andrea L.; Leakey, Richard E,. Out of Africa I: the First Hominin Colonization of Eurasia. Dordrecht; Heidelberg; London; New York: Springer. pp. 47–64. 
  • Scarre, Christopher (ed.) (1988). Past Worlds: The Times Atlas of Archaeology. London: Times Books. ISBN 0-7230-0306-8. 

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Zama za Mawe kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.