Nenda kwa yaliyomo

Tarantula

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Tarantula
Tarantula-miti (Encyocratella olivacea)
Tarantula-miti (Encyocratella olivacea)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia
Faila: Arthropoda
Nusufaila: Chelicerata
Ngeli: Arachnida
Oda: Araneae
Nusuoda: Opisthothelae
Oda ya chini: Mygalomorphae
Familia ya juu: Theraphosoidea
Familia: Theraphosidae
Thorell, 1869
Ngazi za chini

Nusufamilia 15:

Tarantula ni spishi za buibui katika familia Theraphosidae wa nusuoda Opisthothelae. Spishi za nusufamilia Harpactirinae huitwa bui-nyani. Spishi nyingi ni kubwa hadi kubwa sana na zote zina manyoya marefu mengi. Kwa kawaida huwinda kwa kuvamia mawindo.

Ingawa spishi fulani za tarantula zinaweza kuwa ndogo kama mm 5, takriban zote ni kubwa hadi kubwa sana, Kwa kweli, spishi kadhaa zinaweza kufikia sm 11 zenye upana wa miguu wa sm 30 na uzito wa g 170. Chonge zinaweza kufikia urefu wa sm 3.8.

Kama buibui wote, tarantula wana miguu 8, macho 8 na sehemu mbili za mwili, kefalothoraksi au prosoma na fumbatio au opisthosoma, zilizounganishwa na pediseli. Chonge zinaelekea chini wima badala ya chonge zinazopitana za buibui wengi wengine. Pia, kinyume na wale wa mwisho, wana chuchu mbili au nne za kukalidi badala ya sita.

Sumu na manyoya ya kuchomea

[hariri | hariri chanzo]

Tarantula wote wana sumu ambayo hutumia kupooza au kuua mawindo yao. Kwa kawaida sumu hiyo haisababishi zaidi ya hisia inayowaka kwa wanadamu wakati wanaumwa. Walakini, spishi nyingine zina sumu kali zaidi ambayo inaweza kusababisha usumbufu mkubwa unaodumu siku kadhaa. Dalili za kawaida ni mikakamao na mikazo mikali ya misuli. Bui-nyani mwekundu (Pelinobius muticus) anaweza kusababisha maruerue mabaya. Pamoja na sumu, protini nyingine huingizwa pia na hizi zinaweza kusababisha athari za mzio ambazo zinaweza kutisha maisha. Vidonda vya kuchomwa vinaweza kuambukizwa na bakteria ikiwa vidonda havitasafishwa vizuri.

Spishi za Dunia ya Kale hutukuta sana na kuwa na haraka kwa kushambulia. Zaidi ya hayo wana sumu kali sana. Kabla ya kuuma huchukua mkao wa kutishia kwa kunyanyua prosoma yao, kuinua miguu ya mbele juu na kupanua chonge zao. Spishi fulani hutoa pia sauti ya kuchata kwa njia ya kufikicha manyoya magumu kwenye kelisera zao.

Spishi za Dunia Mpya hazina haraka sana kuuma. Badala ya hiyo hutumia manyoya maalum kwenye opisthosoma yao inayoitwa manyoya ya kuchomea, ambayo hutumika kama kinga dhidi ya mbuai. Wanaweza kuyatupa kuelekea adui kwa miguu yao au kuyasugua dhidi ya lengo. Manyoya hayo yana vizari na hutumika ili kuwasha. Mara nyingi yanaua vipanya. Watu wengi ni nyeti kwa manyoya hayo na kupata kuwasha kali na mbati. Kuyavuta na kuingia kwao machoni inapaswa kuepukwa kabisa. Lau kama manyoya yanaposhindwa kumzuia mbuai, tarantula hawa huamua kuuma.

Tarantula hula kila kitu wanachoweza kupata porini na kilicho kidogo kuliko wao. Kwa kawaida invertebrata wadogo hushikwa, kama wadudu, lakini vertebrata wadogo, kama vipanya na watambaazi, huliwa pia. Wanaweza kukamata ndege wadogo lakini hii imeripotiwa mara chache tu. Kinyume na buibui wengi wengine tarantula hawafanyi mitandao. Spishi kadhaa hufunika makao kwa tabaka nyembamba ya hariri na spishi nyingine hunyumbua nyuzi za kukwaza ili kugundua mawindo, lakini mawindo huwa yanachupiwa kila wakati. Manyoya ya tarantula yana jukumu kubwa katika hiyo. Sio tu ukubwa na mahali pa mawindo, lakini pia umbali umedhamiriwa na machunguzi ya manyoya yenye hisia. Aghalabu hayo yapo miguuni lakini pia kwenye sehemu za kinywa. Tarantula huingiza sumu na maji ya mmeng'enyo ndani ya mawindo ili kumpooza na mtawalia kumyeyusha, na kisha kufyonza kioevu kilichomo. Kilichobaki cha mawindo ni kitonge kinachofanana na kidonge kilichotapikwa na bundi k.m. chenye sehemu ngumu zilizovunjika. Machunguzi ya buibui kifungoni yalionyesha kuwa huweka vitonge hivi kila mara mahali pamoja. Takamwili za buibui ni kioevu na huondoka buibui kupitia ncha ya fumbatio. Tarantula-miti wanaweza kufyatua takamwili kwa lengo ikiwa watafadhaika.

Tarantula, wachanga haswa, huwa na maadui wengi, kama ndege, watambaazi na wanyama wengine ambao huishi kwa kutegema invertebrata wadogo. Violezo vipevu mara nyingi hawana maadui wengi sana, lakini mamalia fulani wakubwa mbuai kama rakuni, nyegere, vinyegere na vicheche hufukua tarantula kabla ya kuwaua na kuwala. Maadui muhimu wa buibui wengi, pamoja na tarantula, ni nyigu wa familia Pompilidae wanaoitwa wauabuibui mara nyingi. Baada ya buibui kugunduliwa hupoozwa na kuzikwa kwenye kishimo au kufichwa katika sehemu za mimea kama mashina yenye matundu. Kisha nyigu hutaga mayai yake na baadaye mabuu hula buibui kutoka ndani akiwa hai. Wauabuibui wengi huwinda buibui wadogo, lakini spishi kadhaa zimetabahari katika tarantula. Mifano ni nyigu wa jenasi Hemipepsis (spishi kadhaa katika Afrika ya Mashariki).

Spishi za Afrika ya Mashariki

[hariri | hariri chanzo]